Wednesday, 31 January 2018

Halmashauri ya Kigamboni yapitisha rasmi sheria zake


Baada ya Halmashauri ya Kigambini kugawanywa mwaka juzi kutokea Temeke, Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limekutana na kupitisha sheria ndogo tisa ambazo zitatumika kuendesha halmashauri hiyo.

Sheria hizo mpya ambazo ndani yake kuna kanuni ni sheria ndogo za ushuru na huduma, ada na ushuru, matangazo, maegesho, uvuvi na rasimali za bahari ya hindi, masoko na magulio, usafi wa mazingira, burudani na sheria ya kudumu ya halmashauri.

Madiwani hao wamepitisha sheria hizo katika kikao chao cha pili cha robo cha baraza hilo kilichokuwa na ajenda 10 ikiwemo kupitisha sheria hizo na kanuni zake ili kuachana na sheria zilizokuwa zikitumika hapo awali ambazo zilikuwa ni za Halmashauri ya Temeke kabla ya kutenganishwa.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Stephen Katemba alisema mchakato wa kubadilisha sheria na kanuni hizo umepitia ngazi mbalimbali ikiwemo kushirikisha wadau na wananchi kuanzia ngazi ya mtaa hadi ya kata.

" Hizi sheria zikianza kutumika lazima wananchi watambue kuwa zitakua na adhabu kwa wale ambao watazikiuka, na faini ya makosa yake itaanzia Sh 200,000 hadi Milioni moja punde tu ambapo sheria na kanuni hizi zitaanza kutumika miezi michache ijayo," Alisema Katemba.

Kagame aanza kibarua chake cha AU kwa kasi


Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Paul Kagame ameanza kazi yake hiyo haraka baada ya kukutana na viongozi wa jukwaa la Biashara na Uwekezaji ambapo alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushikishwa kikamilifu kwenye masuala ya utawala.

Kagame ambaye pia ni Rais wa Rwanda alisema Serikali nyingi za Kiafrika awali ziligundua kuwa ni ngumu kuwatumikia wananchi kwa haraka na ubora bila sekta binafsi hivyo akaomba ziungwe mkono ili ziweze kurahisisha maendeleo.

Alisema anaamini mazungumzo yake hayo na wataalamu hao yataenda sawa na vitendo hivyo kutaka sekta binafsi ziungwe mkono ambapo anaamini sasa ushirikiano mkubwa baina ya watawala na sekta binafsi utaendelezwa ili kuongeza chachu ya mafanikio.

" Mfano sisi Rwanda tumeongeza ushirikiano na makampuni ya nje katika kusaidia sekta ya afya hii haina maana kuwa tunabinafsisha hapana bali tunaongeza ubora wa huduma ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu kwa haraka zaidi," Alisema Rais Kagame

Sosopi asema dawa ya muhuni ni kuwa muhuni zaidi yake


Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema, BAVICHA, Patrick Ole- Sosopi amekiri kuwa Chama chake kimeamua kurudi kwenye uchaguzi mdogo haswa wa Kinondoni na Siha kwa kuwa wamegundua dawa ya muhuni ni kuwa muhuni zaidi.

Akizungumza kwenye Kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa Kinondoni Salum Mwalimu Ole-Sosopi amesema kwamba kilichowafanya kususia uchaguzi mara ya kwanza ni kwamba hakukuwa na faida kubwa ya kupatikana kiongozi kwa wananchi wasio na hatia kwa kumwaga damu.

Ole-Sosopi amesema kwamba baada ya kususia uchaguzi ambao uligomewa kupelekwa mbele sasa wagundua kuwa "dawa ya muhuni ni kuwa muhuni zaidi hivyo ifahamike na iwekwe rekodi kuwa CHADEMA tumerudi kushiriki na kufanya uchaguzi".

Mbali na hayo Ole-Sosopi ameongeza kuwa hataki chama chake au kingine kisipendelewe bali waachwe wabishane kwa hoja na mwishowe wananchi waachiwe kufanya maamuzi.

CHADEMA walitangaza kugomea uchaguzi mdogo uliofanyika January 13 kwa madai mbalimbali ikiwepo kufanyia hujuma za wazi katika uchaguzi uliofanyika Novemba 26 huku tume ikilalamikiwa kutofanyia kazi malalamiko hayo.

