Sunday, 10 December 2017

ACT -Wazalendo wasitisha mchakato wa uchaguzi mdogo



Chama cha ACT -Wazalendo kimesitisha mchakato wa uchaguzi mdogo wa majimbo matatu na kata sita kikisubiri uamuzi wa Kamati Kuu.

Kaimu Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Dorothy Semu katika taarifa kwa makatibu wa mikoa ya Tanga, Tabora, Ruvuma, Arusha, Iringa, Pwani na Singida amesema kamati ya uongozi ya chama hicho katika kikao cha dharura cha Desemba 8,2017 mjini Dar es Salaam imetoa maelekezo mawili.

Amesema mosi; kwamba viongozi wa mikoa, majimbo na kata zenye uchaguzi wasitishe mchakato wa kushiriki uchaguzi mdogo.

Pili; Dorothy amesema mikoa itapokea maelekezo kuhusu uchaguzi mdogo kutoka ofisi ya katibu mkuu baada ya Kamati Kuu ya ACT -Wazalendo kukutana hivi karibuni.

Amesema kamati ya uongozi ya Taifa imefikia uamuzi huo kutokana na hali iliyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa kata 43 uliofanyika Novemba 26,2017.

Baadhi ya yaliyojitokeza amesema ni pamoja na kubinywa kwa demokrasia na vurugu zilizotokea katika maeneo mbalimbali.

“Hivyo, kamati kuu itafanya tathmini ya uchaguzi mdogo wa kata 43 na kutoa mwelekeo wa chama juu ya uchaguzi wa majimbo matatu na kata sita unaoanza mchakato Desemba 12,2017 na kukamilika Januari 13,2018,” amesema.

Mwananchi:

No comments:

Post a Comment