MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Mzee Hassan Dalali ‘Handsome Boy’, ameanza harakati za kuhamasisha wanachama wa timu hiyo kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo amepanga kutembelea Tanga na Zanzibar kabla ya mikoa mingine.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mzee Dalali alisema kuwa tayari ameshaanza kuzunguka katika matawi mbalimbali ya Mkoa wa Dar kwa ajili ya kuhamasisha umoja na mshikamano kwa lengo la kuweza kutwaa ubingwa wa msimu huu.
“Tayari nimeshaanza ziara yangu ya kuzunguka matawi ya nchi nzima, kwa hapa Dar nimeshakwenda kuongea na wanachama wa matawi ya Mabibo na leo (jana) nitakwenda Gongo la Mboto, lengo kubwa ni kuhamasisha umoja na mshikamano wa matawi ambao kama ulitoweka lakini sasa umeanza kuzaa matunda kutokana na ushirikiano wa viongozi wa juu wa timu, nawapongeza sana.
“Hili nimeamua kufanya mwenyewe kwa mapenzi ya timu yangu kwa sababu ni muda mrefu umoja na mshikamano umekuwa kama umepotea lakini wiki ijayo nitakwenda Tanga kisha Zanzibar, ikizingatiwa tulikuwepo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, muda mrefu umepita sasa bila ya kuchukua ubingwa lakini kwa mabadiliko chini ya viongozi wangu ambayo wanayafanya, naamini tutafanikiwa na kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Mzee Dalali.
No comments:
Post a Comment