Thursday, 7 December 2017

VIDEO: Siku 17 za Kutoweka kwa Mwandishi wa Mwananchi



Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imelaani vikali huku ikipaza sauti ya kutaka arejeshwe akiwa hai mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti Mwananchi, Azory Gwanda aliyechukuliwa na watu wasiojulikana.
Gwanda ambaye kituo chake cha kazi ni Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Novemba 21, 2017 baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa Kibiti majira ya saa 4:00 asubuhi.

MCL ilipata taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo Novemba 30, 2017 kutoka kwa ndugu zake na mkewe baada ya kushindwa kumpata kwenye simu yake.

Juhudi za kuhakikisha Gwanda anapatikana chini ya uongozi wa kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, wizara husika na wadau wa tasnia hiyo ya habari hazijafanikiwa hadi leo.

Kutokana na mazingira hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai akiwa ameongozana na timu ya wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na viongozi wa Jukwaa la Wahariri(TEF) leo Alhamisi asubuhi ameitisha mkutano wa vyombo vya habari kueleza jinsi kampuni inavyoendesha harakati za kumtafuta mwandishi huyo kupitia jeshi la polisi na wizara ya habari.



“Tumefuatilia tukio hilo hadi kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Kanda Maalumu ya Rufiji ambaye amesema hawana taarifa na kwamba atafuatilia kisha kutoa taarifa. Mpaka leo hatujapata taarifa yoyote,” amesema Nanai.

Katika tukio hilo, waandishi wote na wafanyakazi wa kampuni hiyo inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen wamevalia mavazi meusi huku wakiwa wameinua juu magazeti na mabango yenye ujumbe unaosema kwa maandishi makubwa ‘Bring Back Azory’, #MrudisheniAzory.

Waandishi wa habari walihitaji kujua ni sababu au dalili gani ambazo kampuni inaamini zimesababisha kupotea kwa Gwanda, aina ya habari alizokuwa amepewa kufuatilia za uchunguzi na habari ya mwisho kuripoti katika gazeti la Mwananchi ilikuwa ya aina gani.

Nanai amejibu maswali hayo kwa nyakati tofauti lakini akasema habari ni nyingi zinazoandikwa na vitisho vimekuwapo kwa waandishi wa habari katika mazingira tofauti.

Kupotea kwake

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Nanai amesema kwa mujibu wa Anna Pinoni, ambaye ni mke wake, Azory alichukuliwa na watu ambao hawafahamu waliomfuata eneo ambalo hupenda kukaa kwa ajili ya maongezi na wenzake katika mji wa Kibiti.



Amesema kwa maelezo ya Anna watu hao waliokuwa na gari nyeupe aina ya Toyota Land Cruiser walienda naye shambani kumfuata. Walipofika shambani, Azory alimuuliza mkewe mahali zilipo funguo za nyumba yao na kuelezwa sehemu zinapowekwa siku zote.

Nanai amesema baadaye watu hao na Azory wakaondoka na kumuacha mkewe shambani. Kabla ya kuondoka, Azory alimwambia mkewe kwamba anaenda kazini na atarudi jioni ya siku hiyo (Jumanne Novemba 21, 2017) au siku inayofuata (Jumatano Novemba 22, 2017).

“Mkewe aliporudi nyumbani alikuta nyumba imefungwa na funguo zikiwa mahali alipoziweka, lakini alipoingia ndani alikuta dalili za kupekuliwa kwani vitu mbalimbali vilikuwa vimerushwa shaghalabaghala ndani ya nyumba. Mkewe anasema hakuwa na wasiwasi mpaka siku iliyofuta baada ya kuona simu zake zote hazipatikani,” anaendelea kusimulia Nanai.

Amesema Alhamisi ya Novemba 23, 2017 alikwenda(mkewe) kuripoti Kituo cha Polisi Kibiti na kupewa RB Na:Kibiti/RB/1496/2017 ambako walimweleza kuwa  hawajui alipo na kumwomba awape namba yake ya simu ili wampigie iwapo watapata taarifa zinazomhusu, lakini mpaka sasa hajapewa taarifa yoyote wala kuitwa.



“Baada ya hapo, juhudi za kumtafuta ziliendelea ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari vya ndani na nje, baadhi vikatangaza na kuchapisha. Pia kampuni ilituma ujumbe wake kwa mkewe Kibiti kumpa pole na kupata taarifa zaidi ili kujua kinachoendelea.”

Nanai amesema pamoja na hatua hiyo, MCL imeshaandika barua rasmi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Wengine waliopata barua ni Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Taasisi ya MISA-TAN, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na wadau wengine kuhusu kupotea kwa mwandishi huyo.


No comments:

Post a Comment