Wednesday, 6 December 2017

Nigeria wateua Waziri wa kushughulikia furaha, mahusiano kifamilia



Gavana wa Jimbo la Imo, Rochas Okorocha (kushoto).

Serikali ya Jimbo la Imo nchini Nigeria imeteua waziri atakayeshughulikia masuala ya furaha na mahusiano ya kifamilia.

Uteuzi wa waziri huyo unaelezwa ni mkakati wa kuwasahaulisha wananchi adha za kisiasa na mapigano ya makundi haramu.

Gavana wa jimbo hilo, Rochas Okorocha amesema uteuzi huo ni wa kwanza kufanyika katika Taifa hilo lililopitia kipindi kigumu cha mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram na hali mbaya ya kisiasa.

Okorocha amemteua ndugu yake, Ogechi Ololo kuwa waziri wa masuala ya furaha na mahusiano mema ndani ya familia.

Kabla ya uteuzi huo, Ogechi alikuwa msaidizi wa Gavana Okorocha na mshauri wake maalumu wa masuala ya nyumbani. Pia, anahusika na mapambo wakati wa sikukuu ya Krismasi.

Hata hivyo, msemaji wa gavana huyo, Sam Onwuemeodo hakutoa maelezo zaidi kuhusu majukumu ya waziri huyo.

Akizungumza na Shirika la Habari la AFP alisema, “Hakuna kitu kipya zaidi katika uteuzi huo.”

“Gavana ni mtu mbunifu ambaye kila wakati huanzisha vitu vipya serikalini. Jukumu kubwa la waziri huyu ni kuleta ubunifu ambao utaweza kuigwa na magavana wengine. Gavana anataka kuwafanya watu wawe na furaha kila wakati na ndiyo maana ameunda wizara hii kwa lengo hilo,” amesema.

No comments:

Post a Comment