Thursday, 7 December 2017

Wafanyabiashara wametoa kilio chao kwa wingi wa Kodi kwa Dk Mpango



Dodoma. Wafanyabiashara wametoa kilio chao cha wingi wa kodi zinazotozwa na Serikali na mazingira yasiyo ya ushindani sawa wa kibiashara nchini, jambo linalowafanya kushindwa kuchangia ipasavyo katika maendeleo.

Mambo mengine waliyolalamikia ni kutozwa kodi mara mbili, baadhi ya wafanyabiashara kuingiza nguo kutoka nje ya nchi kwa njia za panya, utaratibu wa utoaji wa vibali kwa mamlaka za Serikali na kodi na ushuru katika sekta ya kilimo.

Wakizungumza jana katika mkutano wao na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wafanyabiashara hao walisema hawawezi kushindana kibiashara kama hakutakuwa na ushindani ulio sawa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania, Felician Kilahama alisema kuna wafanyabiashara wa mbao ambao wamekuwa wakitozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) lakini wengine hawatozwi, jambo ambalo haliweki ushindani sawa wa kibiashara nchini. “Unakuta wale wanaotozwa VAT bidhaa zao zinakuwa juu ya wale ambao hawatozwi kodi jambo ambalo halileti ushindani sawa katika biashara,” alisema Kilahama.

Alisema pia kuna tatizo la wafanyabiashara kuidai Serikali fedha za VAT inazotakiwa kurejesha na kuitaka kuangalia jinsi ya kutatua tatizo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mahoteli, Nura Karamagi alilamikia tozo ya Serikali ya kuingia katika mageti ambayo wanatozwa watalii kwamba inapunguza ufanisi katika sekta hiyo.

Licha ya Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere kusema kuwa kodi hiyo ilishafutwa tangu Julai, Karamagi alisema bado wenye hoteli wamekuwa wakitozwa na inajionyesha katika karatasi za malipo.

Mwenyekiti wa Wasindikaji Mafuta (Tasupa), Ringo Ringo alilamikia kiwango kikubwa cha kodi kinachotozwa cha VAT ikilinganishwa na nchi nyingine kama za Kenya. “Kenya wao wanatoza asilimia 14 tu lakini sisi hapa tunatozwa asilimia 18,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James alisema changamoto iliyojitokeza katika urejeshaji wa VAT ni udanganyifu na kwamba ili kuwalipa malipo halali, Serikali inakagua madai hayo.

Alisema wameanza kuirejesha na kwamba Oktoba walirudisha Sh33 bilioni na Novemba Sh15 bilioni. “Na Desemba tunatarajia kulipa zaidi ya Sh10 bilioni, bado tunapitia hesabu.”

Dk Mpango alisema kukutana na wafanyabiashara hao kulilenga kuwasikiliza na kujumuisha hoja zao katika bajeti ijayo. 

No comments:

Post a Comment