Saturday, 20 January 2018

Chadema kugombea Kinondoni na Siha

 Wakati naibu katibu mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu akichukua fomu ya kuwania ubunge wa Kinondoni, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameeleza sababu zilizowafanya kurejea katika uchaguzi wa Februari 17.

Mwalimu na mwenzake wa Siha, Elvis Mosi walipitishwa na Kamati Kuu ya Chadema jana kugombea ubunge wa majimbo hayo huku Mbowe akisema, “hiki ni chama cha siasa si zege inayoendeshwa na matamanio na ushawishi wa wananchi.”

Chadema na vyama vinavyounda Ukawa- NLD, CUF, NCCR Mageuzi- pamoja na Chaumma na ACT Wazalendo vilisusia uchaguzi mdogo wa ubunge wa Longido, Songea Mjini na Singida Kaskazini uliofanyika Januari 13 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoridhishwa na mazingira ya uchaguzi wa udiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba 26.

Vyama hivyo viliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha uchaguzi huo ili kutoka fursa ya kukutana na kufanya tathmini ya mazingira ya uchaguzi huo jambo ambalo tume hiyo ililipinga ikisema inasimamia sheria.

Jana, Mbowe alisema walipotangaza kutoshiriki uchaguzi wa Januari 13 walitoa sababu za kutoridhishwa na uchaguzi wa madiwani wa kata 43. “Hatukusema kwamba hatutashiriki kabisa uchaguzi hapana, tulitoa sababu kuwa hatukuridhishwa na uchaguzi wa zile kata 43. Bila shaka mmeona wenyewe hata uchaguzi ulivyokuwa, kama haukuwepo na hata vyama vingine vilivyoshiriki kama havikuwepo vile,” alisema mbunge huyo wa Hai.

“Kilio chetu kimesikika ndani na nje ya nchi, kimesikika kwa wananchi na kwa hatua hiyohiyo tumeona hatutawatendea haki wananchi wa Kinondoni na Siha ambao wamewekewa wagombea ambao hawawataki na hilo kila mtu analijua.”

Mgombea wa CCM aliyepitishwa kugombea Jimbo la Kinondoni ni Maulid Mtulia, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CUF kabla ya kuhamia chama tawala kwa madai ya kuunga mkono utendaji kazi wa Rais John Magufuli. Katika Jimbo la Siha, chama tawala kimemuweka Dk Mollel aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, lakini akakihama chama hicho na kujiunga CCM kwa madai ya kuunga mkono utendaji kazi wa Rais Magufuli.

Mbowe alisema, “Tunarudi katika uchaguzi, vyombo vinavyopaswa kusimamia haki vifanye hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vingine vyote, hatutaidai tena haki kwa kupiga magoti hivyo watekeleze majukumu yao ipasavyo.”

Alipoulizwa ilikuwaje wakampitisha Mwalimu ambaye hakushiriki kura za maoni, Mbowe alisema utaratibu wa kura ya maoni ndani ya Chadema haupo kikatiba, wanaamini maridhiano ndiyo njia sahihi ya kutokukigawa chama.

“...Unajua unapofanya kura za maoni unaweza kuwa na makundi mawili na adui yako akayatumia makundi hayo kufanikisha kumpata mtu ambaye ni dhaifu, kwa hiyo Kamati Kuu imeyaona hayo na ililiona hilo Kinondoni ndiyo maana ikamteua Mwalimu,” alisema Mbowe

Vuguvugu laisukuma

Wakati Mbowe akitoa sababu hizo, baadhi ya watu waliojitokeza kuomba kuteuliwa kugombea ubunge wa Kinondoni walisema vuguvugu la kuanzisha mchakato wa kuchukua fomu limesaidia chama hicho kushiriki uchaguzi huo mdogo.

Vuguvugu hilo lilitokana na Chadema Wilaya ya Kinondoni kutoa ruhusa kwa wanachama wao kutangaza nia ya kugombea jimbo hilo kisha mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa uliofanyika Januari 16.

Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki, mkurugenzi wa mambo ya nje na itifaki wa Chadema, John Mrema alinukuliwa akisema msimamo wa Ukawa wa kutoshiriki uchaguzi wa majimbo ya Siha na Kinondoni haujabadilika na kwamba wameunda kamati ndogo inayofanya utafiti kuhusu mchakato huo.

Alisema hata mchakato wa kuchukua fomu uliokuwa unafanywa na ngazi hiyo ya wilaya haukuwa na baraka za ngazi za juu.

Pamoja na hayo, mchakato wa kura za maoni Kinondoni uliendelea kwa wanachama saba ambao ni David Assey, Nicholus Agrey, Rose Moshi, Mustafa Muro, Ray Kimbitor, Juma Uloleulole na Mozah Ally kupigiwa kura.

Katika mchakato huo wa kura za maoni, Kimbitor aliibuka kidedea kwa kuwabwaga wenzake na baada ya kumalizika viongozi wa wilaya walisema wanayapeleka majina hayo yote saba katika kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichoketi jana ili kupata baraka na kusubiri uteuzi wa mgombea mmoja kutoka katika chombo hicho cha uamuzi.

Akizungumzia uamuzi huo wa Kamati Kuu, Kimbitor ambaye pia ni Diwani wa Hananasif alisema shida yao ni kuona Chadema inashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na kuna dalili za chama hicho kuibuka mshindi kutokana na misingi bora iliyojiwekea.

“Kila mtu anajua kulikuwa na sintofahamu Chadema kushiriki au kutoshiriki. Ndiyo maana sisi tulianzisha lile vuguvugu la kuchukua fomu ndani ya chama na hatimaye limezaa matunda kwa chama kuingia katika uchaguzi huu,” alisema Kimbitor.

Katibu wa Chadema Mkoa Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema Kamati Kuu ilipelekewa majina tisa na jina la Mwalimu lilirudi baada ya kupendekezwa na alisisitiza mchakato uliofanywa na ngazi ya wilaya haukuwa na baraka ya juu.

“Kesho (leo) tutatoa ratiba za kampeni baada ya mchakato huu kukamilika. Nawaomba wana-Chadema na Ukawa wawe watulivu kila kitu kitakwenda sawa na mgombea wao yupo makini,” alisema Kilewo.

Kwa upande wake, Mwalimu ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 aligombea Jimbo la Kikwajuni na kushindwa na mgombea wa CCM, Hamad Yussuf Masauni aliishukuru Chadema kwa imani naye na kumpa nafasi hiyo.

“Naingia katika kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya wakazi wa Kinondoni kuwa mbunge wa Kinondoni. Siendi kuwa mbunge wa Chadema au Ukawa, nitakuwa mbunge wa watu wa Kinondoni,” alisema Mwalimu na kuongeza.

“...Naomba wakazi wa Kinondoni watupime, watuchuje na watutathmini wagombea na baadaye waamue nani anakidhi vigezo na anatosha kuwatumikia katika kipindi cha miaka mitatu iliyobakia.”

Alisema Kinondoni ni taswira na sura ya nchi na imebeba vitu vingi kuliko kawaida na ana imani ya wakazi wa jimbo hilo watawapima vizuri kabla ya kufanya uamuzi wa kuwachagua na atahakikisha anasimamia vyema masilahi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment