Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ Ammy Ninje amesema anafurahishwa na mwenendo wa mazoezi ya timu yake ambayo yanatoa taswira ya kufanya vizuri kwenye mchezo ujao.
Kilimanjaro Stars imeendelea na mazoezi yake leo asubuhi kwenye Uwanja wa Machakos Academy, ambapo kocha Ninje ameanza kufanyia kazi namna ya kukaba wakati mpira unapokuwa kwa adui au timu inapopoteza mpira. Sambamba na hilo Ninje pia amefanyia kazi namna ya kutengeneza mashambulizi.
“Timu inaendelea vizuri na mazoezi na nafurahi kuona vijana wanafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza tulipocheza na Libya na tunaamini hayatajirudia kwenye mechi ijayo, tutashinda dhidi ya Zanzibar Heroes”, amesema Ninje.
Kilimanjaro Stars, ilicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Libya Jumapili Desemba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kenyatta na kutoka sare tasa katika mfululizo wa mechi za michuano ya CECAFA inayoendelea nchini Kenya ikiwa katika hatua ya makundi.
Timu hiyo ipo kundi A pamoja na timu za Rwanda, Zanzibar, Libya na wenyeji Kenya. Hadi sasa Kenya ndio vinara wa kundi hilo wakiwa na alama nne baada ya michezo miwili huku Zanzibar Heroes ikishika nafasi ya pili ikiwa na alama tatu ikifuatiwa na Libya yenye alama mbili. Tanzania ina alama moja huku Rwanda ikiburuza mkia ikiwa haina alama.
No comments:
Post a Comment