LEO tutaona jinsi ya kupika makange ya nyama ya kuku ikiwa ni kutokana na mfululizo wa kujifunza kupika vyakula vya aina mbalimbali.
MATAYARISHO NA KUPIKA
Kuku 1
Mafuta ya kupikia lita 1
Tangawizi iliyotwangwa (kusagwa) vijiko vikubwa 3
Kitunguu saumu kilichotwangwa- kijiko kikubwa 1
Kitunguu maji kikubwa 1
Karoti kubwa 1
Pilipili Hoho kubwa 1
Ndimu 2
Chumvi vijiko vikubwa 3
Masala ya kuku (chicken masala) vijiko vikubwa 3
Nyanya ya pakti kijiko kikubwa 1
Nyanya kubwa 1
Pilipili 1
MATAYARISHO
Osha kuku wako vizuri kisha mkate vipande upendavyo.
Muwekee viungo vyako kama tangawizi, vitunguu saumu, ndimu 1 na kipande (kipande kimoja weka pembeni), chumvi vijiko 2, masala ya kuku vijiko 2 kisha mchanganye vizuri na muweke kwenye friji kwa saa mbili.
Kata karoti, pilipili hoho na kitunguu maji kwa urefu au umbo upendalo, ila viwe vipande vikubwa vinavyoonekana baada ya kuiva.
Saga nyanya iweke kwenye kibakuli.
JINSI YA KUPIKA
Chukua kikaango, mimina mafuta na yaache yapate moto wa wastani. Anza kumkaanga kuku taratibu mpaka aive. Tumia kikaango hichohicho, punguza mafuta yabakize kidogo kwa ajili ya kukaanga viungo vilivyobakia. Anza kukaanga kitunguu kisha weka pilipili hoho halafu malizia na karoti. Usikaange kwa muda mrefu kwani havitakiwi kuiva sana.
Weka nyanya ulizosaga, koroga na malizia kwa kuweka chumvi, masala, nyanya ya paketi, pilipili na ile ndimu kipande kilichobakia. Mimina kuku wako na mkoroge kidogo ili aenee vile viungo, kisha mtoe weka kwenye sahani. Hapo makange yako yatakuwa tayari kwa kula, unaweza kula kwa wali au ugali.
No comments:
Post a Comment