Tuesday, 23 January 2018

Watumishi wa serikali wapewa masaa 72

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe limetoa masaa 72 kwa watendaji 37 kutoka katika kata 15 wawe wamewasilisha kiasi cha milioni 73 walichokusanya kama mapato vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Watendaji hao wanadaiwa kukusanya fedha hizo katika kipindi cha robo mwaka kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na kubaki nazo majumbani mwao bila kuwasilisha kwa mweka hazina wa halmashauri.



Akisoma azimio la kikao cha Baraza hilo ambalo limekutana mjini Vwawa, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erick Ambakisye alisema uamuzi huo unafuatia kitendo cha watendaji hao kutowasilisha fedha za makusanyo katika kipindi kilichowekwa kisheria na kusababisha halmashauri kukosa mapato hayo ya Sh. 73,777,736.29 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Mwenyekiti huyo alisema sambamba na hilo baraza limechukua hatua ya kuwaonya kwa barua kwa mara ya pili watendaji wa kata 15 za Wasa, Magamba, Ipunga, Nyimbili, Myovizi, Itaka, Mlangali, Halungu, Isansa, Kilimampimbi, Nambinzo, Bara, Ruanda, Iyula na Shiwinga huku wengine 16 wakiwa wakishindwa kutumia mashine za kielektroniki katika kukusanya mapato ya halmashauri na kutakiwa kujieleza na kuwasilisha fedha walizokusanya ifikapo tarehe hiyo saa 4.00 asubuhi.

Aidha mwenyekiti huyo alisema ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato halmashauri yake iliweka mkataba na watendaji hao wenye lengo kukusanya asilimia 50 ya lengo la makusanyo katika kipindi cha kila robo na kutoa zawadi ya Sh. 500000 kwa kata ya kwanza itakayokusanya vizuri, Sh. 300000 (kata ya pili) na Sh.200000 (kwa kata ya tatu) na kutoa ngao ya kufanya vibaya kwa kata tatu zilizofanya vibaya.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo akizungumza wakati akitoa salamu za serikali alisema wilaya ina fursa ya vyanzo vingi vya mapato lakini watendaji wamekuwa hawakusanyi ipasavyo kutokana na kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa upande mwingine Mbozi alisema hatua kali lazima zichukuliwe kwa watendaji wanaoshindwa kukusanya mapato na kwamba ofisi yake itasimama imara kusaidia katika kuhakikisha halmashauri inakusanya mapato inayostahili.

No comments:

Post a Comment