Monday 22 January 2018

Shule ya Makuti Mtwara yaanza kukarabatiwa


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara QS Omary Kipanga, amesema ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Mitambo iliyopo kata ya Msimbati ambayo iliripotiwa kuwa na madarasa ya makuti, unaendelea shuleni hapo.

Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv Bw. Kipanga mesema ujenzi huo ni wa vyumba vitatu vya madarasa ambao serikali inasimamia, na kimoja ambacho kinajengwa kwa nguvu ya wananchi, pamoja na nyumba ya mwalimu.

“Vyumba vipo na vya matofali na vimeezekwa majengo matatu, lakini kuna ujenzi ambao unaendelea kwa nguvu za wananchi wa darasa moja, lakini na sisi halmashauri katika bajeti yetu ya mwaka 2017/18 tumetenga bajeti kwa ajili ya madarasa mawili na nyumba ya mwalimu, mpaka sasa vyumba vya madarasa vinavyotumika ni vyumba viatu, vingine vitatu vipo kwenye ujenzi”, amesema Mkurugenzi Kipanga.

Sambamba na hilo Mkurugenzi amekiri uwepo wa upungufu wa walimu, ambapo amesema tatizo hilo ni la nchi nzima na sio kwenye halmashauri yake peke yake, hata hivyo serikali inafanya jitihada za kutatua changamoto hiyo.

“Tuna changamoto ya walimu sio kwenye halmashauri yangu tu, ni nchi nzima, kwa sababu mimi katika halmashuri yangu nina upungufu karibu mia 5 na kitu, pale walimu 7, wanafunzi 437 na madarasa 7 yaani la kwanza mpaka la saba”, ameendelea kufafanua Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wa elimu ya sekondari Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara amesema ana tatizo kubwa la kuwepo kwa upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, kwani kwenye halmashauri yake ina uhaba wa walimu 71 wa masomo ya sayansi.

“Kwa upande wa sekondari masomo ya sanaa hatuna tatizo sana, ila kwa masomo ya sayansi mimi kwenye halmashauri yangu ina upungufu wa walimu takriban 71 kwa shule zote, lakini bado tuna mikakati ya kuhakikisha tunapata walimu wa mazoezi ili tuweke priority kwenye masomo ya sayansi”, amesema Mkurugenzi huyo.

Shule ya Mitambo ilianzishwa mwaka 2009, ambapo mwaka 2015 walihitimu wanafunzi wa darasa la saba kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa.

EATV.

No comments:

Post a Comment