Tuesday, 23 January 2018

Mdee, Bulaya ‘wachomoka’ kifungoni


Kifungo walichokuwa wakitumikia wabunge wa Chadema, Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Halima Mdee (Kawe) cha kutokuhudhuria shughuli za Bunge kimemalizika na wamesema wamerejea na kasi ileile.

Wabunge hao waliadhibiwa kwa azimio la Bunge Juni 5 mwaka jana kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge ambayo ni jumla ya siku 47, waliyokosa ukiondoa shughuli zote za mikutano ya kamati za Bunge.

Adhabu hiyo ilikwenda sanjari na kulipwa nusu mshahara na posho kwa kipindi chote walichotumikia adhabu hiyo wakituhumiwa kudharau kiti cha spika.

Mikutano mitatu waliyoikosa ni wa bajeti uliokuwa ukiendelea, wa saba uliofanyika kati ya Septemba 5 hadi 15 na mkutano wa tisa wa Novemba 7 hadi 17.

Makato ya mshahara na posho yamebainishwa katika Kanuni 75 ya Bunge inayosema: “Mbunge aliyesimamishwa kazi atatoka katika Bunge na hataingia tena katika sehemu yoyote ya ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”

Jana, kwa nyakati tofauti Bulaya na Mdee walizungumza na gazeti hili juu ya kurejea kwao, huku wakisema hawajutii kwa adhabu hiyo na hawatorudi nyuma au kutetereka katika kusimamia wanachokiamini.

“Nitaendelea kuwa Mdee yuleyule wa siku zote, kama walidhani wakinifungia mwaka nitabadilika. Hapana! Sitaraji kubadilika. Nimetumwa na wananchi wangu kusema ukweli na nitausema, sijaja kumpigia magoti mtu,” alisema.

Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), alisema wakati akitumikia adhabu hiyo amepata fursa ya kufanya shughuli kwa karibu za jimboni kwake na zile za Bawacha.

Naye Bulaya alisema: “Nimerudi bungeni tayari na leo (jana) nilihudhuria kamati yangu ya uwekezaji na mitaji.”

Alipoulizwa amejifunza nini kutokana na adhabu hiyo, alisema: “Bulaya wa kukosoa, Bulaya anayesimamia kile anachokiamini pasi na kuvunja sheria na taratibu hajabadilika, nitaendelea kuwakosoa.”

“Hata nilipokuwa natoka CCM kuja Chadema nilijua mambo kama haya ya kukamatana, kufungiana yatakuwapo kwa hiyo nilijipanga na wala hawanitetereshi, nimerudi na sitarudi nyuma,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment