JESHI la Polisi mkoani Geita linawashikilia watu wawili wakazi wa Kijiji cha Kasubuya wilayani Nyang’wale kwa kula njama wakiwa wazazi kupokea mahari ya ng’ombe saba na kumwozesha mwanafunzi wa kidato cha pili.
Binti huyo aliyekuwa anasoma katika shule ya sekondari Nyijundu, sasa ana ujauzito.
Aliyethibitisha kukamatwa kwa wazazi hao wa pande zote mbili ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson na kuwataja ni baba mzazi wa msichana huyo, Herman Makanika (48) na Maximillian Makila ambaye ni baba mzazi wa mtuhumiwa aliyemuoa mwanafunzi huyo.
Ingawa hakulitaja jina la mtuhumiwa, Kamanda Mpojoli alimpongeza mwalimu wa shule ya sekondari aliyetoa taarifa za kuwapo kwa tukio hilo na akabainisha jinsi wazazi wa pande zote mbili walivyoshiriki kutenda kosa licha ya mtuhumiwa kutoroka.
Alisema wazazi wa pande zote mbili wanahusika ingawa mtuhumiwa (muoaji) anaendelea kusakwa, hivyo wanapaswa kuwajibika kutokana na kufanya makubaliano kwa kutoa mahari ya ng’ombe saba na mzazi wa msichana kuwapokea ng’ombe hao kama mahari.
Aliongeza kuwa baada ya polisi kuarifiwa ilichukua hatua za haraka na watuhumiwa kukamawta na hadi jana walikuwa wanaendelea kushikiliwa huku juhudi za kumsaka mtuhumiwa zikiendelea kuhakikisha anapatikana na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment