Saturday, 25 November 2017

Waziri wa zamani wa fedha Zimbabwe afikishwa mahakamani




Aliyekuwa waziri wa fedha wa Zimbabwe,Ignatius Chombo amefika mahakamani kujibu mashtaka ya  ulaji rushwa dhidi yake.

Kwa mujibu wa habari,Chombo huyo alikamatwa wiki mbili zilizopita wakati jeshi lilipochukua utawala nchini humo.

Bwana Chombo alifukuzwa katika chama cha ZANU-PF Jumapili iliyopita.

Hata hivyo Chombo ameonekana akiingia mahakamani akiwa hana wasiwasi.

Emmerosn Mnangagwa ameapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe.Baada ya kuapishwa kwake rais huyo mpya ametakwa na baadhi ya wafuasi wake kulishughulikia kundi la G-40 linalosemekana kuwa lilikuwa likimuunga mkono Mugabe na mkewe.

Chombo alikuwa kati ya wanachama wa G40

Hii kali...Roboti iliyopewa uraia nchini Saudi Arabia yataka kuwa na familia



Roboti iliyopewa uraia nchini Saudi Arabia imesema kuwa ina haki ya kuwa na familia.

Roboti hiyo kwa jina la Sophia  ilitengenezwa nchini Hong Kong na kupewa uraia nchini Saudi Arabia mwezi uliopita.

Roboti hiyo İimesema kuwa ingependa kuwa na familia wakati ilipohudhuria mkutano wa habari ulioandaliwa nchini UAE.

Kwa mujibu wa habari roboti hiyo imesema kuwa familia ni kitu muhimu sana.

Robot hiyo imesema kuwa kila mwanadamu ana haki ya kuwa na familia na watu wenye hisia sawa na yeye.Jambo hilo ni muhimu sana hata kwa roboti.Aliwaambia wanadamu wajisikie furaha kuwa na familia.

Filamu mpya ya bollywood yazua mzozo nchini India



Filamu mpya ya Bollywood  ambayo bado haijazinduliwa imeleta kizaazaa baina ya viongozi wa juu nchini India.

Filamu hiyo kwa jina la Padmavati imepingwa vikali na wanasiasa wa chama tawala serikalini pamoja na makundi ya mrengo wa kulia hata kabla ya uzinduzi wake.

Maisha ya mtayarishaji wa filamu hiyo pamoja na waigizaji yapo hatarini kutokana na kuigizizwa kwa filamu hiyo.

Filamu inaelezea historia ya Malkia Padmavati wa dini ya kihindu wakati wa karne ya 14.

Malikia Padmavati alijichoma moto akiwa hai baada ya Mfalme Khalji ambae alikuwa ni muislamu kuwavamia na kumuua mumewe.

Waigizaji maarufu Deepika Padukone na  Ranveer Singh wamecheza kama Padmavati na Sultan Khalji.

Makundi yanayoipinga filamu hiyo yanadai kuwa filamu hiyo imebadilisha baadhi ya matukio ya kihistoria.

Hata hivyo mtayarishaji wa filamu hiyo amekana tuhuma hizo.

Baadhi ya watu kutoka katika Kabila la warajput pamoja na waumini wa kihindu wamepinga filamu hiyo kutokana na mahusiano ya kimapenzi yaliyoonyeshwa kati ya mfalme wa kiislamu na malkia wa kihindu.

Wamedai ni aibu kubwa na uvunjaji heshima kwa kabila lao.

Dk Shika kupanda jukwaani kumnadi mgombea wa CCM


Mwanza. Katika kampeni za lala salama leo, CCM itawapandisha jukwaani aliyekuwa mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi na Dk Louis Shika, aliyejizolea umaarufu baada ya kuibuka kwenye mnada wa nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi.

Katambi aliyejiunga na CCM akitokea Chadema na Dk Shika watamnadi kwa wapiga kura wa Kata ya Mhandu jijini Mwanza mgombea wake, Constantine Sima.

Katibu wa uenezi wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Mustapha Banigwa amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa wengine watakaopanda jukwaani katika mkutano utakaofanyika mtaa wa Machinjioni ni waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha aliyerejea CCM akitokea Chadema.

Mkutano huo pia utahutubiwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa mbunge wa Bunda, Stephen Wasira, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na mbunge wa Bukombe, Doto Biteko.

Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini utafanyika kesho Jumapili Novemba 26,2017.

Mwananchi:


Chadema yawaomba wapiga kura kukaa mita 100



Dar es Salaam. Chadema wamewataka   wapiga kura kukaa umbali wa mita 100  wakati wa kusubiri matokeo yao kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyia kesho katika kata 42 nchini, ili kulinda kura zao.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Jeshi la Polisi lilipinga wapiga kura kukaa umbali wa mita 100 na baadaye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhitimisha sakata hilo kwa kutamka kuwa kukaa umbali wa mita 200, baada ya kupiga kura hairuhusiwi.

Akielezea mwenendo wa uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema,  Benson Kigaila amesema  sheria inaruhusu wapiga kura kukaa umbali huo ili kulinda kura zao.

“Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inataka wapiga kura kusimama umbali wa mita 100, kwa hiyo tuwaambie wapiga kura wetu wakishamaliza kupiga kura wakae umbali wa mita hizo, waongeze na nyingine moja walinde kura zao,” amesema

Kigaila amewataka  wapiga kura hao kwenda kwenye vituo vya kupigia kura na kutimiza wajibu wao bila kuogopa kitisho chochote na baadaye walinde kura zao hadi zitakapotangazwa.

“Waende wakapige kura wasiogope kitisho chochote,” amesema a kuwataka baadaye waende kwenye makao makuu ya kata yatakako tangazwa matokeo hayo kuhakikisha, washindi wanatangazwa kwa haki.

Kiongozi huyo wa Chadema amesema kumekuwa matukio ya uvunjaji wa haki kwenye mikutano yao ya kampeni ikiwamo makada wake kuvamiwa na kupigwa.

“Upinzani ukishinda utatangazwa wapende wasipende, ambaye atatangaza matokeo tofauti ashughulikiwe kama mwizi mwingine wa kawaida kwa sababu wezi huwa wanashughulikiwa,”

“Kwa hiyo watu waende walinde haki yao ya kikatiba, wapige kura na walinde matokeo. Yatangazwe matokeo sahihi.” amesema  kiongozi huyo wa  Chadema

Rais Magufuli aeleza sababu ya kuliacha jengo la Tanesco akiwa waziri



Dar es salaam. Rais John Magufuli amesema hakubomoa jengo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopo Ubungo alipokuwa waziri wa ujenzi kwa kuwa aliogopa kufukuzwa kazi.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumamosi Novemba 25,2017 alipozindua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), kampasi ya Mloganzila.

Akizungumza mbele ya waziri mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda aliyehudhuria uzinduzi huo, Magufuli amesema wakati huo aliogopa baada ya kuzuiwa na waziri mkuu huyo, lakini sasa yeye ndiye Rais hakuna wa kumzuia.

Akizungumzia ubomoaji unaoendelea sasa amesema, “Nilishatoa maagizo, najua Mizengo Pinda kwenye hili alinipinga wakati ule, lakini najua leo hawezi akanipinga kwa sababu mimi ndiye Rais. Wakati ule nilikuwa waziri wake, ndiyo maana nilinyamaza nilijua ninaweza nikafukuzwa, hutakiwi kumpinga mkubwa.”

 “Hilo jengo la Tanesco, narudia kama itakuwa ni kubomoa nusu, no problem (hakuna tatizo); kama ni lote hakuna tatizo, pamoja na jengo la wizara ya maji. Najua katibu mkuu wa wizara ya maji yupo hapa ananiangalia, wakaanze kulitoa eneo lililopo kwenye hifadhi ya barabara,” amesema.

Machi 6, 2011 akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Chato, mkoani Kagera, Pinda ambaye alisifia utendaji wa Dk Magufuli alimwagiza kusimamisha ubomoaji maeneo kadhaa yaliyokuwa kwenye hifadhi ya barabara likiwemo jengo la Tanesco hadi Serikali itakapotoa kauli nyingine kuhusu hilo.

Pinda alikuwa akizungumzia hatua ya Dk Magufuli aliyekuwa amewaagiza wananchi waliojenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba hizo na wasitarajie kulipwa fidia.

Pinda wakati huo akiwa waziri mkuu alisema spidi (kasi) ya Magufuli ilikuwa kubwa hivyo alimuagiza kusimamisha ubomoaji huo hadi suala hilo litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.

