Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itatuma wakaguzi kwa ajili ya kukagua mali za chama cha ushirika mkoa wa Mara.
Amesema Serikali imeanza kufuatilia mali za vyama vya ushirika nchini zikiwemo za chama hicho.
Waziri Majaliwa ametoa kauli hiyo jana, Januari 21 mwaka 2018 katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Amesema ukaguzi huo utakwenda sambamba na kufuatilia fedha wanazodai waliokuwa watumishi wa chama hicho.
“Kumekuwa na matatizo makubwa ndani ya vyama vya ushirika kiasi cha kudumaza maendeleo ya wananchi,” amesema.
Pia, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mhandisi Elius Mwakalinga kufanya tathimini ya ubora ya jengo la kituo cha pamoja cha forodha cha Sirari kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Amesema mkurugenzi huyo afanye tathmini na kuishauri Serikali kama jengo hilo linafaa kutumika.
Januari 17, Waziri Mkuu alikagua kituo hicho kilichopo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara na kusema hajaridhishwa na ujenzi wake kwa kuwa upo chini ya kiwango.
Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment