Thursday, 7 December 2017

Wananchi wakubaliana na Vita dhidi ya rushwa inayoendeshwa na Rais



 Dar es Salaam. Wananchi wanaonekana kukubaliana na vita dhidi ya rushwa inayoendeshwa na Rais John Magufuli, matokeo ya utafiti yamebainisha.

Utafiti huo kuhusu hali ya rushwa nchini uliofanywa na taasisi ya Repoa kwa kuwezeshwa na taasisi ya Afro Barometer, ulihusisha wananchi 2,400 katika mikoa yote.

Utafiti huo unaoitwa “Mtazamo wa Wananchi Katika Rushwa wa 2017”, unaonyesha kuwa ushiriki wa Serikali katika kupambana na vita dhidi ya rushwa umeongezeka.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo yaliyotangazwa jana, wananchi saba kati ya 10 (asilimia 71) ya waliohojiwa walisema ushiriki wa Serikali katika kupambana na vita dhidi ya rushwa ni mzuri, imani hiyo ikiongezeka kutoka asilimia 37 kulingana na matokeo ya mwaka 2014/15.

Akiwasilisha matokeo hayo, Profesa Pellizzio Riccard kutoka Repoa alisema utafiti huo unaonyesha imani ya wananchi kuongezeka katika vita dhidi ya rushwa ndani ya taasisi za Serikali.

Kwa mujibu wa utafiti huo, rushwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepungua hadi asilimia 14 kutoka 37, Takukuru (asilimia 11 kutoka 29), Jeshi la Polisi (asilimia 36 kutoka 50), mahakimu na majaji imepungua hadi asilimia 21 kutoka 35.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwaka 2015, imekuwa ikiwafikisha mahakamani watu wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa kubwa kama uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Pia imepambana na ufisadi katika mashirika ya umma, ukwepaji kodi, utoroshaji makontena bandarini na kutimua wafanyakazi wa umma wanaojihusisha na ufisadi.

Hata hivyo, mmoja wa wasomi waliohudhuria hafla ya kutangazwa kwa matokeo hayo jana, Dk Simeon Mesaki alisema mtazamo huo unaweza kuwa tofauti na hali halisi.

“Kama utafiti unahusu mtazamo, matokeo yanaweza kuwa tofauti na hali halisi. It is the all about perception against reality (ni suala la mtazamo dhidi ya uhalisia),” alisema.

“Lakini, pili inawezekana kwamba jinsi Serikali inavyofanya kazi na watu wakaona, basi imani ni wazi itaongezeka. Kwa mfano, wananchi wanaona vigogo wa Escrow wanapandishwa mahakamani basi imani inaongezeka.”

Dk Mesaki alihofia kama kasi hiyo inaweza kudumu. “Je, vita hii itaendelea na kasi yake au ni povu tu kwa sababu Serikali iliyopo imeamua kutengeneza legitimacy (uhalali) yake?” alihoji.

Mbali ya Profesa Riccard, uwasilishaji wa matokeo hayo uliohudhuriwa na wasomi, wadau kutoka balozi na taasisi mbalimbali ulifanywa pia na mtafiti Lulu Silas kutoka Repoa.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakaluka alisema kupungua kwa vitendo vya rushwa kumetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuimarisha nidhamu na kurejesha imani ya polisi kwa wananchi.

Mwakaluka alisema wapo askari waliochukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa kazi, kupewa onyo kali huku kiwango cha uelimishaji kikiongezeka kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

Jeshi la Polisi na mahakama zimekuwa zikitajwa mara kwa mara kuwa taasisi ambazo wananchi wanaziona kuwa zinaongoza kwa vitendo vya rushwa.

Mbali ya matokeo hayo, mkurugenzi mkuu wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema pamoja na imani kuongeza, bado wananchi wanaogopa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.

Dk Mmari alisema hiyo inatokana na woga wa kujulikana endapo watatoa taarifa hizo.


No comments:

Post a Comment