Vyama vya CCM na Chadema vinatarajia kuzindua kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni Jumamosi Januari 27,2018.
Wakati CCM ikisema itazindua kampeni katika viwanja vya Biafra; Chadema haijaweka wazi eneo la uzinduzi.
Uchaguzi katika jimbo hilo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya CUF, Maulid Mtulia kujivua uanachama wa chama hicho akisema anamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye alijiunga na CCM.
Mtulia amepitishwa na CCM kuwania tena ubunge jimboni humo ambako atachuana na Salum Mwalimu wa Chadema ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar.
CCM imeanza kwa kumtambulisha Mtulia katika vikao vya ndani na kwenye kata mbalimbali.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba amesema kampeni zitaanza saa sita mchana.
Amewaomba wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa hadhara.
Naye Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Itifaki wa Chadema, John Mrema amesema watazindua kampeni Kinondoni Jumamosi, ikiwa ni siku moja baada ya uzinduzi kufanyika katika jimbo la Siha.
“Jimbo la Siha kampeni zitafanyika uwanja wa Ngarenairobi na Kinondoni bado hatujajua ni wapi ila tutawaeleza. Kampeni hizi zitahudhuriwa na viongozi wakuu na ndiyo maana tumetofautisha siku ya uzinduzi,” amesema.
Uchaguzi katika jimbo la Siha unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya Chadema, Dk Godwin Mollel kujivua uanachama na kujiunga na CCM ambayo imempitisha kuwania tena nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment