Monday 4 December 2017

Wafanyabiashara waishauri Halmashauri kuboresha huduma ya Kodi


Chama cha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mbeya, kimeshauri Jiji la Mbeya kuangalia namna bora ya kuboresha na kukusanya tozo za kodi ya huduma kutoka kwa wafanyabiashara ili kuboresha kiwango cha huduma.

Mratibu wa TCCIA Mkoa wa Mbeya, Emily Malinza alibainisha hilo juzi jioni kwenye mkutano uliowakutanisha uongozi wa jiji la Mbeya, wadau wa masuala ya kodi na wafanyabiashara kwenye majadiliano ya pamoja kuhusu programu ya kukuza uwekezaji na biashara kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa jiji hilo.

Malinza alisema wafanyabiashara wamekuwa wakifika TCCIA kuuliza tozo za kodi wanazotozwa na jiji namna zinavyowanufaisha, kwa kukuwa wanatozwa tu lakini hawaoni huduma.

Wafanyabiashara wengi wanauliza tozo wanazolipa zinakokwenda, wakati hakuna huduma wanayoipata kutoka jiji kwa mujibu wa sheria inayoelekeza.

“Sasa jibu ni rahisi tu kwamba kodi inayochukuliwa ni chache kiasi hata matokeo yake hayawezi kuonekana,” alisema Malinza na kuongeza:

“Lakini TCCIA tunaamini kabisa kama kutaboreshwa huduma zitokanazo na tozo hizo, mapato yakaongezeka na hata huduma nyingine ambazo jiji linatoa zitaboreshwa.”

Akichangia katika mkutano huo, ofisa biashara Mkoa wa Mbeya, Stanley Kibakaya alisema licha ya majadiliano hayo kujitikiza zaidi kushusha kiwango vya tozo ili kupata makusanyo mengi zaidi, jiji liwe na mpango mkakati kukuza na kutangaza kujua umuhimu wa vyanzo vingine vya mapato.

“Ukiangalia kwenye ada za leseni za biashara, kila mara wanatangaza umuhimu wa kulipa ada za leseni na kuna mbinu kabisa kama hujalipa hatua zinazotakiwa kuchukuliwa,” alisema.

Naye mhasibu wa Jiji la Mbeya, Andrew Kiyungu alisema tayari wameandaa mpango mkakati wa kuwafikia wafanyabiashara ambao hawasajaliwa kwenye mfumo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) na wana leseni za biashara.

Kiyungu alisema mkakati huo umegawanywa katika makundi matatu ambayo ni wafanyabiashara wakubwa ambao wamesajaliwa na Vat hawataguswa na punguzo la kodi, watabakia kwenye tozo ya asilimia 0.3.

“Kundi la pili ni wafanyabiashara wa kati ambao wanalipa leseni kuanzia Sh100,000 hadi Sh200,000, menejimenti ya jiji ilipendekeza wakilipa Sh30,000 kwa kila mwezi itakuwa na afya kwa halmashauri na watawafikiwa wengi zaidi kwa bei nafuu na itasaidia kukuza mapato ndani,” alisema.

Alisema kundi la tatu ni wafanyabiashara wadogo ambao wanalipa leseni za biashara kuanzia Sh40,000 hadi Sh80,000, menejimenti ya jiji ilipendekeza kundi hiyo kulipa Sh15,000 kwa mwezi.

Alisema hatua zote hizo ni mkakati wa kuwafikia wafanyabiashara wengi wanaopaswa kulipa tozo ili kukuza mapato yatakayosaidia kuboresha huduma mbalimbali za jamii.

Naye kaimu mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Afrael Manase alisema ili wasonge mbele na kuboresha huduma kwa jamii, lazima sekta binafsi zishirikishwe kila hatua tofauti na hapo watashindwa kumudu utoaji huduma.

No comments:

Post a Comment