Pinda, ambaye alikuwa waziri mkuu kuanzia 2008 baada ya kujiuzulu kwa Edward Lowassa alisimamisha ubomoaji huo ili kutoa nafasi kwa Serikali kujipanga upya.

Alisema Serikali inamuamini Magufuli kuwa kiongozi mwenye uwezo na ndio maana ilimpa nafasi akawabane makandarasi wazembe.

Dk Magufuli akiwasilisha bajeti bungeni mwaka 2012/13, alizungumzia ubomoaji akisema siasa iachwe akisisitiza sheria zimepitishwa ikiwamo Sheria namba 13 ya mwaka 2007 na ya hifadhi ya barabara iliyoanza tangu mwaka 1932.

Alizungumzia jengo la Tanesco alisema liko kwenye hifadhi ya barabara na kwamba hata kama asipolibomoa yeye kuna siku litabomolewa vinginevyo sheria ibadilishwe.

Novemba 15 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Magufuli alimuagiza wakala wa barabara nchini (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.

Mwananchi:

Mourinho amponda Mkhitaryan, amwambia kiwango chake kimeshuka



Mkufunzi wa Manchester United Jose Mourinho ameukosoa mchezo wa Henrikh Mkhitaryan huku Borussia Dortmund ikisema kuwa iko tayari kumsajili kwa mara nyengine mshambuliaji huyo wa Armenia

Mkhitaryan, ambaye alijiunga na United kutoka Dortmund mwezi Julai 2016 kwa dau la £26.3m, hakushirikishwa katika kikosi cha United katika mechi mbili zilizopita.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hatahivyo atarudi katika kikosi cha kwanza cha United katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Brighton.

Mourinho alisema kuwa kiwango cha mchezo wa Mkhitaryan kimekuwa kikipungua hatua baada ya hatua

Mkhitaryan alianzishwa mechi 10 kati ya 11 za ligi ya Uingereza kabla ya kuachwa nje baada ya kutolewa katika dakika 62 katika mechi ambayo United ilipoteza kwa Chelsea kwa 1-0 mnamo tarehe 5 mwezi Novemba.

"Sikufurahia kiwango chake cha mchezo'', alisema Mourinho kuhusu mchezaji ambaye amefunga mabao mawili pekee katika mechi 16 alizochezeshwa msimu huu.

Waziri Kigwangalla awajibu wanaosema vyuma vimekaza




Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Hamisi Kigwangalla amesema maisha yataendelea kuwa magumu kwa watu wasio na shughuli maalum ambao wamezoea kuishi kwa ujanja ujanja.

Ameyasema hayo wakai akijibu maswali ya wananchi kupitia mtandao wa ‘Twitter’ ambao wengi walitaka kujua kuhusu utendaji kazi wake na hali halisi ya maisha yalivyo wakidai kuwa ni magumu.

“Wanaofanya shughuli zao halali hawatoona vyuma vimekaza, badala yake watafurahia sema watoto wa mjini, wasanii sanii na wajanja wajanja ndiyo watapata shida! Hawa wajanja wajanja ni wangapi? Na wenye shughuli halali ni wangapi?”, alisema Kigwangalla akiacha maswali kwa mmoja wa watu waliomuuliza.

Waziri Kigwangalla aliendelea kwa kutoa ufafanuzi juu ya namna ya kujenga uchumi kupitia kufanya kazi na sio kutegemea kupata pesa kwa njia rahisi rahisi.

“Mfumo wa uchumi unataka watu tufanye kazi kwa ubunifu ndipo tupate maisha mazuri siyo kufanya usanii kidogo tayari ukatajirika! Kukaza vyuma maana yake kuziba mianya ya wasanii ili walio kwenye uchumi halisi na wasanii wawe sawa siyo kuonea watu!” alimaliza.

Waziri Kigwangalla hivi sasa yupo jimboni kwake Nzega vijijini akiwa amepiga kambi kwaajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Nata.

CAF yataka Yanga, Simba Kupeleka Majina




Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezitaka Simba na Yanga haraka kupeleka majina ya wachezaji wake kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa ajili ya ushiriki wa michuano yake mwakani, pia watakaguliwa mahesabu yao.

Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, huku Simba wakishiriki Kombe la Shirikisho kutokana na kuwa mabingwa wa Kombe la FA.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema klabu hizo zinatakiwa kuwasilisha majina yao Caf mapema kabla ya mwisho wa mwezi huu.

“Simba na Yanga wanatakiwa kutuma majina ya usajili wa wachezaji wao mapema kabla ya Novemba 30, mwaka huu kwa sababu wakichelewa inaweza
kuwa tatizo kwao,” alisema Lucas.

 “Na kwa sasa kamati ya leseni za klabu inakwenda kufanya ukaguzi katika klabu hizo ili kufahamu kama zimetimiza matakwa ya kupata leseni ya kushiriki michuano ya Caf.

“Timu zitakaguliwa ofisini na watendaji wake, umiliki wa nyaraka mbalimbali, ukaguzi wa mahesabu na ripoti ya fedha ya mwaka mzima kama Kanuni ya 11 ya ligi kuu na kanuni ya saba ya Caf zinavyojieleza kuhusiana na leseni za klabu,” alisema Lucas.

Chelsea wawasili Liverpool tayari kwa kazi



Chelsea wametua salama jijini Liverpool kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Liverpool ambayo inasubiriwa kwa hamu leo Anfield.

Lakini kiungo mkongwe wa timu hiyo, Cesc Fabregas amefanya kituko wakati wakiwasili, ameonekana akiwa amefunika uso wake gubi gubi.

Kwa kila timu, mechi hiyo ni muhimu, Liverpool ikataka kurejesha imani na kasi yake katika EPL lakini Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wanataka kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutetea taji.

Tambwe yupo fiti kuivaa Tanzania Prisons leo



MSHAMBULIAJI Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe anatarajiwa kurejea leo timu yake, Yanga ikimenyana na Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Tambwe hajacheza mechi hata moja ya mashindano msimu huu, baada ya kuumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba Agosti  20 mwaka huu, Yanga ikijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba.

Na baada ya kufanya mazoezi mfululizo wiki hii, ikiwa ni mara ya kwanza kufuatia kushindwa kufanya mazoezi japo kwa siku mbili mfululizo awali, kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina anatarajiwa kumtumia Tambwe katika sehemu ya mchezo wa leo.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dissmas Ten alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba Tambwe yuko fiti na atakuwepo kwenye mchezo wa leo.

Ten alisema majeruhi ambao wataendelea kukosekana katika kikosi hicho ni Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao wote wanapambana na hali zao warejee uwanjani mapema. 

Kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi alikuwa anasumbuliwa na Malaria naye anaweza kukosekana katika mchezo wa pili mfululizo leo, baada ya kutokuwepo pia wakati Yanga ikiichapa 5-0 Mbeya City Jumapili iliyopita.

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliendelea jana kwa mchezo mmoja tu, wenyeji Ndanda FC wakilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi nyingine za leo, Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Kesho Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Zimbabwe: Morgan Tsvangirai aomba Mugabe kusamehewa



Kiongozi wa chama cha ZANU-PF Lovemore Matuke amesema kuwa hakushiriki katika harakati za kumuondoa Mugabe madarakani.

Kwa mujibu wa habari,Matuke amesema kuwa Mugabe na familia wako salama na daima atakumbukwa kama shujaa.

Wakati huohuo kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai amewataka wananchi wamsamehe Mugabe.

Morgan Tsvangirai amesema kuwa ni vyema Mugabe akasamehewa na taifa kwani si taifa halijengwi kwa kulipiza visasi.

Misri: Rais al Sisi aahidi adhabu kali kwa wliohusika na shambulizi dhidi ya mskiti Sinai


Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi aahidi adhabu kali kwa magaidi waliohusika na ashambulizi dhidi ya mskiti lililopelekea vifo vya watu zaidi ya 230  Sinai

Rais wa Misrii Abdel Fatah al Sisi ameahidi adhabu kali kwa magaidi waliohusika na shambulizi walilotekeleza  katika mskiti wakati wa kutekelezwa ibada ya Ijumaa.

Watu 235 walifariki na wengine zaidi ya 130 kujeruhiwa katia shambulizi lililolenga mskiti wa al Arish unaopatikana Sinai nchini Misri.

Jeshi la Polisi litatoa jibu linalostahili kwa waliotekeleza shambulizi hilo.