Kampuni ya Ontour Tanzania Limited imenunua kwa Sh30.9 milioni meno ya viboko tani 3.5 yaliyokuwa yakipigwa mnada na Serikali baada ya kukusanywa kwa miaka 14.
Mnada huo umefanyika leo Januari 29, mwaka 2018 jijini Dar es Salaam na kuongozwa na kamati maalumu ya mnada inayoundwa na maofisa wa Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), kuongozwa na Karerema Kwareh kutoka wizara hiyo.
Awali, Kwareh alieleza masharti ya mnada huo, huku sharti namba tano linalimtaka mnunuzi kununua mzigo wote likiibua mjadala kwa baadhi ya wanunuzi wakitaka liondolewe.
Licha ya kupingwa na wanunuzi, Kwareh amesema wazo hilo limechukuliwa na litafanyiwa kazi katika mnada ujao, si mnada wa leo.
Mfanyabiashara wa kwanza alitaka kununua meno hayo kwa Sh25.2 milioni lakini alizidiwa kete na mkurugenzi wa Ontour, Crey Kilasi aliyetoa Sh30.9 milioni.
Kaimu Mkurugenzi wa Tawa, Mabula Misungwi amesema meno hayo yameuzwa ili thamani yake isiendelee kushuka na hatua hiyo haiwezi kuwa chachu ya kuongezeka kwa ujangili.
"Nyara hizi huwa zina thamani yake na zinavyozidi kukaa huwa thamani inashuka. Meno haya ni yale yanayopatikana kutokana na vifo vya kawaida vya viboko na yale yanayokamatwa kwa majangili," amesema Misungwi.
Amesema meno ya kiboko yana soko kubwa ulaya ambako hutumika kutengenezea urembo na bidhaa nyingine za mapambo.
Akizungumza baada ya kufanikiwa kununua meno hayo, Kilasi amesema atatumia wastani wa miezi sita kutafuta soko.
"Soko lake kubwa ni Japan na China ambapo huyatumia kama mbadala wa meno ya tembo, bei yake inaweza ikafikia Dola 25 za Marekani," amesema Kilasi.
Amesema asilimia 60 ya meno hayo ndio inaweza kuuzika vyema sokoni, huku asilimia 40 yakiwa hayapo katika hali nzuri.