Watafiti nchini Japana wameiwekea treni kipasa sauti ambacho kinabweka kama mbwa na kutoa mlio wa swara ili kuzuia treni kugonga swara njiani.
Gazeti la Asahi Shimbun lilisema kuwa sauti hizo zinatumiwa kuwafukuza swara kutoka kwa reli kwa lengo la kupunguza idadi ya wanaogongwa na kuuawa na treni.
Maafisa kutoka kwa taasisi ya reli wanasema kuwa mlio wa sekunde tatu wa swara humfanya swara kuwa makini na kusikiliza, ukifuatiwa na sekunde 20 za mbweko wa mbwa, inaweza kusababisha swara kukimbia.
Watafiti wanasema kuwa majaribio ya usiku wakati swara wanakusanyika kando ya reli yamesababisha swara hao kupungua.
Swara hukaribia reli nyakati za usiku kulamba chuma za reli wakitafuta virutubishi muhimu vya madini ya mwili.
Wizara ya uchukuzi nchini Japan inasema kuwa kulikuwa na visa 613 vya treni kugonga swara na wanyama wengine mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment