RAIS wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia pamoja na ujenzi wa bandari itakayotumika kusafirishia na kuingiza maliasili hizo.
Akiwa katika eneo hilo lililoko Mangapwani na Bumbwini lenye ukubwa wa hekta 399.25 juzi, Dk. Shein alipata maelezo kuhusu hatua zinazoendelea katika mradi huo.
Katibu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Ali Halil Mirza, alisema hatua inayoendelea hivi sasa ni upembuzi yakinifu unaotekelezwa na Benki ya Dunia ambao utakamilika miezi sita ijayo.
Mirza alisema kukamilika kwa upembuzi huo yakinifu ndiko kutaleta mapendekezo ya kulisanifu eneo hilo kwa ajili ya bandari na majengo mengine ya utawala na shughuli nyingine zinazoenda sambamba na mradi huo.
Alisema miongoni mwa sababu ya kutengwa eneo hilo kwa shughuli hizo ni kutokana na kuwa na kina kirefu cha maji ya bahari ambacho kitarahisisha kujengwa kwa bandari hiyo muhimu ambayo itatumika kwa ajili ya kusafirishia gesi asilia na mafuta ndani na nje ya nchi.
Alisema miongoni mwa faida kubwa za mradi huo baada ya kukamilika kwake ni pamoja na kuondoa kabisa uhaba wa mafuta nchini na kuipatia Serikali pato kubwa.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, akiwa na ujumbe wake alipata fursa ya kulikagua eneo la Kampuni ya Salama International linalojengwa maalum kwa ajili ya kusafisha mafuta na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Abdallah Said Abdallah.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa eneo hilo ambalo ni kwa ajili ya kusafisha mafuta limefikia asilimia 65 za ujenzi.Mkurugenzi huyo alieleza kuwa matenki ya uwezo wa kuhifadhi lita milioni 24 kwa wakati mmoja yanajengwa kwa ajili ya kuhifadhia diseli, petroli, mafuta ya taa pamoja na mafuta ya kulainisha mitambo.
Alieleza kuwa kuanzia mwezi ujao wataendelea na shughuli za ujenzi zilizobaki, shughuli ambazo zilianza mwaka 2015.
Alisema hadi walipofikia wameshatumia dola za Marekani milioni tano (sawa na zaidi ya Sh. bilioni 10) ikiwa ni awamu ya kwanza.
Alisema watakuwa wakisafisha tani 600 ambazo zitatumika Zanzibar kwa asilimia 70 na kiasi kilichobaki kitauzwa nje ya nchi.
Akiwa katika eneo hilo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya uhifadhi wa mazingira katika mchakato wa usafishaji wa mafuta mara mradi huo utakapokamilika.
No comments:
Post a Comment