Viongozi wakuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Rais Wallace Karia na Makamu Rais Michael Wambura wataongoza ujumbe wa shirikisho katika mazishi Kocha wa zamani wa Taifa Stars, marehemu Joel Nkaya Bendera.
Bendera aliyefariki dunia Desemba 6, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, atazikwa leo Jumapili Desemba 10, 2017 makaburi ya Kijiji cha Manundu, Korogwe mkoani Tanga.
Ujumbe huo pia utamjumuisha Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la TFF, Mhe. Mohammed Abdulaziz, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Vedastus Lufano pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Kanda ya 12 (Mikoa ya Tanga na Kilimanjaro), Khalid Mohammed.
Khalid Mohammed atakuwa na wenyeji wengine ambao ni viongozi wa mpira wa miguu mkoa na wilaya za Tanga ambao wataungana familia pamoja na waombolezaji wengine kumpumzisha Mbunge huyo wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1995 hadi 2005) katika Jimbo la Korogwe Mjini.
Mwili wa marehemu Bendera umeagwa Jumamosi Desemba 9, mwaka huu asubuhi kwenye Viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Lugalo, Dar es Salaam. Enzi zake Joel Nkaya Bendera alifikia cheo cha Naibu Waziri Michezo mbali ya kuongoza mikoa ya Morogoro na Manyara kwa cheo cha Mkuu wa mkoa.
No comments:
Post a Comment