Wednesday 6 December 2017

Saratani Ya Shingo Ya Kizazi, Inasababishwa Na Ngono Na Mambo Mengine Ya Fahamu Hapa


 
UTAFITI mpya wa kitabibu umebaini kuwa saratani ya shingo ya kizazi, inasababishwa pamoja na mambo mengine na ngono kama ilivyo kwa ugonjwa wa Ukimwi, madaktari bingwa wa magonjwa ya maradhi hayo wamesema.


wametaja mambo mengine yanayoweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi kuwa ni kujiingiza kwenye mapenzi katika umri mdogo, kuolewa mara nyingi, kuwa na wapenzi wengi, kusafisha sehemu za siri kwa bidhaa zenye kemikali na kuzaa mara nyingi.




Katika kiwango cha kimataifa, wastani wa mwanamke kuzaa bila kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa saratani, ni watoto wanne.

Madaktari hao walisema saratani ya shingo ya kizazi inatokana na aina 40 ya virusi, aina mbili ikiwa ni virusi vinavyosambaa kwa njia ya ngono  “Human papilloma virus (HPV) Squamos cell carcinoma kirusi namba 16 na Adenocarcinoma namba 18, ni kati ya virusi 40 vinavyosababisha saratani ya kizazi na vyenyewe vinachangia tatizo hilo kwa asilimia 70.” Wanasema saratani ya uzazi ndiyo inayoongoza ikilinganishwa na nyingine nchini na asilimia 80 ya wagonjwa, wameambukizwa kwa ngono. “Saratani hiyo husambaa kwa ngono kutoka mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine.

Mwanamke mwenye saratani ya kizazi akifanya ngono, mwanamume huchukua virusi na kumwambukiza mwingine atakayefanya naye ngono,” alisema na kuongeza:

“Wagonjwa wengi na wale ambao tayari wana maambukizi, wamekuwa wakikutwa na virusi hawa wa aina mbili ambao wamekuwa wakienezwa zaidi kwa njia ya zinaa. Inawezekana mwanamume akawa ametoa kirusi kwa mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine.”

“Hata hivyo, kuna wanaume ambao tayari wameshakuwa na maambukizi ya HPV wanatembea na virusi, hawa tunawaita (high risk sexual male patner) wanaume hawa utakuta kila akioa mke anakufa kwa saratani ya shingo ya uzazi, lakini kamwe virusi hao hawawezi kumwathiri yeye.”

Kuanza ngono mapema nako kunachangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya saratani hiyo, kwani binti anakuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi mapema na hivyo kuweza kumwathiri mapema zaidi, tofauti na yule aliyeanza baadaye.

“Idadi kubwa ya wanawake wamekutwa na saratani mapema sana, ukilinganisha na umri wao, lakini wengi wao wamekuwa wakikutwa na ugonjwa huu kuanzia umri wa miaka 35 kwenda juu. Hii inamaanisha kuwa walipata maambukizi hayo walipokuwa na miaka 20-25.”

Licha ya hivyo mgonjwa anaweza asitambue tatizo hilo mpaka miaka 10 hadi 15 baadaye ambapo
tatizo linajitokeza hadharani. “Unapopata maambukizi ya HPV inakuchukua muda mpaka kujulikana, kwa kawaida mwanamke anaishi miaka 10 hadi 15 na baadaye anagundulika na tatizo hili, lakini itategemea na kushuka kwa kinga zake.

Kama ikitokea hapo katikati ukajitokeza ugonjwa mwingine kama HIV basi saratani nayo itajitokeza.” Utafiti walioufanywa Septemba 2011 kuhusu tatizo la HIV na saratani ya shingo ya uzazi unaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanawake waliokuwa na maambukizi ya HIV na CD4 ziliposhuka tu, saratani ya kizazi nayo iliibuka, hiyo inamaanisha kuwa tatizo hilo ni kubwa tofauti na linavyodhaniwa. Kwa upande wake virusi vya HPV huambukizwa kwa mwanamke moja hadi mwingine, pale mwanamume anapofanya tendo hilo na mwanamke mwenye maambukizi na kwenda kufanya tendo hilo na mwanamke mwingine. Kinga Madaktari hao wameeleza kinga ya maradhi hayo kuwa ni pamoja na matumizi ya kondomu na uaminifu wa wapenzi katika uhusiano wao.

Ninatoa wito kwa Watanzania na jamii kiujumla kujijengea tabia ya kupima mara kwa mara ili kubaini maambukizi mapema. Ongezeko la watu wanaougua saratani ya shingo ya uzazi imetokana na ongezeko kubwa la watu, ikiwa ni pamoja na tabia ya kuchangia ngono kwa wapenzi.

Alisema chanjo ya saratani ya shingo ya uzazi inayotarajiwa kuanza kutolewa kwa mabinti wa miaka tisa mpaka 12 baadaye, Ni moja ya juhudi ya Serikali katika kupambana na ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment