Saturday, 27 January 2018

Bodi ya Ligi yaipiga rungu Mbeya City

Timu ya Mbeya City

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia Mkurugenzi wa Ligi Boniface Wambura imetangaza kuipiga faini ya jumla ya shilingi milioni moja klabu ya Mbeya City kwa makosa mawili tofauti.

Wambura amebainisha hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam na kusema timu hiyo ilitenda kosa la kutumia mlango usio rasmi kuingilia uwanjani katika mechi iliyofanyika Januari 1,2018 Jijini Mbeya ambapo kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa kanuni za ligi kuu na kutozwa laki 5 kama adhabu yao.

Aidha, Wambura alisema Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa waraka kwa wamiliki wa viwanja kuhakikisha timu zote zinaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi nasio vinginevyo.

Mbali na hilo, Wambura amesema Klabu hiyo pia imepigwa faini ya laki 5 kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa madai alikataa kutoa 'penalti' kwa timu hiyo.

Kwa upande mwingine, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia Mkurugenzi wa Ligi Boniface Wambura imetangaza kumfungia kocha wa timu hiyo Ramadhani Mwazurimo mechi mbili na kupigwa faini ya laki 5 kutokana na kutoa lugha ya kashfa katika mechi ya Tanzania Prisons dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Lowassa amnadi Salum Mwalimu Kinondoni

Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama cha Demokrasia na  Maendeleo CHADEMA, Edward Lowassa jioni leo amemnadi Mgombea wa Ubunge wa Kinondoni kupitia chama hicho, Salumu Mwalimu huku akiwataka wakazi wa Kinondoni kuacha kumuongelea mgombea wa CCM, Maulid Mtulia maana amekuwa msaliti kwao.

Lowassa alitumia wakati huo pia kuwashukuru wananchi wa Kinondoni kwa kumpigia kura wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, na kuwaomba zile kura walizompigia 2015 basi wazielekeze kwa Mwalimu ambaye anaamini ni msomi mwenye kuweza kuwatetea wakazi wa Kinondoni.

" Msiogope vijana wa Kinondoni wenzetu wamekuwa wajanja wakilinda kura zao sasa na sisi kama ambavyo wazungumzaji wengine wamesema basi tunaomba mlinde kura zetu ikiwezekana tulale katika vituo vya kupigia kura kuhakikisha hatuibiwi.

Nae Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Fredrick Sumaye alisem, " Hakikisheni mnamchagua Mwalimu huyu ndie mtu safi wa kuhakikisha analeta maendeleo katika jimbo lenu,"

Kwa upande wake Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, alisema " Achaneni na wao wanaosema mimi sio mkazi wa hapa nachoomba ni kura zenu ambazo zitanifanya nikawatetee kuwajengea shule, kuhakikisha ajira kwa vijana,"

Kampeni za chama hicho zitaendelea kesho katika eneo la Kigogo jijiji Dar es Salaam ambapo zitaongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe.

Taliban watumia 'ambulance' iliojaa vilipuzi kuwaua watu 95 Afghanistan

Mlipuaji wa kujitolea mhanga amewaua takriban watu 95 na kuwajeruhi wengine 158 katika mji mkuu wa wa Afghanistan Kabul, kulingana na maafisa.

Washambuliaji waliendesha ambyulensi iliokuwa imejaa vilipuzi kupitia kizuiazi cha polisi hadi katika barabara ambayo ilikuwa imetengewa wafanyikazi wa serikali.

Kisa hicho kilitokea katika jumba la wizara ya maswala ya ndani na afisi ya Muungano wa Ulaya na baraza kuu la amani.

Kundi la wapiganaji wa Taliban linasema kuwa walitekeleza shambulio hilo ambalo ni baya zaidi katika kipindi cha mwezi mmoja.

Walioshuhudia wanasema eneo hilo ambalo lina majumba ya balozi nyingi pamoja na makao makuu ya polisi mjini humo, lilikuwa na watu wengi wakati bomu hilo lilipolipuka siku ya Jumamosi .

Maafisa wanasema kuwa idadi ya waliofariki inaendelea kuongezeka huku majeruhi wakipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Shirika la kimataifa la msalaba mwekundi limesema kuwa utumizi wa 'ambulence' unakera.Wiki moja iliopita ,wapiganaji wa Taliban waliwaua watu 22 katika hoteli moja ya kifarahari mjini Kabul.

Hili ndilo shambulizi baya zaidi kuwahi kufanyika mjini Kabul katika kipindi cha miezi kadhaa.

Mnamo mwezi Oktoba, watu 176 waliuawa katika shambulio la bomu mjini Afghanistan katika kipindi cha wiki moja.

Vikosi vya maafisa wa usalama vya Afghanistan vimeshambiliwa pakubwa na wapiganaji wa Taliban ambao wanataka kuweka sheria ya kiislamu katika taifa hilo.

Mnamo mwezi Mei, takriban watu 150 waliuawa na mpiganaji wa kujitolea mhanga mjini Kabul.

Kundi la wapiganaji wa Taliban walikana kutekeleza shambulio hilo lakini serikali ya Afghanistan inasema kuwa kundi la Haqqani ambalo ni mshirika wake lilitekeleza shambulio hilo kupitia usaidizi wa Pakistan.

Pakistan imekana kusaidia kundi lolote la wapiganaji linalotekeleza mashambulizi nchini Afghanistan .

Mwezi huu, Marekani ilikatiza usaidizi wake wa usalama kwa Pakistan, ikisema kuwa taifa hilo limeshindwa kuchukua hatua dhidi ya makunni ya kigaidi katika ardhi yake.


Matapeli wa Viwanja DSM kukiona

Serikali ya Mkoa wa Dsm Imetangaza rasmi vita dhidi ya Matapeli wa Viwanja na Nyumba ambao wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali ikiwemo ofisi za mawakili ,mahakama pamoja na Madalali kuwadhulumu wajane pamoja na watu wasiokuwa na Uwezo.

Mkuu wa Mkoa wa Dsm Paul makonda akizungumza na waandishi wa habari baada ya kwenda kwa familia ya Bi,Stella Bejumula pamoja Mume wake ambao ni watumishi wastaafu wa serikali ambao wametapeliwa nyumba kwa zaidi ya Miaka sita na kuishi maisha ya Kutangatanga na kutegemea Misaada ikiwemo chakula kutoka kwa watu mbali mbali..

Aidha Familia hiyo ya Bejumula ilitoa mtiririko mzima wa kadhia ya Kutapeliwa ambapo mwaka 2012 walikopa bank ya Crdb Mkopo na kufanikiwa kurejesha zaidi ya asilimia 80,na kubaki million ishirini ambayo alitokea Mtu mmoja kuwakopesha kwa riba lakini baadae akadaiwa kutengeneza Mkataba bandia wa mauzo kuwa familia hiyo imemuuzia kwa milion 96 Huku nyumba hiyo ikiuzwa kwa mtu mwingine katika kipindi cha siku 4 tu baada ya deni kulipwa.

Aidha Makonda alikwenda katika nyumba iliyopo kitalu B namba 91 ambayo ilikuwa ikimilikiwa na mzee na Bi,Bejumula na kutoa agizo la mmiliki aliyeuziwa eneo hilo kufika ktika ofisi za Mkuu wa Mkoa na nyaraka alizofanikisha kununua eneo hilo.

Makonda pia aliwakabidhi wazee hao wastaafu vyakula mbali mbali ikiwemo,Mchele,mafuta,unga, ngano na sukali huku akimtaka mfadhili anayewasaidia malazi aendelee kuwasaidia wakati akishughulikia suala hilo hali iliyozua simanzi eneo hilo …

Yanga SC yavunja rekodi ya Azam FC Chamazi

Mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara baina ya mabingwa watetezi klabu ya Yanga dhidi ya Azam FC umemalizika katika uwanja wa Azam Complex Chamazi kwa mabingwa hao kushinda jumla ya mabao 2-0.

Kwa ushindi wa Yanga SC unaifanya timu hiyo kuvunja rekodi ya wana lamba lamba Azam FC ya kutokupoteza hata mchezo mmoja toka kuanza kwa ligi kuu soka Tanzania Bara msimu huu wa mwaka 2017/18.

Wafungaji katika mchezo alikuwa Shabani Chilunda wa Azam FC wakati kwa upande wa Yanga SC akiwa Obrey Chirwa na Gadiel Michael.

Kwa matokeo hayo inaifanya mabingwa watetezi Yanga SC kufikisha jumla ya pointi 28 wakiwa nafasi ya tatu, Azam FC ikisalia na alama zake 30 nafasi ya pili huku Simba SC ikiongo katika msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 32 na mchezo mmoja mkononi ambao unatarajiwa kupigwa hapo kesho siku ya Jumapili.

Katika michezo mingine iliyopigwa hii leo timu ya Mbeya City ikiwa nyumbani imekubali kutoka sare ya mabao 0 – 0 dhidi ya Mtibwa Sugar wakati Mwadui FC ikiwa nyumbani imelizimishwa sare ya magoli 2 – 2 na Njombe Mji wakati Kagera Sugar ikitoka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Lipuli FC.

Mtulia kuweka hadharani mikakati yake Kinondoni

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM Wilaya wa Kinondoni, Harold Maruma amesema mgombea ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya chama hicho, Maulid Mtulia atatumia uzinduzi wa kampeni kueleza mikakati yake ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

CCM inazindua kampeni leo Jumamosi Januari 27,2018 kuanzia saa 10:00 jioni katika viwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam.

Maruma amesema baadhi ya changamoto zitakazozungumzwa na mgombea huyo ni barabara na mikopo kwa akina mama.

"Tunaomba wakazi wa Kinondoni kujitokeza  kwa wingi na Jeshi la Polisi limetuhakikishia kuwa hakuna mtu atakayedhurika wakati wa kampeni na wakati wa kurudi nyumbani," amesema.

Wengine wanaoshiriki uzinduzi wa kampeni hizo ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba na wabunge wake wa mkoa wa Dar es Salaam.

Tayari viongozi wakuu wa chama hicho tawala waliofika katika uwanja wa Biafra wametambulishwa na kuipisha bendi ya bendi ya TOT inayotoa burudani ya nyimbo za  kuhamasisha wana CCM.

Watu 30 Wapoteza Maisha Katika ajali ya moto Korea Kusini

Imethibitika zaidi ya watu 30 wamekufa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya moto uliotokea katika Hospitali moja nchini Korea Kusini.

Hata hivyo maafisa wa nchi hiyo wanasema idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka kutokana na baadhi ya watu kujeruhiwa vibaya.

Imefahamika kuwa moto huo ulianzia katika chumba cha dharura cha Hospitali ya Sejong, kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Zaidi ya majeruhi 100 wanasemekana wamo katika jengo la hospitali hiyo.

Mwaka jana watu 29 walikufa katika mji wa Echeon, Korea Kusini, na wengine kujeruhiwa baada ya moto kuzuka katika sehemu ya mazoezi ya wazi.

VIDEO: Makonda Aangua Kilio


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda  leo ametembelea na kutoa pole  kwa Familia ya Wastaafu ya Bwana Edward Bejumula na Bi. Stella Bejumula walioteseka kwa Miaka Sita bila Makazi baada ya kudhulumiwa Nyumba yao ambapo ameahidi kulivalia njuga suala hilo kuhakikisha haki inatendeka bila kuvunja sheria.

 TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI .....USISAHAU KUSUBSCRIBE



VIDEO: Full Video CCM Wakizindua Kampeni Kinondoni


Chama cha Mapinduzi CCM kimezindua kampeni zake za Ubunge wa jimbo la Kinondoni huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba pamoja na Waziri wa zamani wa Maji, Steven Wassira wakimnadi mgombea wa Chama hicho, Maulid Mtulia.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI...USISAHAU KUSUBSCRIBE

Kauli ya Jaji Mkuu yaamsha upya hoja ya mgawanyo wa madaraka


Kauli ya hivi karibuni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kuwa viongozi wa Serikali na wanasiasa wasiingilie Mahakama na kudharau amri za mhimili huo, imeamsha upya hoja la mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola ambayo imekuwa mjadala kwa muda mrefu.

Mjadala kuhusu mgawanyo huo wa Serikali, Bunge na Mahakama umekuwapo nchini kwa muda mrefu hasa wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuwa inaonekana Serikali ama inaizidi nguvu au inaingilia shughuli za mihimili mingine, licha ya kwamba yote hiyo inatakiwa kuonekana sawa.

Hata hivyo, baadhi ya watu huamini kwamba mhimili wa Serikali ambao unaongoza dolo ndio wenye nguvu kwa kuwa unasimamia mapato na matumizi ya mihimili mingine.

Hata Rais John Magufuli alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu suala hilo Novemba 2016, alisema, “Mihimili hiyo (Bunge, Serikali na Mahakama) inaweza ikalingana, lakini inawezekana kuna mhimili ambao umechimbiwa zaidi kwenda chini.”

Akisisitiza jibu lake, Rais alizungumzia jinsi alivyokwenda kwenye shughuli ya mahakama na akaombwa fedha na uongozi wa mhimili huo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zake kwa kutambua kuwa, Rais ndiye mwenye uwezo wa kuwapatia fedha hizo.

Ndani ya mjadala huo, pia yamekuwapo madai miongoni mwa wananchi kupitia maoni yao wakati wa mchakato wa Katiba, wanasiasa, wanaharakati kuwa Serikali imekuwa inaingilia shughuli na mihimili mingine – Bunge na Mahakama, jambo ambalo linaathiri uhuru wake.

Pengine ni kutokana na madai hayo au mengine, ndipo Jaji Mkuu anaibuka na ujumbe mahususi kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa Serikali;

“Nawasihi viongozi wote wa Serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria, wabaki ndani ya maeneo yao ya kikatiba na wajiepushe na kuingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na mamlaka ya Kikatiba ya Mahakama.”

Akaongeza kwamba kuanzia sasa (Mahakama) watakuwa wakali kwa mtu atakayeingia katika anga zao, huku akiwataka mahakimu na majaji kuchukua hatua kwa watu wanaodharau amri zao, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mamlaka ya utoaji haki ni ya Mahakama pekee.

Hata hivyo, akijibu kwa nini aliamua kutoa kauli hiyo, Jaji Mkuu anasema ni kutokana na taarifa za vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiripoti matukio hayo ya amri za Mahakama kuvunjwa.

Hakuishia hapo, Jaji Mkuu akawataka mahakimu ambao kwa bahati mbaya amri zao zinavunjwa na wanaonekana hawachukui hatua waanze kufanya hivyo kama Bunge linavyofanya, kwamba ukiingia katika anga zake, utaitwa mbele ya kamati, utaulizwa maswali na hatua zinachukuliwa.

Jaji Mkuu anasema Mahakama ina nguvu kama hiyo na si Jaji Mkuu mwenye nguvu hiyo pekee bali kwenye kila Mahakama; mahakama za mwanzo, mahakama za wilaya na mahakama za hakimu mkazi na asitokee mtu akajivika kofia ya kimahakama, atachukuliwa hatua.

Jaji Juma anasema kwa mujibu wa Katiba, sheria ndio inayotakiwa ipewe nguvu na si masuala ya kisiasa kwa kuwa nguvu ya Serikali ni sheria na si mtu.

“Sheria ikikupa nguvu unaitumia, ikikupa mamlaka unayatumia. Siasa haikupi nguvu, sheria ndio inakupa nguvu na tujaribu tubaki ndani ya sheria na ndani ya Katiba hakutakuwa na mvurugano. Vilevile tunawataka wale ambao wamepewa mamlaka yao, wabaki huko waliko na tukifanya hivyo hatutakuwa na migongano yoyote,” anahitimisha.

Kauli hiyo ya inaungwa mkono na Ibara ya 107 A (1) ya Katiba ya Tanzania inayosema: “Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar, na kwa hiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki.”

Mjadala mtandaoni

Muda mfupi baada ya maelezo hayo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, “Mh Jaji Mkuu kauli kuhusu wanasiasa na watendaji wa Serikali kutokuingilia Mahakama ni kauli muhimu kwa wakati huu, lakini Mahakama ambayo ni imara katika haki inawezaje kukubali kuingiliwa? Mahakama inapaswa kujitazama zaidi. Mahakama ikiyumba Taifa linayumba.”

Si Lema tu aliyezungumzia hilo, wananchi wengine mbalimbali walitoa maoni yao kuhusu kauli hiyo kupitia ukurasa wa Facebook wa Mwananchi, Twitter na Instagram, huku wengine wakienda mbali zaidi kwa kumtaka Jaji Mkuu kuwaeleza maneno hayo wafuasi wa CCM, wakidai kwamba wapinzani hawana jeuri ya kuingilia Mahakama.

Kwa jinsi mjadala ulivyokwenda ni wazi kuwa Jaji Mkuu Profesa Juma ameona kuna kitu ambacho pia wananchi wanakiona hakiendi sawa na kuamua kufikisha ujumbe wake kwa njia hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanatafsiri kauli ya Jaji Mkuu kama “kuchoshwa kwa mhimili huo kuingiliwa na hivyo ameamua kufikisha ujumbe kwa wenye tabia hizo ili waache mara moja.

Hatua ya Jaji Juma bila shaka ni ya kupongezwa kwani si tu imeonyesha kwamba mahakama imezinduka na kutambua wajibu na nguvu zake na hivyo inafungua pazia la demokrasia na mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili hii mitatu ya dola.

Hatua hiyo ikizingatiwa na kutekelezwa itasaidia kuifanya mahakama iaminike na kiwe chombo pekee kimbilio kwa kila mtu kwa ajili ya utoaji haki.

Ingawa Jaji Mkuu hakutoa mifano ya matukio ya kuingilia uhuru wa mahakama, mifano ipo mingi, mfano wameshuhudiwa baadhi ya watendaji wa Serikali wakiamuru ubomoaji wa nyumba ambazo inadaiwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara, zikiwamo zilizokuwa na amri ya mahakama ya kuzuia zisibomolewe.

Mbali na mahakama, hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliwakaririwa akisema hata Bunge limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali.

“Maneno na vitendo vya Rais vinaashiria kuwa Bunge halina uhuru wake na mimi kama mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu,” alisema Zitto kupitia mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa “Ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya Serikali.

Moja ya matukio ambayo mbunge huyo alitaja kama kuingilia mhimili huo ni kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kwa kigezo cha gharama, huku hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha Bunge moja kwa moja bila malipo vikizuiwa.

Akijadili suala la uhuru wa mahakama na kauli ya Jaji Mkuu, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa anasema kwa muda mrefu wanasiasa na watetezi wa haki wamekuwa wakipigia kelele suala hilo lakini halikuonekana kufanyiwa kazi, hivyo hatua ya Jaji Mkuu italeta matumaini yalikuwa yametoweka.

Anasema katika suala la utoaji haki, Mahakama inapaswa kusimama kwa miguu yake isishurutishwe na isiingiliwe; majaji wazingatie sheria wakati wa kutoa hukumu.

Haiingii akilini kwamba mahakama inatoa amri fulani, lakini watendaji walioko chini ya Serikali wakapuuza na wakaendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna amri yoyote,” anasisitiza.

“Jaji Mkuu yuko sahihi kama kweli anamaanisha. Kwa muda mrefu tumeshuhudia viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya wakijitokeza kuingilia mhimili huo na kusababisha ama kupingana au kuwagawa na matokeo yake wanashurutishana na kutishana hadharani.”

Onesmo anasema hata kama Mahakama imekosea, kuna utaratibu wa kisheria wa kufuata ili kuipinga na si kama hali ilivyo sasa.

Anasema kuwa jambo hilo la kuingiliwa Mahakama likiachiwa liendelee litasababisha athari kuu tatu kwa jamii na kuzitaja kuwa ni pamoja na kuvunja Katiba.

Mosi, anasema mahakama ni chombo cha kutoa haki na endapo haitakuwa huru, ni wazi kuwa Katiba itakuwa inavunjwa na mwananchi atakosa haki zake za msingi.

Pili, anasema tatizo jingine ni kutengeneza Taifa lisilo fuata utawala wa kisheria na kwamba watu wataamua wanavyotaka wao, jambo ambalo litakuwa si zuri kwa mustakabali wa nchi.

“Jingine, ni kuingia katika migogoro isiyo na tija; itafika wakati wananchi watachoshwa na matendo hayo na kusababisha migogoro mikubwa na matokeo yake hayatakuwa mazuri,” anasisitiza Mratibu huyo wa masuala ya haki za binadamu.

Ni kutokana na umuhimu huo na mjadala mpana katika mchakato wa Katiba ikawekwa ibara ya 169 inazungumzia kwa kina uhuru wa mahakama.

Katiba inayopendekezwa

196 (1) Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitaongozwa na masharti ya Katiba hii na hazitaingiliwa ama kwa kudhibitiwa, kushinikizwa au kupewa maelekezo na mtu au chombo chochote.

(2) Nafasi ya madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano haitafutwa wakati wowote ule ikiwa kuna mtu ambaye kwa wakati huo anashikilia nafasi hiyo.

(3) Mishahara na malipo mengine ya Majaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano yatalipwa kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

(4) Mshahara na malipo mengine yanayolipwa kwa Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano hayatabadilishwa kwa maana ya kumuondolea faida Jaji husika.

(5) Malipo ya mafao ya kustaafu ya Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakamu Kuu ya Jamhuri ya Muungano hayatabadilishwa kwa maana ya kumuondolea faida Jaji husika wakati wote wa uhai wake.

(6) Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani, Mahakamu Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Mahakama Kuu ya Zanzibar hatashtakiwa kwa jambo lolote alilolifanya au kutolifanya kwa nia njema katika   

Mwananchi. 

Chadema yazidi kukimbiwa na madiwani wake



Wimbi la madiwani wa Chadema kujivua uanachama na kujiunga na CCM limezidi kukikumba chama hicho kikuu cha upinzani nchini baada ya leo Januari 27, mwaka 2018 madiwani wake wanne kujiunga na chama tawala, wakiwemo watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo  mkoa wa Kilimanjaro.

Wakati diwani wa Kimara (Chadema), Pachal Manota akitambulishwa katika uzinduzi wa kampeni za ubunge za chama hicho jimbo la Kinondoni zilizofanyika viwanja wa Biafra, wenzake watatu walitambulishwa kwenye mkutano wa kampeni za ubunge jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro uliofanyika eneo la Makiwaru.

Madiwani hao ni Juliana Malamsha, Martha Ushaki (wote Viti maalum) na Frank Umega (kata ya Kelamfua).

Wametambulishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rodrick Mpogolo wakati akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel.

Mpogolo amesema viongozi wa upinzani wanajiunga na CCM baada ya kubaini ajenda ya kuwahudumia wananchi, kuwaletea maendeleo ipo katika chama tawala pekee .

"Kuna  wimbi kubwa la viongozi wa upinzani kujiunga na CCM. Hii inatokana na viongozi hao kubaini kuwa ajenda ya huduma na maendeleo iko katika chama hiki pekee. Tupeni Dk Mollel ili tuweze kutekeleza agenda hii muhimu,” amesema Mpogolo.

Uamuzi wa madiwani wa Chadema kuhamia CCM mpaka sasa umeziweka Halmashauri tano zilizo chini ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwa hatarini kuchukuliwa na CCM.

Halmashauri hizo ni Arusha, Arumeru, Hai, Siha na Iringa ambazo madiwani wake, hasa kutoka Chadema wametimkia CCM kutokana na sababu tofauti, kubwa ikiwa ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli.

Ahadi ya Jafo Siha yafananishwa na rushwa


Wasomi wameifananisha na rushwa ya uchaguzi ahadi iliyotolewa kwa wananchi wa Jimbo la Siha kuwa watapata neema iwapo watamchagua mgombea wa CCM, Dk Godwin Mollel ambaye anatetea ubunge aliouachia mwishoni mwa mwaka jana kwa kujivua uanachama wa Chadema.

Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo wakati akimnadi mgombea Dk Mollel.

Wamesema kauli hiyo inaweza kusababisha ushindi wa Dk Mollel kupingwa, huku Profesa Abdallah Safari akienda mbali zaidi na kufananisha kauli hiyo na iliyowahi kutolewa na mawaziri kadhaa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga mwaka 2011 na kusababisha ushindi wa aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Dalali Kafumu kubatilishwa na Mahakama.

Akiwa jukwaani, Jafo alisema CCM ndicho chama chenye Serikali na ndicho kinachoweza kutatua changamoto na shida za wananchi, na kwamba akishinda Serikali itafanya kila njia kuboresha maisha ya wananchi.

Jafo alisema ikiwa wananchi watamchagua Dk Mollel ambaye hivi karibuni alijiondoa Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama tawala, Serikali itashirikiana naye na miaka miwili iliyobaki Siha itakuwa moja ya wilaya ambazo zitapiga hatua kubwa na kufanya vizuri katika utekelezaji wa maendeleo.

Lakini ahadi hiyo ya Waziri Jafo kwa wananchi wa Siha haijapokelewa vizuri na wasomi waliohojiwa na Mwananchi.

“It is a sort of (ni kama-rushwa) kwa wapiga kura kupitia miradi ya maendeleo ya Serikali, anaposema Dk Mollel akishinda ndipo hospitali ijengwe,” alisema Dk Hamad Salim, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Dk Salim alisema kauli hiyo inaashiria rushwa na kushauri mawaziri watenganishwe na vyama vya siasa.

“Kuna haja ya kutenganisha mawaziri na vyama vya siasa. Mawaziri wanapaswa kuwa watendaji wa Serikali. Kauli ile inakera mno. Ni afadhali tu angesalimia na kuongea kama mwana CCM kuliko kuihusisha Serikali,” alisema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema kauli ya Jafo inakwenda kinyume na sheria ya gharama za uchaguzi.

“Sheria ya gharama za uchaguzi iliyoanzishwa mwaka 2010 haikusikika sana kwenye uchaguzi wa 2015, lakini inaeleza vizuri. Kifungu cha 21(a) na (c) vinakatza hata mgombea tu kuahidi kutoa zawadi ili achaguliwe, kwa sababu itahesabika kama rushwa?” alisema Dk Mbunda.

Naye Profesa Safari alisema ikiwa mgombea wa Chadema katika jimbo hilo, Elvis Mosi atashindwa katika uchaguzi huo, wataitumia kauli ya Jafo kupinga matokeo mahakamani.

Katika ufafanuzi wake, Profesa Safari alisema kauli ya Jafo inaashiria utoaji wa rushwa na inaweza kusabababisha kesi kama ya Jimbo la Igunga.

“Hiyo ni corruption (rushwa) kabisa na ndiyo maana ile kesi ya Igunga tulishinda,” alisema Profesa Safari ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara.

“Ni kauli mbaya sana na inaweka mazingira ya kupinga uchaguzi huo endapo mgombea wa CCM atashinda. Kesi ya Igunga imekuwa ikirejewa katika kesi nyingi tu.”

Hata hivyo, mkurugenzi wa taasisi ya Fordia, Buberwa Kaiza amesema kauli ya Jafo inaweza isihesabike kama rushwa kwa sababu hospitali yenyewe haijajengwa, japo kimaadili kutoa ahadi kama hiyo ni kosa.

“Maadili ya uchaguzi yanazuia kabisa mtu kutumia mali za Serikali kufanyia kampeni chama cha siasa. Maadili pia yanazuia kabla na baada ya uchaguzi kutumia majukumu ya Serikali kama ahadi ya uchaguzi,” alisema.

“Kama ilani ya uchaguzi ya CCM ilisema watajenga hospitali na yeye alikuwa akikumbushia, sawa. Lakini kama alisema mgombea wao akichaguliwa ndipo watajenga, hilo ni kosa.”

Wakimbizi kutoka Kongo wazidi kumiminika nchini


Zaidi ya raia 800 kutoka jamhuri ya kidemikrasi ya Kongo wamewasili mjini kigoma kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini wakidai kukimbia vita katika nchi hiyo.

Raia hao wa DRC ambao wengi ni wanawake na watoto wametokea mashariki ya nchi hiyo na wamewasili kwa maboti kwa nyakati tofauti katika bandari ndogo ya Kibirizi mjini kigoma na kueleza kuwa hali ya vita katika nchi hiyo ni mbaya na kuomba serikali ya Tanzania kuwapokea.

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa amefika katika eneo hilo na kueleza kuwa wamewapokea lakini serikali inafanya tathmini ya ujio wao.