Saturday, 20 January 2018

VYAKULA VINAVYOSAIDIA KUONDOA MAUMIVU WAKATI WA HEDHI


WIKI iliyopita tuliona jinsi matunda yanavyosaidia kutibu maradhi mbalimbali mwilini, leo tutaangalia aina mbalimbali za matunda yanayoweza kutibu matatizo mbalimbali yanayowahusu wanawake wakati wa siku zao (menstruation period). Miongoni mwa matunda hayo ni papai bichi lakini lililokomaa ambalo lina uwezo wa kulainisha misuli ya njia ya uzazi hivyo kufanya kipindi cha hedhi kutokuwa na maumivu.

Katika suala hili, ili wanawake kujiepusha na kupatwa na matatizo ya maumivu, kutokwa damu kwa wingi kusiko kawaida, kuchelewa kuona siku zao, wanashauriwa kuzingatia suala la lishe. Wanapaswa kujua vyakula gani wale na vipi wasile ili kujiwekea kinga ya kudumu dhidi ya tatizo hili.

LISHE YA KUDHIBITI MATATIZO YA HEDHI
Matatizo mbalimbali yanayohusiana na hedhi, yanaweza kudhibitiwa na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa kutibu mfumo mzima wa mwili, ili kuondoa sumu iliyojilimbikiza katika mwili wa mgonjwa kwa kipindi cha muda mrefu, sumu ambayo imegeuka na kuwa chanzo cha matatizo yanayojitokeza wakati wa hedhi.

Mfumo mzima wa mwili unapokuwa umezingirwa na sumu (toxins), ndiyo huwa chanzo cha matatizo mbalimbali, yakiwemo hayo yanayojitokeza kwa wanawake wakati wa hedhi na dawa pekee katika hili ni kwanza, kuondoa sumu hizo mwilini kwa njia ya lishe.

Ili kuondoa sumu hizo mwilini, mgonjwa anatakiwa kuanza mpango maalum wa kula matunda na mbogamboga pekee, kutwa mara tatu kwa muda wa siku tano mfululizo. Katika siku hizo, anachokuwa anakula ni matunda, juisi za matunda kama machungwa, mananasi, zabibu, tufaa, papai bichi, karoti, parachichi, nyanya, mboga mbalimbali pamoja na maji, kila wakati wa kula unapowadia, maji hayo mtu anywe nusu saa baada ya mlo.

Hii ina maana kwamba mlo wa mtu huyu, katika kipindi cha siku hizo tano, utakuwa vyakula vilivyotajwa hapo juu, kuanzia asubuhi, mchana na jioni, katika kipindi hicho, matunda, juisi na mbogamboga atakazokuwa anakula zitakuwa zinafanya kitu kinachoitwa kitaalamu ‘detoxification’, yaani uondoshaji wa sumu mwilini kwa njia ya asili
aliyotuumba nayo Mungu. Hata hivyo, kwa wale wanawake ambao ni wembamba sana, ambao pengine katika kipindi cha funga hiyo ya matunda wanaweza kupoteza uzito sana, wanaweza kunywa glasi ya maziwa freshi sambamba na mlo wao wa matunda. Hii ni kwa sababu ya kuepuka kupoteza uzito kuliko kawaida.

UFUATE MLO KAMILI Baada ya kumaliza siku tano za kula na kunywa juisi na matunda, mtu mwenye kufanya zoezi hili atatakiwa kuzingatia ulaji wa mlo kamili utakaotilia maanani matunda, mboga za majani, vyakula vya nafaka kama ugali wa mahindi, mtama, ulezi n.k. Nafaka zinazoshauriwa ni zile ambazo hazijakobolewa na kuondolewa viini lishe (wholegrain).

Waepuke kula vyakula vitokanavyo na unga mweupe, ikiwemo mikate myeupe, sukari, vitu vitamu (confectioneries), vyakula vya kwenye makopo. Aidha, mtu huyu anashauriwa kuepuka kunywa chai iliyowekwa majani mengi au kahawa iliyowekwa kahawa nyingi

. UVUTAJI SIGARA UKOME Kwa wale akina mama wenye matatizo wakati wa siku zao na ambao wameamua kuingia katika mpango huu wa kusafisha mwili, hawana budi kuachana kabisa na uvutaji sigara kama ni wavutaji ili kufanikisha zoezi hilo. Kwa ujumla uvutaji sigara ni mbaya kwa afya ya binadamu.

Makala hii imeandaliwa na Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai, kwa ushauri wasiliana naye kwa namba 0754391743 au 0717 961 795. Usikose pia kusoma makala zangu za Afya Yako kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda kila Jumatatu uelimike.

No comments:

Post a Comment