Thursday, 18 January 2018

Mambosasa akanusha Polisi kuzuia Wanawake kuvaa nguo fupi




Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  Lazaro Mambosasa amekanusha kutoa tamko la kuzuia wanawake kuvaa nguo fupi zisizo na heshima kwa maelezo kuwa  jambo hilo ni la kimaadili siyo sheria.

Amesema Jeshi la Polisi lina kazi ya kushughulikia makosa ya kisheria na si maadili.

Mambosasa ametoa kauli hiyo leo Januari 18, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Redio Clouds, ikiwa ni siku mbili baada ya kunukuriwa katika mkutano wake na wanahabari kuwa amezuia uvaaji wa nguo fupi jijini Dar es Salaam.

 “Niliwaeleza wazi kuwa suala la mavazi bado halijatungiwa sheria hivyo polisi hatuhusiki nalo mtu anayevaa kimini katika maeneo kama kanisani au msikitini  ni ukiukwaji wa maadili,” amesema na kuongeza,

“Niliwaeleza  kuwa katika nyumba hizo za ibada kuna kamati ya ulinzi na usalama za eneo husika wao watakushughulikia lakini si polisi.”

Amesisitiza, “Nilikwenda mbali zaidi na kuwaeleza kuwa hivyo vimini kuna mahali vinahitajika kama ufukweni, sehemu za starehe. Ikitokea mtu amepigwa, amedhalilishwa au amekamatwa na askari kwa kuwa amevaa kimini ana haki ya kulalamika kuwa ameshambuliwa.”

No comments:

Post a Comment