Monday, 22 January 2018

Magogo yaliyokosa mmiliki bandarini kuuzwa wakati wowote kuanzia sasa



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema magogo 938 yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yatauzwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukosa wamiliki wa mzigo huo.

Maamuzi hayo yamekuja  baada ya Waziri Kigwangalla mwezi uliopita kufanya ziara ya kushitukiza bandarini hapo baada ya kupata taarifa kuwa kuna shehena hiyo ya magogo ambayo umiliki wake ulikuwa na utata.

Mhe. Kigwangalla alieleza kuwa magogo hayo yamekuwa bandarini kwa miaka 10 huku mengine yakiwa kwenye makontena 55 .

Kutokana na utata huo, Kigwangalla alitoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 kujitokeza wakiwa na nyaraka zote ili kuthibitisha kama kweli yalivunwa Zambia kama ilivyodaiwa au laah!.

“Kulikuwa na vikao mbalimbali ndani ya serikali kujadili suala hilo, na tumekubaliana kuyauza baada ya wahusika kutojitokeza kuthibitisha umiliki wake,” amesema Waziri Kigwangalla.

Waziri Kingwangalla amesema jukumu la kuyauza magogo hayo wamepewa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wanaoruhusiwa kisheria kufanya kazi hiyo, ambapo watashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS).

No comments:

Post a Comment