Katika kuonesha kwamba wanaunga mkono suala la elimu bora nchini Taasisi ya Teacher's Junction imeandaa mashindano kwa shule za binafsi nchini ambapo wanafunzi wa darasa la nne, sita la saba watafanya mitihani ya kujipima nguvu lengo likiwa ni kuongeza ufanisi baina ya wanafunzi hao na pia kuwarahisishia walimu kujua wapi wanapaswa kuongeza nguvu.
Mashindano hayo yamepangwa kufanyika kuanzia Februari 28 hadi Machi 1 na kushirikisha takribani shule 120 nchini.
Akizungumza na wandishi wa habari leo, Afisa Mradi wa taasisi hiyo, Njama Salum alisema walianzisha mradi huo ili kuongeza kiwango cha elimu nchini kwa wanafunzi wa shule za msingi lakini pia wakiwa na mpango wa kupeleka mradi huo hadi kwenye shule za Sekondari.
" Kiu ya taasisi yetu ni kuona kiwango cha elimu kinaongezeka nchini, hivyo kwa kushirikiana na wadau wa elimu hasa wamiliki wa shule tukaja na wazo hili la kufanya mashindano ambayo tunaamini yanawajenga wanafunzi kuanzia kiakili hadi kujiamini pale wanapofanya mitihani ya Kitaifa.
" Kikubwa tunatoa zawadi za medali kwa wanafunzi wanaofanya vizuri lakini shule ambazo zitafanya vizuri tunatoa zawadi za ngao. Na mitihani hii hufanyika mara tatu kwa mwaka ambapo kwa kuanzia tunaanza mwezi Machi kisha tutafanya mwingine Mei halafu Agosti tutafanya mwingine," alisema Njama.
Alisema tayari washapata zawadi lakini bado anatoa fursa kwa wadau wengine wa elimu kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono ili kuweza kuzalisha kizazi bora cha vijana wenye elimu ambao watakuja kuwa msaada mkubwa kwa Taifa hapo baadaye.
Akizungumzia sababu za kutohusisha Shule za Serikali, Njama alisema sio kwamba wamezitenga shule hizo lakini wao kama taasisi waliangalia ni wapi wanaweza kupenyeza wazo lao kwa haraka zaidi na kwamba taratibu za kuonana na viongozi wa kiserikali ili kuangalia uwezekano wa kupeleka mradi huo kwenye shule hizo unafanikiwa kusudi kila mwanafunzi nchini aweze kunufaika nao.
Kwa upande mwingine Njama alisema taasisi yake pia imekuwa ikisaidia walimu ambao wapo mitaani bila ajira kwa kuwatafutia kazi kwenye shule za binafsi ambazo wana ushirika nazo lengo likiwa ni kumaliza tatizo la ajira nchini.
" Sisi pia tunasaidia vijana wenzetu ambao wana taaluma ya ualimu ambao wapo mitaani ambapo kwa mwaka uliopita zaidi ya vijana 356 ambao wana taaluma ya ualimu tuliwatafutia kazi katika shule mbalimbali nchini," alisema Njama.
No comments:
Post a Comment