Iringa. Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Albert Chalamila amesema chama hicho mkoani humo kimepoteza mwelekeo kutokana na baadhi ya wanachama kuendekeza majungu, ufitini na uongo.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, amesema huu ni wakati wa kuijenga CCM mpya na katika uongozi wake hataruhusu mtu ampelekee majungu ofisini.
“CCM Iringa imepoteza mwelekeo kutokana na kuwapo genge la wafitini, kusemana uongo, umbea, kutukana na wapo wachache wapo tayari kukiharibu chama. Katika utawala wangu sitaki mtu wa kuja kuleta majungu ofisini,” amesema Chalamila.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema iliitwaa jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na Peter Msigwa. Pia, ilishinda udiwani katika kata nyingi hivyo kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Amesema jukumu lililo mbele yake ni kuwaleta pamoja wanachama wa CCM ili kurejesha heshima ya chama hicho ndani ya Mkoa wa Iringa ambayo kwa sasa imetoweka.
“Iringa leo imepoteza majimbo matatu, jimbo la Iringa Mjini, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kutokana na wingi wa kura wa Chadema wakapata mbunge wa Viti Maalumu. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha tunarejesha majimbo hayo CCM,” amesema Chalamila.
Pia, amesema katika uongozi wake atafanya uhakiki wa mali za CCM na miradi yake ili kuona namna bora ya kukiendeleza chama hicho.
Wakati huohuo, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Salim Abri (Asas) amewashukuru wajumbe wa mkutano kwa kumuamini na kumchagua.
Akijifananisha na paka, Abri amesema atatumia fursa hiyo kuwakamata panya walio ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
No comments:
Post a Comment