Saturday, 25 November 2017

Mbeya City yafanya mabadiliko haya



Klabu ya soka ya Mbeya City imelazimika kubadili jezi yake iliyokuwa imepanga kuitumia kwenye mechi ya ugenini leo dhidi ya Singida United.

Mbeya City imefikia uamzi huo baada ya kuwepo kwa mfanano kati ya jezi yake ya Singida United ambao ni wenyeji wao katika mchezo wa leo.

Jezi hizo ni kama zinavyoonekana hapo chini ambapo kushoto ni jezi ya wenyeji Singida United na kulia ni jezi ya Mbeya City iliyokuwa imepangwa kutumika leo.



Hata hivyo bado Mbeya City hawajasema ni jezi gani ambayo watatumia lakini msimu huu jezi zao za pili kwaajili ya mechi za ugenini ni zile zenye rangi ya damu ya mzee hivyo huenda ndio zitakazotumika leo.

Singida United inayoshika nafasi ya 5 ikiwa na alama 17 inacheza leo na Mbeya City yenye alama 11 katika nafasi ya 10 kwenye mchezo wa raundi ya 11, uwanja wa Namfua mjini Sungida.

Kocha wa Simba awaambia wachezaji wake kutowadharau Lipuli katika mechi yao Kesho



KOCHA wa Simba, Joseph Omog amewataka wachezaji wake kutowadharau wapinzani wao wa kesho timu ya Lipuli ya Iringa na kuwataka kuwa makini kwa dakika zote 90.

Akizungumza kabla ya kuanza mazoezi ya jana kwenye uwanja wa chuo cha Polisi Kurasini, Omog, alisema kuwa hawatakiwi kuwabeza wapinzani wao hao kwa kuwa mpira ni mchezo wa makosa.

“Hakuna timu ndogo kwenye ligi, wachezaji nimekuwa nikiwaambia hivyo, lazima nidhamu ya mchezo ifuatwe, kama wachezaji watafuata maelekezo tuna nafasi nzuri ya kushinda,” alisema Omog.

Alisema kuwa kwenye mazoezi ya timu hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Sportpesa, amekuwa akikazania wachezaji wake kucheza soka la kasi na kuhakikisha wanatumia vyema nafasi wanazozipata.

“Kwanza naangalia zaidi ushindi kabla ya kutazama wingi wa mabao, kama tutatengeneza nafasi nyingi na kuzitumia vizuri tunaweza kupata ushindi wa mabao mengi,” aliongeza kusema Omog.

Alisema kuwa licha ya ugeni wa Lipuli kwenye ligi, anaamini nao wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mchezo huo wa kesho utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

“Walipata pointi moja walipokuja hapa kucheza na Yanga.., kwa hiyo si timu ya kubeza, tutapambana kwa ajili ya pointi tatu,” aliongezea kusema Omog.

Simba ipo kileleni kwa msimao wa ligi ikiwa na pointi 22 sawa na Azam FC wanaoshika nafasiya pili lakini wekundu hao wa msimbazi wana magoli mengi.

Faiza Ally amuonyesha mpenzi wake mambo mapya


Muigizaji wa Filamu Bongo, Faiza Ally ameamua kumuweka wazi mpenzi wake mpya baada ya kuachana na Mr. Sugu aliyebahatika kupata naye mtoto mmoja aitwaye Sasha.

Mrembo huyo ametumia fursa ya mtandao wa kijamii wa Instagram kuweka picha akiwa na mwanaume huyo anayehisiwa  kuwa  baba mzazi wa mtoto wake wa pili wa kiume aliyempata miezi kadhaa iliyopita, picha hiyo imewaonyesha wawili hao wakiwa wanapigana busu zito.





Rais Magufuli ampongeza kikwete



Rais wa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa sifa na pongezi kwa rais mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kufanikisha ujenzi wa hospitali ya Mloganzila.

Rais ametoa pongezi hizo leo wakati akihotubia wananchi waliohudhuria ufunguzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila jijini Dar es salaam.

“Wakati ujenzi wa Hospitali hii unaanza mimi nilikuwa naagizwa tu na niliambiwa nikatafute eneo kubwa nikawaza nitalitoa wapi lakini baadae mzee Jakaya akanipigia tena simu  akaniambia kuna eneo huko Mloganzila ni la serikali nenda kaangalie na ujenzi uanze haraka, ndio nikaja hapa”, amesema Rais Magufuli.

Rais magufuli ameongeza kuwa “Watu tunapenda sifa lakini hizi sifa sio zangu ni za rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwani mimi nilikuwa naagizwa tu nikiwa waziri wa Ujenzi, ndio maana nimeona niseme wazi kuwa sifa zote zimwendee mzee Kikwete”.

Aidha rais Magufuli ameweka wazi kuwa wakati anakwenda kuona eneo la Mloganzila wala hakukuwa na barabara lakini aliambiwa na rais Kikwete aanze ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara haraka iwezekanvyo na alifanya hivyo sambamba na waziri wa maji amnbaye naye aliagizwa kuanza ujenzi wa miundombinu ya maji.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila jijini Dar es salaam ni mpango na jitihada za rais wa awamu ya nne.




Hiki ndio kikosi cha Yanga dhidi ya Tanzania Prisons leo



Yanga wanaokwenda Chamazi kuwava Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, leo, hawa hapa..

1. Youthe Rostand
2. Juma Abdul
3. Gadiel Michael
4. Andrew Vincent
5. Nadir Haroub
6. Pato Ngonyani
7. Pius Buswita
8. Raphael Daud
9. Obrey Chirwa
10. Ibrahim Ajibu
11. Emmanuel Martin

AKIBA:
 Beno Kakolanya
Hassan Kessy
Maka Edward
Yusuph Mhilu
Said Mussa
Geofrey Mwashiuya

Mali: Maafisa 4 wa UN wauawa



Umoja wa Mataifa umesema maafisa wake wanne walinda amani pamoja na mwanajeshi mmoja wameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa eneo la mpakani baina ya Mali na Niger.

Afisa mkuu anayekiongoza kikosi hicho cha walinda amani walioko Mali bw. Mahamat Saleh Annadif, bila kutaja washambulizi ni akina nani, amelaani vikali tukio hilo akisema ametamaushwa na kisa hicho dhidi ya maafisa wake ambao walikuwa wakiendeleza kazi ya udumishwaji wa amani na vilevile kutoa misaada hasa ya kimatibabu kwa wakaazi wa maeneo ambayo yamekumbwa na hali mbaya ya kuzorota kwa usalama.

Kuna makundi kadhaa ya wapiganaji yanayopatikana eneo hilo la Mali, yaliyo na uhusiano na kundi la Al Qaeda.

Umoja wa mataifa umekuwa na kikosi cha walinda amani huko Mali tangu 2013 wakisaidiwa pia na kikosi cha kijeshi cha Ufaransa.

Mbowe afunguka kuhusu kampeni za udiwani



Moshi. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wamewazidi CCM kimkakati katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika kesho  katika kata 43 nchini.

Mbowe amesema chama tawala hakina mpango mkakati wa kufahamu mambo gani wananchi wanataka na shida gani zinawakabili zaidi ya kuzungumzia kwa jumla na kujinasibu kufanya mambo makubwa ikiwamo kujenga barabara, kununua ndege na kupambana na mafisadi.

Amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa ndiyo maana katika kampeni za kuwanadi wagombea wa uchaguzi huo alinadi ajenda tatu ambazo ni dhana ya uhuru, maendeleo na demokrasia.

Mbowe amesema maendeleo hayapimwi kwa kununua magari, kujenga viwanja vya ndege, kupambana na mafisadi bali yanapimwa kwa maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

"Tunaaminishwa uchumi unakuwa kwa sababu nchi imenunua ndege, inapambana na mafisadi na inajenga viwanja vya ndege, hayo ni mambo mazuri hakuna anayepinga, lakini je, mwananchi wa kawaida ananufaika vipi," amesema Mbowe.

Amesema hali ya maisha ni ngumu, hivyo Serikali isijifungie na isizibe masikio kusikia wanacholalamika wananchi.

"Wananchi wana hali ngumu, sisi tuliozunguka na kuzungumza nao tunajua, biashara zinafungwa, wananchi masikini hali zao zimezidi kuwa ngumu, watumishi hawajapandishiwa mishahara hivyo hali kuzidi kuwa duni kwa wanaotegemea kuchuuza bidhaa kwa sababu hakuna anayemudu kununua," amesema Mbowe.

Amesema amani ya kudumu na demokrasia haiwezi kuwepo kama hakuna nafasi ya vyama vya siasa kufanya kazi zake bila kuonekana kama wahalifu.

Mbowe amesema wananchi wana kiu na shauku ya kuhudumia mikutano ya kisiasa.

Mwananchi:

Zitto Kabwe asema kinachotakiwa ni mabadiliko ya maendeleo kabla ya 2020


 

Mtwara. Kiongozi wa Chama wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kitendo cha kuchukua watu kutoka vyama vya upinzani siyo mafanikio bali kinachotakiwa ni kuwaletea wananchi mabadiliko ya maendeleo kabla ya mwaka 2020.

Zitto alisema hayo juzi katika mkutano wa kampeni za udiwani Kata ya Reli mjini Mtwara.

“CCM kazi yao sasa hivi ni kuchukua watu kutoka vyama vya upinzani, wanaona ni mafanikio wakisajili dirisha dogo. Huu mtaa wenu si ulikuwa hivi tangu mwaka 2015 kuna mabadiliko yoyote?

“Itakapofika mwaka 2020 mtaangalia wamechukua watu wangapi kutoka upinzani au mtaangalia mabadiliko kwenye mtaa wenu?” Alihoji Zitto.

Pia, alisema ameshangaa kuona foleni ya watu waliojipanga kwenye meli ya Wachina inayotoa huduma za afya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma akidai hiyo ni dalili ya kuonyesha kuna tatizo.

Aliendelea kusema kuwa maendeleo si idadi ya madaraja, bandari na barabara za juu zilizojengwa bali ni afya, elimu na uwezo wa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi.

Zitto alisema kwa sasa Tanzania inajenga reli lakini inachukua vyuma kutoka Uturuki ikiwa ni pamoja na kampuni ya kuponda kokoto kwa ajili ya ujenzi wa reli.

“Nchi ya aina gani, kuna haja gani ya huu uhuru ambao tunao mpaka sasa? CCM inaamini ninyi nyote mtawapa kura,” alisema.

Mgombea wa udiwani wa kata hiyo, Mwajuma Hassan alisema kwamba vipaumbele vyake ni kuhakikisha kila mkazi wa kata hiyo anajiajiri.

Pia, mgombea huyo aliahidi kusimamia huduma za kijamii kama afya, maji na elimu.

Mwananchi:

Waziri wa zamani wa fedha Zimbabwe afikishwa mahakamani




Aliyekuwa waziri wa fedha wa Zimbabwe,Ignatius Chombo amefika mahakamani kujibu mashtaka ya  ulaji rushwa dhidi yake.

Kwa mujibu wa habari,Chombo huyo alikamatwa wiki mbili zilizopita wakati jeshi lilipochukua utawala nchini humo.

Bwana Chombo alifukuzwa katika chama cha ZANU-PF Jumapili iliyopita.

Hata hivyo Chombo ameonekana akiingia mahakamani akiwa hana wasiwasi.

Emmerosn Mnangagwa ameapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe.Baada ya kuapishwa kwake rais huyo mpya ametakwa na baadhi ya wafuasi wake kulishughulikia kundi la G-40 linalosemekana kuwa lilikuwa likimuunga mkono Mugabe na mkewe.

Chombo alikuwa kati ya wanachama wa G40

Hii kali...Roboti iliyopewa uraia nchini Saudi Arabia yataka kuwa na familia



Roboti iliyopewa uraia nchini Saudi Arabia imesema kuwa ina haki ya kuwa na familia.

Roboti hiyo kwa jina la Sophia  ilitengenezwa nchini Hong Kong na kupewa uraia nchini Saudi Arabia mwezi uliopita.

Roboti hiyo İimesema kuwa ingependa kuwa na familia wakati ilipohudhuria mkutano wa habari ulioandaliwa nchini UAE.

Kwa mujibu wa habari roboti hiyo imesema kuwa familia ni kitu muhimu sana.

Robot hiyo imesema kuwa kila mwanadamu ana haki ya kuwa na familia na watu wenye hisia sawa na yeye.Jambo hilo ni muhimu sana hata kwa roboti.Aliwaambia wanadamu wajisikie furaha kuwa na familia.

Filamu mpya ya bollywood yazua mzozo nchini India



Filamu mpya ya Bollywood  ambayo bado haijazinduliwa imeleta kizaazaa baina ya viongozi wa juu nchini India.

