Saturday, 20 January 2018

MATATIZO YA MOYO YANAVYOSABABISHA VIFO-5


MAKALA haya maalumu lengo lake ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba ili kupata ufahamu zaidi kuhusu kuimarisha afya zetu na jamii nzima kwa ujumla. Leo tunaendelea kujadili magonjwa ya moyo na tutaelezea tatizo la tundu katika kuta za chini za moyo.
Endelea: Tundu katika kuta za chini za moyo Katika muendelezo wa magonjwa ya moyo, leo tutazungumzia ugonjwa unaojulikana kama tundu katika kuta za ventrikali za moyo au kwa kitaalamu Ventricular Septal Defect (VSD), tatizo ambalo hutokea mara nyingi ambapo watoto wawili hadi sita kati ya 1,000 huzaliwa na tatizo hilo.

Dk. Marise Richard anasema tundu katika kuta za chini za moyo au VSD ni pale panapokuwepo na uwazi katika sehemu ya kuta ya septum inayotenganisha chemba za ventrikali ambazo ni chemba za chini za moyo.

“Pale moyo unapoanza kuumbika huanza kama bomba lililo wazi na kuendelea kujigawa katika sehemu
mbalimbali na kuunda kuta. “Iwapo kitendo hicho hakitatekelezeka ipasavyo, hutokea uwazi katika kuta ya septum kwenye chemba za chini,” anasema Dk. Richard.

Kuwepo tundu hilo huruhusu damu yenye oksijeni kupita
kutoka chemba ya kushoto ya chini ya moyo na kuingia katika chemba ya kulia ya chini ya moyo, badala ya kuingia kwenye mshipa wa aorta na kuelekea nje ya moyo kama inavyotakiwa.

Tundu la VSD linaweza kuwa dogo, la kati au kubwa. Tundu dogo katika kuta za chini za moyo huruhusu damu ndogo kutoka upande mmoja wa moyo kwenda wa pili, hivyo haliathiri utendaji wa kawaida wa moyo na kwa kawaida huwa halihitaji matibabu maalumu.

Anasema matundu ya aina hiyo huziba yenyewe wakati moyo unapoendelea kukua kipindi cha utotoni. Matundu yenye ukubwa wa kati na kubwa katika kuta za chini za moyo huruhusu kiwango kikubwa zaidi cha damu kupenya kutoka upande mmoja wa moyo kwenda mwingine, na mara nyingi huhitajia matibabu maalumu.

Dk Richard anafafanua kuwa watoto wenye tundu dogo katika moyo, huweza kukua bila matatizo yoyote, wakati wale wenye tundu kubwa huanza kuonesha dalili mapema. Vifuatavyo ni vihatarishi ambavyo vinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na tundu katika kuta za chini za moyo.

1) Maambukizi ya rubella katika kipindi cha ujauzito.

2) Ugonjwa wa kisukari cha wakati wa ujauzito ambao haujadhibitiwa

3) Matumizi ya pombe, dawa za kulevya na baadhi ya dawa za hospitali katika kipindi cha ujauzito pia huweza kusababisha mtoto azaliwe na tundu katika kuta za chini za moyo.

Mpenzi msomaji, ninajua unajiuliza je, mtoto anayezaliwa na tundu katika kuta za chini za moyo huwa na dalili gani? Kama nilivyosema iwapo tundu ni dogo huwa halina dalili yoyote na pale mtoto anapoendelea kukua tundu hilo hujifunga lenyewe. Lakini tundu likiwa kubwa, ijapokuwa mtoto anayezaliwa huwa haonyeshi dalili yoyote katika kipindi hicho, lakini baadaye huwa na dalili zifuatazo.

1) Rangi ya ngozi, midomo na kucha hubadilika na kuwa ya bluu.

2) Kunyonya au kula kwa shida sana, na pia ukuaji wa shida.

3) Kupumua kwa shida.

4) Kuchoka haraka.

5) Kujaa miguu na kuvimba tumbo.

6) Kuwa na mapigo ya moyo ya haraka

7) Anapopimwa mtaalamu huweza kusikia ishara ya ongezeko la sauti ya ziada ya mapigo ya moyo wa mtoto hali ambayo wataalamu huiita holosystolic murmur kwa kutumia kifaa cha hupima mapigo ya moyo. Dk Richard anasema madhara ambayo yanaweza kusababishwa na tundu katika kuta za chini za moyo ni Eisenmenger syndrome.

Hali ambayo hutokea pia pale mtu anapokuwa na tundu katika kuta za juu za moyo. Tatizo hili hutokea wakati mtiririko wa damu unapoongezeka kutoka kushoto kwenda kulia kupitia tundu katika kuta za moyo, suala ambalo huongeza mtiririko wa damu katika mishipa ya mapafu na kusababisha shinikizo la damu katika mapafu. Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment