BAADA ya kufunga bao pekee lililowapa ushindi Yanga dhidi ya Ruvu Shooting juzi, kiungo Pius Buswita, amewapa neno la faraja mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaeleza "sasa tunarudi kwenye kasi yetu".
Buswita, alisema mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa nafasi ya tatu wanayoshika kwenye msimamo wa ligi.
“Mashabiki wasiwe na hofu, taratibu tunarudi kwenye kasi yetu na tunaweza kufanya vizuri zaidi, lengo letu ni kuhakikisha tunashinda katika kila mchezo bila kuangalia matokeo ya wengine,” alisema Buswita.
Aidha, alisema kuwa timu hiyo bado ina nafasi ya kutetea ubingwa wao, jambo ambalo mashabiki wanapaswa kuwa na matumaini hayo.
“Ukiangalia hakuna tofauti kubwa ya pointi na timu inayoongoza ligi, tutaendelea kupambana kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu,” alisema Buswita.
Kiungo huyo wa zamani wa Mbao FC, juzi alifunga bao pekee wakati Yanga wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, ushindi huo umeifanya Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kukusanya pointi 25 huku Azam wakiwa na pointi 30 wakifuatiwa na Simba wenye pointi 29 (kabla ya mchezo wake wa jana dhidi ya Kagera Sugar)
No comments:
Post a Comment