Tuesday, 23 January 2018

Chanjo saratani kutolewa bure


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuanzia Aprili, mwaka huu, itaanza kutoa bure chanjo dhidi ya kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi (human papillon virus) kwa wasichana wa kuanzia umri wa miaka 14.

Hatua hiyo inatokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kuonyesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na  wagonjwa wapya wa saratani ya mlango wa kizazi 51 kwa kila wanawake 100,000 huku vifo vikiwa 38 kwa kila wanawake 100,000, ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Naibu Waziri wa wizara hiyo Dk. Faustine Ndugulile, alisema hayo jana alipokuwa akizindua kampeni ya uchunguzi wa mabadiliko ya awali ya saratani hiyo na ya matiti, uliofanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.

 Alisema hatua hiyo ya chanjo inalenga kukinga kirusi kinachoeneza saratani ya mlango wa kizazi ambayo Tanzania inaongoza kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na wagonjwa wengi.

Aidha, alisema katika awamu ya kwanza ya utoaji wa chanjo hiyo mwaka huu wamepanga kuwafikia wasichana wa kuanzia miaka 14 wapatao 616,734. "Hawa 616,734 ndio tumepanga kuwapatia chanjo mwaka huu na katika mwaka ujao tutawafikia wasichana wa kuanzia miaka tisa hadi 14 na mwaka utakaofuata tutawapa chanjo wale wenye umri wa kuanzia miaka tisa," alisema Dk. Ndugulile. Alisema chanjo hiyo itasaidia kuwalinda wasichana ambao wako katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa virusi vinavyosababisha saratani ya matiti na mlango wa kizazi. "Saratani ya mlango wa kizazi moja ya sababu ambazo zinachangia ni wasichana kushiriki ngono katika umri mdogo, kuwa na wenza wengi lakini pia kubeba mimba nyingi kunaweza kusababisha mtu kupata maambukizi," alisema.

Hata hivyo, aliwataka kinamama kupima afya zao mara kwa mara na wanapobainika kuwa na maambukizi, wanatakiwa kuwaona wataalamu ili kupatiwa matibabu. "Saratani hii inatibika kabisa kama mtu atapata vipimo vya afya yake kila mara, lakini watu wengi wamekuwa wakija katika hospitali wakiwa wamechelewa sana hali ambayo saratani inakuwa imesambaa katika maeneo mengine ya mwili kama vile mifupa, ini na damu na kuwa vigumu kutibika,"alisema  Dk. Ndugulile aliwaagiza wakuu wa mikoa wote kuhakikisha kuwa wasimamia upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi katika mikoa yao ili kufikia malengo ya serikali iliyojipangia hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu iwe imefikia kimama milioni tatu.

Aliongeza pamoja na juhudi hizo pia serikali kwa sasa inaboresha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ambayo ni taasisi pekee nchini katika kukabiliana na tatizo la saratani, kwa kuweka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kutoa huduma za matibabu ambazo zilikuwa zinatolewa nje ya nchi.

 "Katika mwaka 2016 Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ilipokea wanawake 1,934 wa saratani ya mlango wa kizazi. Takwimu hizi zimekuwa zikongezeka si tu kwamba kujua ukubwa wa tatizo na hii itatusaidia kuona jinsi gani jamii imeamka na kuhamasika kufahamu athari za saratani na kuanza kuchukua hatua," alisema.

No comments:

Post a Comment