Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) imeanzisha mfumo wa kimtandao wa huduma za bima kwa wateja wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Akizungumza Kamishna wa TIRA, Dk Baghayo Saqware amesema mfumo huo unazitaka kampuni kuweka taarifa kwenye mtandao kwa mizigo inayoingizwa kutoka nje ya nchi na bima wanazotoza.
Hatua hiyo imekuja baada ya marekebisho ya Sheria ya Bima inayowataka waagizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi kutumia kampuni za ndani za bima.
Kabla ya marekebisho ya sheria hiyo, waagizaji wa mizigo nchini waliweza kutumia kampuni za bima za nje ili kupata kinga ya bidhaa zao.
Akifungua mafunzo ya wadau wa bima kuhusu namna ya kutumia mfumo wa kusimamia ulipaji wa bima kwa mizigo na bidhaa kutoka nje, Dk Saqware amesema utarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa ajili ya mamlaka za serikali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Takwimu Taifa (NBS).
Amesema mfumo huo utasaidia kufahamu kama sekta ya bima inakua ukilinganisha na ukuaji wa uchumi.
Dk Saqware amesema mfumo huo utazirahisishia mamlaka za serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kupata taarifa za bima kwa urahisi.
Amesema kampuni za bima na mawakala wataoshindwa kutoa taarifa zao kwenye mfumo wa mtandao huo watakuwa wanavunja sheria za nchi na hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Amesema utumiaji wa kampuni za ndani za bima utasaidia kampuni za bima, madalali na mawakala kukua kibiashara na kuongeza mapato.
Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT), Bosco Bugali alisema mtandao huo pia utawasaidia wanaodai fidia kulipwa kwa haraka na kwa ufanisi kwani hawatahangaika kuwasiliana na kampuni za bima za nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment