Saturday, 20 January 2018

Maseneta wakwamisha serikali ya Trump

Bunge la Seneti nchini Marekani limeshindwa kuidhinisha mswada ambao ungeongeza ufadhili wa serikali ya kitaifa kwa mwezi mmoja.

Kufuatia hatua hiyo huduma nyingi za serikali zitakwama, hata hivyo athari kamili itaanza kuonekana siku ya Jumatatu, wakati wafanyakazi wa serikali watarejea kazini.

Mara ya mwisho shughuli za serikali zilikwama nchini Marekani ni mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu, na ilidumu kwa muda wa siku kumi na sita wakati ambapo wafanyakazi wengi wa serikali walishurutishwa kwenda likizo ya lazima.

Ni mara ya kwanza kwa huduma za serikali kukwama huku chama cha Republican kudhibiti mabunge yote na ikulu ya White house.

Ikulu ya whitehouse imewalaumu wabunge wa Democrats kwa kuweka siasa juu ya maswala ya kiusalama , familia za wanajeshi, watoto walio katika mazingira magumu, na uwezo wa taifa hilo kuwahudumia raia wa Marekani.

Lakini kiongozi wa wabunge wa Democrats Chuch Schumer, alisema kuwa rais Trump alikataa makubaliano yasiopendelea upande wowote na hakukishinikza chama chake katika bunge la Congress.

Mkwamo wa huduma za serikali nchini Marekani ulifanyika mara ya mwisho 2013 na ukachukua muda wa siku 16.

Republicans waliutaja muswada huo kwa jina la ''Schumer Shutdown' na hawakukosea.

Chuck Schumer na wabunge wenzake wa Democrats kupitia usaidizi wa wabunge wachache wa Republican walizuia muswada ambao ungesaidia serikali kuendelea na shughuli zake, hata ijapokuwa kwa muda.

Hatahivyo kuchukua jukumu na kutoa lawama ni vitu viwili tofauti.

Democrats watasema kuwa walikuwa wamekubaliana na rais kupitisha muswada usiopendelea upande wowote kuhusu mabadiliko ya sheria ya uhamiaji, kabla ya kukiuka makubaliano hayo wakati wa mkutano katika afisi ya Oval wiki iliopita.

Swala la kurushiana lawama lilianza saa sita usiku na mshindi bado hajatangazwa.

Hatahivyo atakayeshindwa katika mkwamo huu ni chama kitakachoingia katika vita na idadi ndogo ya wabunge ikiwa ni habari mbaya kwa rais Trump na chama cha Republicans.

Habari njema ni kwamba , pande zote mbili na ngome zao za kisiasa zitafurahishwa kwa kufanya mambo kuwa magumu.

Kwa nini pande hizo mbili zisikubaliane?

Swala linalogombaniwa ni lile la Democrats kutaka zaidi ya wahamiaji wasio na vibali walioingia nchini Marekani kutofurushwa.

Wahamiaji hao walipatiwa vibali vya kuwa nchini humo kwa muda chini ya mradi ulioanzishwa na rais wa zamani Barrack Obama.

Mnamo mwezi Septemba, bwana Trump alitangaza alikuwa anasitisha mpango huo huku akilipatia bunge la Congress hadi mwezi Machi kuwa na mpango mbadala.

No comments:

Post a Comment