Sunday, 10 December 2017

Manchester United v Manchester City, nani kutoka kifua mbele leo


Manchester United wanawakaribisha majirani zao Manchester City hii leo katika mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa sana, vilabu hivi viwili vinaongoza mbio za ubingwa jambo ambalo linaufanya mchezo huu kuwa mgumu sana.

Mchezo hii sio mrahisi kwa upande wowote ule na United wamepoteza michezo saba kati ya michezo kumi na mbili ambayo wamekutana na katika siku za hivi karibuni Man City wanaonekana kuimarika kuliko United.

Derby ya leo ni tofauti sana na derby nyingi zilizopita kati ya timu hizi kwani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2013 Manchester United na Manchester City zinakutana huku wakiwa katika nafasi mbili za juu.

Wakati City wakiwa wamefunga mabao mengi ugenini (27) msimu huu, wenzao United wanaringa na rekodi ya uwanja wao wa nyumbani ambapo michezo 42 hawajafungwa huku wakiwa wameshinda 30.

Jose Mourinho anaonekana kuijenga na kuiimarisha sana United katika eneo lao la ulinzi ambapo hadi sasa wameruhusu nyavu zao kuguswa mara 9 tu katika uwanja wao wa Old Traford msimu huu.

Tayari Manchester City wameshashinda michezo 13 mfululizo na kama watakwenda kushinda mchezo wa leo dhidi ya United baasi wataifikia rekodi waliyoweka Arsenal 2001/2002 ya kushinda michezo 14 mfululizo.

Lakini Jose Mourinho ana rekodi mbovu mbele ya Pep Gurdiola ambapo michezo 19 waliyokutana Mou ameshinda 4 tu na tena ni mchezo 1 tu wa ligi alioshinda, akisuluhu 7na vipigo 8.

Mkuu wa mkoa aagiza waliotia mimba wanafunzi 20 wakamatwe



MKUU wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ameitaka polisi mkoani humo kuwakamata watu waliowatia mimba wanafunzi 20 ambao walishindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba mwaka huu.

Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa kikao cha bodi ya uteuzi wa wanafunzi waliofaulu na wanaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2018 na kuongeza kuwa wanafunzi hao wa kike ndiyo walioshindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba kutokana na kupata ujauzito kwenye mkoa huo.

“Naagiza polisi kuwakamata watu hao waliowatia mimba wanafunzi wakashindwa kufanya mitihani yao ya kumaliza darasa la saba mwaka huu,” alisema Ndikilo na kuongeza kuwa sheria ziko wazi kwa wanaowatia mimba wanafunzi hivyo wahusika hao wakamatwe wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Alisema haiwezekani kuwakalia kimya wahusika kwani wamewaharibia maisha watoto hao ambao ndoto zao zimeyeyuka kwa kukatishwa na watu wasio na utu hivyo.

Mvua yaharibu makazi Mtwara



Baadhi ya wakazi wa Kiangu na Chuno mjini Mtwara wamelazimika kuyahama makazi yao yaliyojaa maji baada ya mvua kunyesha.

Mvua ilinyesha usiku wa kuamkia jana Jumamosi Desemba 9,2017 saa nane usiku pasipo kukata hadi saa kumi na moja jioni. Mvua ilikata kwa muda na kuendelea kunyesha usiku hadi leo Jumapili Desemba 10,2017.

Katika maeneo hayo MCL Digital imeshuhudia wananchi wakiokoa mali zao ambazo zilikuwa zimelowa.

Miongoni mwa mali zilizoharibika ni magodoro, samani, majokofu na televisheni.

Baadhi ya vijana wamekuwa wakiwasaidia wazee kuhamisha mali na kuwaondoa maeneo yaliyozingiwa maji.

Mkazi wa Kiangu, Edith Mboni ameiomba Serikali kujenga mitaro itakayopeleka maji baharini ili kuwaondolea adha hiyo.

Amesema mtaro uliopo ni mdogo hivyo kutokana na wingi wa maji unashindwa kuhimili.

Mkazi mwingine, Hassan Mbarali  ameiomba Serikali kujenga miundombinu imara ili kuwaepusha na maafa ambayo yamekuwa yakijirudia mvua kubwa inaponyesha.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Desemba 8,2017 ilitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwapo vipindi vya mvua kubwa katika  maeneo ya ukanda wa Pwani.

Maeneo hayo ni mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Pia,  visiwa vya Unguja na Pemba.

Viongozi wakuu wa TFF kumzika Bendera



Viongozi wakuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Rais Wallace Karia na Makamu Rais Michael Wambura wataongoza ujumbe wa shirikisho katika mazishi Kocha wa zamani wa Taifa Stars, marehemu Joel Nkaya Bendera.

Bendera aliyefariki dunia Desemba 6, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, atazikwa leo Jumapili Desemba 10, 2017 makaburi ya Kijiji cha Manundu, Korogwe mkoani Tanga.

Ujumbe huo pia utamjumuisha Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la TFF, Mhe. Mohammed Abdulaziz, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Vedastus Lufano pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Kanda ya 12 (Mikoa ya Tanga na Kilimanjaro), Khalid Mohammed.

Khalid Mohammed atakuwa na wenyeji wengine ambao ni viongozi wa mpira wa miguu mkoa na wilaya za Tanga ambao wataungana familia pamoja na waombolezaji wengine kumpumzisha Mbunge huyo wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1995 hadi 2005) katika Jimbo la Korogwe Mjini.

Mwili wa marehemu Bendera umeagwa Jumamosi Desemba 9, mwaka huu asubuhi kwenye Viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Lugalo, Dar es Salaam. Enzi zake Joel Nkaya Bendera alifikia cheo cha Naibu Waziri Michezo mbali ya kuongoza mikoa ya Morogoro na Manyara kwa cheo cha Mkuu wa  mkoa.

Alberto Msando aikosoa UVCCM




Wakili msomi, Alberto Msando ambaye alijiunga na (CCM) amefunguka na kuwachana vijana wa chama hicho UVCCM baada ya viongozi wake kumdanganya  Dkt. John Pombe Magufuli juu ya idadi wa vijana wao.

Albert Msando aliomba nafasi kwa Rais Magufuli ili aweze kuwasema vijana wa CCM baada ya moja ya taarifa yao kusema wapo vijana wa CCM zaidi ya milioni sita jambo ambalo linapingana na taarifa zao wenyewe.

"Nimeazima taarifa ya utekelezaji na mpango mkakati naona mmesema kwamba UVCCM mpo milioni sita, je ni kweli? Kama vijana mtakuwa mnafanya mambo kama haya tutakuwa na nchi ya hovyo sana na chama cha hovyo sana, mmeandika takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya vijana wenye umri kati ya 14-35 ni asilimia 34 ya watu wote nchini. mara tu baada ya ukurasa wa nane, ukurasa wa tisa mmeandika kundi la vijana ni kubwa takwimu zinaonyesha sasa wamefikia asilimia 65 ya idadi ya watu nchini ina maana hatujijui tupo wangapi? alihoji Msando

Wakili Msomi Msando aliendelea kuonyesha mapungufu hayo ambayo yalikuwa na lengo la kumdanganya Rais John Pombe Magufuli

"Kwenye kitabu hiki mmemwambia Rais Magufuli kuwa vijana wa UVCCM mnafika milioni sita lakini kwenye jedwali la kweli mmeandika idadi ya vijana wa UVCCM kila mkoa 2013/2017 jumla walio hai ni milioni moja laki sita wasio hai ni laki nne sasa kwanini mumdanganye Rais?  Tukafanye kazi na hizi ndiyo takwimu zenu sasa hivi mnamwambia Rais tunakaribia milioni sita mnataka Rais aondoke akiwa na picha ya kuwa mpo zaidi ya milioni sita wakati mpo milioni moja laki tano, jamani hatuendi hivyo tunakata CCM mpya ya vijana wachapa kazi, wanachama wote ambao hawapo hai warudi, tupate wanachama wapya" alisema Msando.

ACT -Wazalendo wasitisha mchakato wa uchaguzi mdogo



Chama cha ACT -Wazalendo kimesitisha mchakato wa uchaguzi mdogo wa majimbo matatu na kata sita kikisubiri uamuzi wa Kamati Kuu.

Kaimu Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Dorothy Semu katika taarifa kwa makatibu wa mikoa ya Tanga, Tabora, Ruvuma, Arusha, Iringa, Pwani na Singida amesema kamati ya uongozi ya chama hicho katika kikao cha dharura cha Desemba 8,2017 mjini Dar es Salaam imetoa maelekezo mawili.

Amesema mosi; kwamba viongozi wa mikoa, majimbo na kata zenye uchaguzi wasitishe mchakato wa kushiriki uchaguzi mdogo.

Pili; Dorothy amesema mikoa itapokea maelekezo kuhusu uchaguzi mdogo kutoka ofisi ya katibu mkuu baada ya Kamati Kuu ya ACT -Wazalendo kukutana hivi karibuni.

Amesema kamati ya uongozi ya Taifa imefikia uamuzi huo kutokana na hali iliyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa kata 43 uliofanyika Novemba 26,2017.

Baadhi ya yaliyojitokeza amesema ni pamoja na kubinywa kwa demokrasia na vurugu zilizotokea katika maeneo mbalimbali.

“Hivyo, kamati kuu itafanya tathmini ya uchaguzi mdogo wa kata 43 na kutoa mwelekeo wa chama juu ya uchaguzi wa majimbo matatu na kata sita unaoanza mchakato Desemba 12,2017 na kukamilika Januari 13,2018,” amesema.

Mwananchi:

Hii ndio zawadi ya Manara kwa Papii Kocha baada ya kutoka jela



 Jumamosi ya December 9 2017 ni siku ya furaha kwa watanzania na wapenzi wa muziki wa dansi kwa ujumla, hiyo inatokana na Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli kutangaza msamaha kwa wafungwa wakiwemo msanii Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na Mwanae Papii Kocha.

Rais Magufuli ametangaza msamaha kwa Babu Seya na mwanae Papii Kocha akiwa mjini Dodoma katika maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania na muda mchache baada ya taarifa hizo kutoka watu mbalimbali tumeona wakioneshwa kufurahishwa na uamuzi huo wa Rais Maguli.

Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa club ya Simba Haji Manara ni moja kati ya watu waliooneshwa kufurahishwa na maamuzi hayo na kaamua kuandika hivi kupitia ukurasa wake wa instagram katika picha ya Papii Kocha akiwa kavaa jezi ya Simba.

“Nchi imezizima sababu yenu . Mungu ametenda miujiza kupitia kwa Rais wetu..uliitangaza Simba hadi gerezani..ntakuvalisha jezi mpya iliosainiwa na wachezaji wote🙏🙏…ila Wenger bado hajatwaa taji…. kama ulivyomuacha🙇🙇”>>> Haji Manara

Huo ni ujumbe wa Haji manara kupitia ukurasa wake wa instagram, kama utakuwa unakumbuka vizuri Babu Seya na watoto wake watatu akiwemo Papii Kocha walihukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2004 baada ya kukutwa na hatia ya kesi ya kubaka na kunajisi watoto 10.

Umoja wa kiarabu waitaka Marekani kufuta uamuzi wake kuhusu Jerusalem



Umoja wa kiarabu katika mkutano wake uliofanyika mjini Cairo umetolea wito Marekani kutupilia mbali uamuzi uliochukuliwa kuhusu jiji la Jerusalem.

Mawaziri wa mambo ya nje katika Umoja wa Kiarabu wametolea wito Marekani kutupilia mbali uamuzi kuhusu Jerusalem , uamuzi ambao unakiuka mikataba ya kimataifa iliyosainiwa kuhusu mji wa Jerusalem.

Umoja wa kiarabu unasema kuwa uamuzi wa Trump ni hatari na una kiuka mikataba ya kimataifa.

Wito umetolewa kwa ulimwengu mzima kukemea uamuzi wa Trump.

Kufuati uamuzi huo, Marekani haina vigezi kuwa mpatanishi katika mzozo baina ya Israel na Palestina.

Marekani yazidi kupata tabu kufuatia suala la mji wa Jerusalem



Ghasia zazuka mbele ya ubalozi wa Marekani baina ya waandamanaji na Polisi katika maandamano mjini Beyruth nchini Lebanon.

Ghasia rimeripotiwa kutokea  mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Beyruth  nchini Lebanon.

Maandamano hayo ymaefanyika kwa lengo la kuonesha ghadhabu kufuatia  uamuzi wa Marekani kutangaza kutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Polisi ililazimika kutumia gesi ya kusababisha machozi ili kuwasambaratisha waandamanaji waliokuwa wakielekea  katika ubalozi wa Marekani.

Kiongozi wa mamlaka ya wapalestina akataa kukutana na makamu wa rais wa Marekani



Kiongozi wa mamlaka ya wapalestina Mahmud Abbas hatokukutana na  makamu wa rais wa Marekani MiÄźke Pence katika ziara yake Mashariki ya Kati.

Mshauri wa nmasula ya kisiasa wa Mahmud Abbas  Bwana Majdi Haldi amesema kuwa uamuzi huo wa kiongozi wa mamlaka ya wapalestina kutokuonana na makamu wa rais wa Marekani umechukuliwa kufuatia uamuzi wa Trump kutangaza kuwa seirikali yake anatambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Mike Pence anatarajiwa kufanya ziara Palestina ili kuzungumzia  mazungumzo ya amani.

Korea Kaskazini yawekewa vikwazo na Korea Kusini


Korea Kusini imetangaza vikwazo vipya dhidi ya mashirika 20 mengine ya Korea Kaskazini, na watu kadha, ili kujibu jaribio la kombora pamoja na mradi wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Wizara ya fedha ilisema hatua hizo zinalenga kuzuia fedha kugharamia mradi wa silaha, kinyume cha sheria.

Karibu mashirika na watu hao wote, yamo katika sekta za benki na safari za meli, na tayari yamepigwa marufuku na Marekani.

Hatua hiyo inachukuliwa majuma mawili baada ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya kufyatua kombora ambalo linasemekana linaweza kufika pahala popote pale nchini Marekani.

Rais Magufuli aweka saini nyaraka za msamaha kwa wafungwa



Rais John Magufuli ametia saini nyaraka za msamaha alioutoa kwa wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.

Rais Magufuli ametia saini nyaraka hizo leo Jumapili Desemba 10,2017 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Msamaha huo aliutoa jana Jumamosi Desemba 9,2017 katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).

Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya kurekebisha tabia za wafungwa.

Taarifa ya Ikulu imesema Rais Magufuli amesisitiza kuwa pamoja na kutolewa msamaha huo, vyombo vya dola viendelee kusimamia sheria.

Amelitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha mali, yakiwemo mazao ya kilimo na kufanya kazi za ujenzi.

“Nimeona nitumie kifungu hiki cha Katiba -Ibara ya 45 (1) ambacho nilipewa na Watanzania, ingawa kilikuwa hakijawahi kutumika, unajua mtu ambaye alihukumiwa kunyongwa halafu baadaye anaachiwa, ni kitu kinashangaza kwa sababu hakijawahi kutokea, lakini nimeona nifanye hivyo kwa ajili ya Watanzania,” amesema.

Rais Magufuli amesema, “Muendelee kusimamia wajibu wenu na kusimamia sheria, mtu anayehukumiwa kufungwa afungwe kweli, na nilishatoa wito kwa magereza, pasiwepo wafungwa wa kukaa tu na kupumzika, wafanye kazi, kufungwa si kustarehe.”

Akizungumzia hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa amemshukuru Rais kwa kutoa msamaha huo wa kihistoria.

Amesema wafungwa na maofisa Magereza wameipongeza hatua hiyo ambayo itasaidia kuwatia moyo wafungwa wanaorekebishwa tabia katika magereza nchini.

Kamishna Jenerali Malewa amesema wafungwa waliopatiwa msamaha wa kuachiwa huru, waliruhusiwa kutoka magerezani tangu jana.

Amesema maofisa Magereza wamewaasa kwenda kuonyesha mfano bora kwenye jamii watakakokwenda kuishi.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza agizo lake la kutengeneza viatu kwa ajili ya askari badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.

Jeshi la Magereza linazalisha jozi 150 za viatu kwa siku katika kiwanda cha Karanga kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa kushirikiana na mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF, jeshi hilo limeanza kuboresha kiwanda hicho ili kufikia uzalishaji wa jozi 450 kwa siku.

Mwananchi:

Hii ndio sababu itakayompelekea Guardiola kustaafu



Kocha wa Manchester City Pep Guardiola, amesema atastaafu kufundisha soka endapo kitafika kipindi ambacho timu atakayokuwa anaifundisha itashindwa kucheza mfumo wake wa kumiliki mpira yaani (TIKTAKA).

Guardiola ameyasema hayo kwenye mkutano na wanahabari kuelekea mchezo wa leo wa ligi kuu ya EPL dhidi ya mahasimu wao Manchester United. Alipoulizwa atafanya nini endapo aina ya soka analofundisha halitafanya kazi, amejibu, “nitastaafu”.

"Kama hilo litatokea, nitastaafu kwa sababu sitajisikia vizuri kuona mpira hauchezwi vizuri”, ameongeza kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Mtaalam huyo wa ufundi raia wa Hispania amesisitiza kuwa anatamani kuona mpira ukichezwa zaidi kuliko aina nyingine ya mbinu hivyo hawezi kuendelea kufunisha wakati kitu anachokifurahia hakipo tena.

“Tangu mchezo wangu wa kwanza na timu B ya Barcelona nilifundishwa kucheza soka la kuvutia hadi naanza kufundisha soka timu B ya Barcelona nilifundisha ‘TIKTAK’ na nilifanya hivyo na timu ya wakubwa na timu zingine nilizofundisha”, amemaliza Guardiola.