Chama Kikuu cha Ushirika (Kacu), kimewatahadharisha wakulima wa tumbaku kuheshimu mkataba wa kampuni za ununuzi ili kusijitokeze kama yaliyowakuta msimu uliopita, baada ya zaidi ya kilo milioni tatu kukosa soko.
Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa Kacu, Emmanuel Peter baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi.
Alisema mwaka huu wakulima wameingia mkataba na kampuni za ununuzi kuzalisha kilo milioni nane za tumbaku, hivyo wanapaswa kulima bila kuzidi.
Mwaka jana, tumbaku iliyozidi kwa Kahama ilikuwa kilo milioni 3.25 ambayo ilikuwa ni ziada ya mkataba wa kuzalisha kilo milioni sita ambazo kampuni ziligoma kununua ziada hiyo.
Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya muda mrefu zilikubali kwa masharti ya kununua kwa bei ya dola 1.25 za Marekani (Sh2,700) kwa kilo kwa tumbaku ya daraja la kwanza badala ya Sh5,000 au Sh6,000 kwa bei iliyotumika awali.
“Wakulima acheni kulima nje ya idadi iliyopo kwenye mkataba wa kampuni za kununua, ili kujiepusha na usumbufu uliojitokeza kwa nchi nzima ni zaidi ya kilo milioni 20 zilizozidi hali iliyosababisha tumbaku kukaa muda mrefu ghalani na kukosa ubora,” alisema Peter.
Wanunuzi wakuu wa zao hilo ni kampuni ya TLTC na Alliance One.
Katika uchaguzi huo, Peter alifanikiwa kutetea nafasi yake baada ya kupita bila kupingwa huku makamu wake akichaguliwa Geofrey Mbuto.
Wajumbe wa bodi wanaokamilisha safu ni Tano Nsabi, Cecilia Shigemo, Patrick Songoro na Elias Madata huku mjumbe mwakilishi kutoka nje ya bodi akichaguliwa Benedicto Bulugu.
No comments:
Post a Comment