Filamu hiyo kwa jina la Padmavati imepingwa vikali na wanasiasa wa chama tawala serikalini pamoja na makundi ya mrengo wa kulia hata kabla ya uzinduzi wake.

Maisha ya mtayarishaji wa filamu hiyo pamoja na waigizaji yapo hatarini kutokana na kuigizizwa kwa filamu hiyo.

Filamu inaelezea historia ya Malkia Padmavati wa dini ya kihindu wakati wa karne ya 14.

Malikia Padmavati alijichoma moto akiwa hai baada ya Mfalme Khalji ambae alikuwa ni muislamu kuwavamia na kumuua mumewe.

Waigizaji maarufu Deepika Padukone na  Ranveer Singh wamecheza kama Padmavati na Sultan Khalji.

Makundi yanayoipinga filamu hiyo yanadai kuwa filamu hiyo imebadilisha baadhi ya matukio ya kihistoria.

Hata hivyo mtayarishaji wa filamu hiyo amekana tuhuma hizo.

Baadhi ya watu kutoka katika Kabila la warajput pamoja na waumini wa kihindu wamepinga filamu hiyo kutokana na mahusiano ya kimapenzi yaliyoonyeshwa kati ya mfalme wa kiislamu na malkia wa kihindu.

Wamedai ni aibu kubwa na uvunjaji heshima kwa kabila lao.

Dk Shika kupanda jukwaani kumnadi mgombea wa CCM


Mwanza. Katika kampeni za lala salama leo, CCM itawapandisha jukwaani aliyekuwa mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi na Dk Louis Shika, aliyejizolea umaarufu baada ya kuibuka kwenye mnada wa nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi.

Katambi aliyejiunga na CCM akitokea Chadema na Dk Shika watamnadi kwa wapiga kura wa Kata ya Mhandu jijini Mwanza mgombea wake, Constantine Sima.

Katibu wa uenezi wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Mustapha Banigwa amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa wengine watakaopanda jukwaani katika mkutano utakaofanyika mtaa wa Machinjioni ni waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha aliyerejea CCM akitokea Chadema.

Mkutano huo pia utahutubiwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa mbunge wa Bunda, Stephen Wasira, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na mbunge wa Bukombe, Doto Biteko.

Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini utafanyika kesho Jumapili Novemba 26,2017.

Mwananchi:


Chadema yawaomba wapiga kura kukaa mita 100



Dar es Salaam. Chadema wamewataka   wapiga kura kukaa umbali wa mita 100  wakati wa kusubiri matokeo yao kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyia kesho katika kata 42 nchini, ili kulinda kura zao.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Jeshi la Polisi lilipinga wapiga kura kukaa umbali wa mita 100 na baadaye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhitimisha sakata hilo kwa kutamka kuwa kukaa umbali wa mita 200, baada ya kupiga kura hairuhusiwi.

Akielezea mwenendo wa uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema,  Benson Kigaila amesema  sheria inaruhusu wapiga kura kukaa umbali huo ili kulinda kura zao.

“Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inataka wapiga kura kusimama umbali wa mita 100, kwa hiyo tuwaambie wapiga kura wetu wakishamaliza kupiga kura wakae umbali wa mita hizo, waongeze na nyingine moja walinde kura zao,” amesema

Kigaila amewataka  wapiga kura hao kwenda kwenye vituo vya kupigia kura na kutimiza wajibu wao bila kuogopa kitisho chochote na baadaye walinde kura zao hadi zitakapotangazwa.

“Waende wakapige kura wasiogope kitisho chochote,” amesema a kuwataka baadaye waende kwenye makao makuu ya kata yatakako tangazwa matokeo hayo kuhakikisha, washindi wanatangazwa kwa haki.

Kiongozi huyo wa Chadema amesema kumekuwa matukio ya uvunjaji wa haki kwenye mikutano yao ya kampeni ikiwamo makada wake kuvamiwa na kupigwa.

“Upinzani ukishinda utatangazwa wapende wasipende, ambaye atatangaza matokeo tofauti ashughulikiwe kama mwizi mwingine wa kawaida kwa sababu wezi huwa wanashughulikiwa,”

“Kwa hiyo watu waende walinde haki yao ya kikatiba, wapige kura na walinde matokeo. Yatangazwe matokeo sahihi.” amesema  kiongozi huyo wa  Chadema