Kama unakumbuka, shabiki na mwanachama mkongwe wa Simba Chuma Suleiman maarufu kama Bi. Hindu alikuwa hataki kusikia kabisa habari za mambo ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ndani ya klabu yao hususan masuala ya hisa na kampuni.
Leo December 3, 2017 MO ameshinda kwa kishindo zabuni ya kuwekeza ndani ya Simba, baada ya MO kutangazwa mshindi na wanachama wengi waliohudhuria mkutano huo kuridhia, Bi Hindu alijitokeza na kwenda hadi MO kumpongeza.
ShaffiDauda.co.tz ikapiga story na bibi huyo kutaka kujua msimamo wake upo kwa sasa baada ya kuwa miongoni mwa wanachama waliokuwa wakipinga mchakato huo.
“ Tuliambiwa wanachama tutafukuzwa tutakuwa hatukanyagi klabuni, ndio kitu kilichokuwa kinaniuma rohoni kwa sababu klabu hii imejengwa na wauza vitumbua, wapasua kuni, lakini baada ya kueleweshwa nimeelewa na nipo safi. Atakaenifata kuniuliza nitamweleza akielewa ataungana na sisi kama hataki basi namuacha.”
Bi. Hindu amesema wapo watu watakaosema amevuta ‘mtonyo’ ili kukubali mabadiliko hayo ambayo yameridhiwa pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sambamba na serikali kupitia wizara inayosimamia masuala ya michezo.
“Kuna watu wanaweza wakasema nimepewa ‘kitita’ lakini mimi sipo huko, nipo katika kujenga Simba kwa sababu aibu inatukuta kila siku sisi mikono kichwani.”
No comments:
Post a Comment