Wednesday, 6 December 2017

Lissu afurahi kutembelewa na Rais mstaafu Mwinyi


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya umri wa miaka 93 alionao Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi bado amediriki kufunga safari kwenda kumtembelea na kumpa pole.

Lissu, ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutembelewa na Mzee Mwinyi katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako anaendelea na matibabu.

Lissu amelazwa hospitalini hapo tangu Septemba 7 anakotibiwa akiuguza majeraha ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma akitokea kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu kuhusu kutembelewa na Mzee Mwinyi, mwanasheria huyo wa Chadema pamoja na mke wake, Alice walisema wamefurahi kutembelewa na kiongozi huyo.

“Nimefurahi sana kwamba umri wote alionao wa miaka 93 si kidogo, ametafuta muda kuja kunipa pole hospitalini ni kitu kizuri sana, ni ubinadamu mkubwa sana,” alisema Lissu ambaye alionekana mwenye furaha.

Rais mstaafu Mwinyi anakuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Serikali waliomtembelea Lissu kwani hivi karibuni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye alifika hospitalini hapo kumjulia hali.

Mzee Mwinyi akiambatana na mke wake na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Kenya walifika hospitalini hapo kumjulia hali mbunge huyo na picha zinawaonyesha wawili hao wakizungumza huku nyuso zao zikiwa na tabasamu

No comments:

Post a Comment