Friday, 19 January 2018

Simba kukutana na waliokwamisha mipango

Vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC leo alfajiri wameondoka kwa ndege kuelekea mjini Bukoba mkoani Kagera kwaajili ya mchezo wao wa raundi ya 14.

Simba ambayo jana ilishinda mchezo wake wa raundi ya 13 kwa mabao 4-0 dhidi ya Singida United kwenye uwanja wa Uhuru, inakwenda kukutana na Kagera Sugar ambayo ilikwamisha mipango yake ya ubingwa msimu uliopita.

Kagera Sugar ilitibua mipango hiyo April 2 mwaka jana baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa uwanja wa Kaitaba hivyo kuinyima nafasi ya kurejea kileleni ikibaki na alama 55 katika nafasi ya pili na kuwaacha Yanga wakiwa na alama 56 kileleni.

Endapo Simba ingeshinda mchezo huo ingefikisha alama 58 hivyo huenda ingetwaa ubingwa kutokana na bingwa wa msimu uliopita kupatikana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, baada ya timu hizo mbili za Kariakoo kufungana pointi.

Simba ambayo kwasasa inaongoza ligi kwa alama 29 mbele ya Azam FC yenye alama 27, itashuka dimbani Kaitaba siku ya Jumapili.


No comments:

Post a Comment