King Majuto ammwagia sifa Rais Magufuli kwa uimara wake


Msanii mkongwe wa filamu za bongo, Mzee Majuto amefunguka na kudai yeye ndio mtu wa kwanza kutabiri ujio wa Rais Magufuli katika kuongoza nchi ya Tanzania huku akisisitiza kwamba anajisikia faraja kuona ana misimamo iliyokuwa imara.

Mzee Majuto amebainisha hayo muda mchache alipotembelewa na Rais Magufuli leo katika hospitali aliyolazwa ya Tumaini iliyopo Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa tezi dume unaomsumbua kwa kipindi kirefu.

"Mimi ndiyo mtu wa kwanza kumtabiri kwamba akiwa Rais itakuwa shughuli. Nilishukuru sana kuchaguliwa huyu bwana, tumepata Rais sio masihara watu wote sasa hivi wana adabu zao wanajua nini maana ya kazi ukisema jambo watu wanatekeleza, wezi wanakamatwa, wala rushwa wanakamatwa, wenye vyeti feki hata kama amefanya kazi miaka 20 fukuza, hii safi", alisema Majuto.

Pamoja na hayo, Mzee Majuto aliendelea kwa kusema "sisi wazee tunafarijika sasa hivi, viwanda kila kona vimetapakaa na leo amekuja kutembea hospitalini hapa sijui kama wengine hawajikojolea huko kwa uoga maana hataki masihara. Hii ndio raha ya kupata viongozi wenye msimamo".

Kwa upande mwingine, Mzee Majuto amesema kupata sio rahisi kupata Rais mwenye misimamo na asiyekuwa na masihara kama Dkt. John Magufuli.


Nabii Nyakia aeleza jinsi alivyotekwa na watu wasiojulikana


Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda jijini Dar, Nabii James Nyakia amesimulia alivyonusa kifo baada ya kutekwa na kuteswa kwa siku kadhaa na watu wasiojulikana.

Tukio hilo la kutisha lilimtokea nabii huyo mwaka jana alipokuwa akitangaza Injili huko Mkuranga mkoani Pwani.

Akizungumza na gazeti hili katika kanisa hilo baada ya kukimbia huko, Nabii Nyakia alisema kuwa, alikuwa katika program ya kutangaza habari njema wilayani humo ndipo siku moja akakutana na kundi ambalo baadaye alisikia ndilo lile la watu wasiojulikana ambao walimkamata akiwa msituni na kuanza kumtesa.

“Nilikuwa nimeamua kwenda kupeleka neon la Mungu vijiji mbalimbali vya Mkuranga.

“Nakumbuka siku moja nilikuwa katikati ya msitu mkubwa kwani Mkuranga imezungukwa na mapori na misitu.

“Nikiwa njiani kwenda kufanya mkutano wa Injili, ghafla walitokea vijana waliokuwa na silaha za kijadi kama marungu na mapanga. Pia kulikuwa na wachache waliokuwa na bunduki.

“Walinieleza kuwa hawakutaka kusikia habari za kueneza injili kwani walisema wao wanataka dini yao tu na nadhani walishanijua kwa sababu muda mwingi kazi hii ya Mungu niliifanyia huko.

“Niliwaomba sana wasiniue, lakini cha moto nilikiona maana kama ni kupigwa, nilipigwa sana. Kwa kifupi mateso hayakuwa ya kawaida.

“Nilichokifanya ilikuwa ni kumuomba Mungu kimoyomoyo na kumwita aniokoe au anipokee mikononi mwake kwani niliamini kama ni kufa, ningekufa nikiwa ninaitenda kazi ambayo Mungu ameniita kwayo.

“Baada ya maombi na mateso ya saa zaidi ya sita, wale jamaa nilisikia wakiambizana kwamba waliachie, lakini kwa onyo kwamba nisiendelee na shughuli hiyo.

“Waliponiachia nilirejea kwa mwenyeji wangu, lakini tulizidi kumwomba Mungu hadi tuliposikia baadhi yao walikamatwa na polisi na wengine kuuawa na sasa kuna utulivu wa kutosha,” alisema Nabii Nyakia akiwa na makovu ya mateso hao kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.

Chama cha Mitindo chazinduliwa rasmi leo



Baada ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) miezi mitatu iliyopita, kutaka wabunifu nchini kuanzisha chama kitachowakutanisha pamoja katika shughuli zao, leo Januari 31, Chama cha Mitindo Tanzania (FAT) kimezinduliwa rasmi.

Akizindua chama hicho, Katibu Mtendaji Basata, Godfrey Mngereza amesema uanzishwaji wake licha ya kuwainua wabunifu wachanga na wakubwa kutambulika kimataifa, utakuza viwanda vya pamba na ngozi nchini ambavyo vitategemea malighafi za ndani.

Mngereza amesema wabunifu wakijengewa utamaduni wa kutumia bidhaa za ndani kama ngozi na nguo kutengeneza mavazi yenye utamaduni wa ndani, wataendana na kauli ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda. Mngereza amesema Serikali inafanya kazi na chama kinachotambulika kisheria kikiwa kimesajiliwa hivyo kupitia chama hicho wataweza kuelekeza matatizo yao.

Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi (TAFCA), Adrian Nyangamalle amesema watahakikisha wanawasaidia katika changamoto mbalimbali zitakazotokea katika chama hicho.

“Tutatoa ushirikiano sehemu yoyote inayohitajika kuisukuma Serikali ili malengo ya chama hiki yatimie kwa haraka,” amesema Nyangamalle.

Mwanzilishi wa FAT, Asia Idarous amesema wamekuwa na changamoto mbalimbali katika tasnia hiyo, hivyo wanaishukuru Serikali kwa kutaka kuanzisha chama hicho kitakachowaunganisha na Serikali ili kuifikisha Sanaa hiyo kimataifa.

Gigy money aponda utaratibu wa Basata kuhusu video vixen



Gigy Money ameonyesha kutokubaliana na utaratibu wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) uliowataka ma-video vixen kujisajili katika Baraza hilo.

Muimbaji huyo ameiambia XXL ya Clouds Fm kuwa Basata walimueleza hilo lakini anaona kuna ma-video vixen wengi ambao hawajasalijiwa na wanafanya kazi hiyo.

“Waliniambia hivyo, lakini sasa Hamisa Mobetto anafanya nini, Tunda tuseme anafanya nini, officialnai anafanya nini, ma-video vixen unataka kuniambia wanajulikana Basata, why Gigy kwa sababu umeonekana ashapata chochote kitu,” amesema Gigy Money.

“Basata mtajalije utamaduni wa msanii mkiwa hamjali Ugali wake, haujali mfuko wake, wewe unaniona tu napendeza unajua mimi napoteza shilingi ngapi,”

Gigy Money kwa sasa anafanya vizuri na ngoma yake mpya inayokwenda kwa jina la Mimina baada ya kutamba na ngoma ‘Papa’.


Akutwa ameuwawa na mwili wake ukichunwa ngozi



Mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Mpande mkoani Songwe amekutwa amekufa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani huku akiwa amechunwa ngozi na kutolewa baadhi ya viungo vya mwili wake na watu wasiojulikana.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani hapo Yusuph Sarungi amesema ni kweli tukio hilo limetokea na wameweza kubahatika kumtambua kwa jina marehemu huyo kuwa ni Luntinala Tunyepa mwenye umri wa miaka ipatayo 75.

Aidha, Sarungi amesema mpaka sasa chanzo cha tukio la kuuawa mwanamke huyo hakijafahamika huku akisema wanaendelea na msako mkali ili kuweza kuwabaini watu hao waliotenda hivyo.

Msikilize hapa chini Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe Yusuph Sarungi akielelezea mkasa mzima wa tukio hilo.

Karia kuongoza ujumbe wa TFF mkutano wa CAF


Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limetoa taarifa leo kuwa viongozi wake watatu wa juu watakuwa ni miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria mkutano mkuu wa CAF.

Viongozi hao ni Rais wa TFF Wallace Karia, Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred.

Mkutano huo mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF utafanyika Februari 2, 2018 nchini Morocco.

Morocco ni mwenyeji wa michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN zilizoanza Januari 13 na leo ni hatua ya nusu fainali ambapo wenyeji Morocoo wanacheza na Libya huku Sudan wakikipiga na Nigeria.

Shule iliyoongoza kidato cha nne yataja siri ya ufaulu


Baada ya shule ya Sekondari ya wasichana ya St. Francis Mjini Mbeya kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa jana wameeleza kuwa bidii ya walimu na wanafunzi ndio siri ya mafanikio hayo.

Wakizungumza na EATV  baadhi ya walimu akiwemo Mwalimu wa Somo la Kemia ambaye pia ni Mwalimu wa Nidhamu katika Shule hiyo, Neema Kimani, Mwalimu Msaidizi wa Taaluma Reginald Chiwangu bidii na kumtanguliza Mungu ndio siri ya mafanikio hayo.

''Kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, bidii ya walimu na wanafunzi, utawala bora na kusikiliza ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ndio vimechangia shule yetu kuongoza kitaifa'', wamesema.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo akiwemo Joyce Msigala, Lorette Leone na Bibiana Karumuna wamesema kuwa matokeo hayo yametoa mwanga wa jinsi gani  walijiandaa ili kufanya vizuri kwenye mtihani wao.

Wahitimu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya St. Francis waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ambao ndio wameongoza kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza walikuwa 92.

EATV.

Nape aipongeza Serikali kuhusu umeme na kuipa ushauri


Mbunge Nape Nnauye leo Bungeni ameipa changamoto Serikali juu ya gharama za kuunganisha umeme na kuishauri kuendelea kuchaji elfu 27,000 hata baada ya mradi REA kupita ambapo wataanza kuchaji 177,000 kuunganisha umeme.

Nape Nnauye ametoa ushauri huo alipopata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Bungeni kwenda kwenye Wizara ya Nishati

"Kwanza niipongeze Serikali chini ya Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayofanya ya usambazaji mzuri wa umeme vijijini hasa REA awamu ya 3, kwa kuwa gharama za kuunganisha umeme wakati mradi unaendelea ni elfu 27,000 na mradi ukipita ni 177,000 na kwa kuwa idadi kubwa na nzuri ya watumiaji wa umeme ni biashara nzuri kwa TANESCO kwanini bei hii isiwe moja ya elfu 27" alisema Nape Nnauye

Hata hivyo Nape Nnauye aliendelea kusisitiza kuwa kama jambo hilo halitawezekana basi REA waendelee na uwekaji wa nguzo na miundombinu na TANESCO wafanye kazi moja ya kupeleka umeme na kukusanya kodi baada ya kupeleka umeme.

Naibu Waziri Wizara ya Nishati alijibu hoja hiyo na kudai kuwa amepokea ushauri huo wa Mbunge wa Mtama na kuwa atapeleka katika ngazi zingine na kuona Serikali nini itafanya

"Wazo alilosema Kaka yangu Nape Nnauye linapokelewa na litafanyiwa kazi kwani ni la msingi kwa sababu Wizara yetu na shirika letu la TANESCO na wadau wengine wa nishati tunauza bidhaa hii hivyo ni vema tunapouza tupate wateja wengi ili tupate mapato na kuendesha shughuli mbalimbali na uwekezaji mpya wa maeneoya nishati"

Mbunge aliyesimamia kuapishwa kwa Odinga atiwa mbaroni


Jeshi la Polisi nchini Kenya, leo Januari 31, 2018 mchana limemtia mbaroni mbunge wa Jimbo la Ruaraka, Tom J Kajwang’, ambaye alisimamia “kuapishwa” kwa kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga kwenye viwanja vya Uhuru Park jana Jumanne.

Kajwang amekamatwa na maofisa hao waliokuwa wamevalia kiraia nje ya Mahakama ya Milimani jijini Nairobi muda mfupi baada ya kuhudhuria katika Mahakama Kuu mbele ya Jaji George Odunga kusikiliza uamuzi wa kesi aliyowawakilisha wabunge wanaopinga kukatwa mishahara yao na posho nchini humo.

Kajwang’ na mwanasheria mwingine Miguna Miguna, ndiyo walisimamia matukio yote ya “kuapishwa” Odinga kama ‘rais wa watu’ katika viwanja vya Uhuru Park. Imeelezwa kuwa, Kajwang’ alikuwa amevaa vazi na wigi ambapo alish

Wasanii wa filamu watoa msaada wa vifaa tiba

Wasanii wa filamu kutoka taasisi ya ‘Binti Filamu Foundation’ yenye wanawake kumi wa kundi la waigizaji la Bongo Muvi, leo wametoa msaada wa vifaa-tiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 30 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, mmoja wa wasanii hao, Halima Yahya ‘Davina’ alisema:
“Tumejipanga kuwafikia wanawake na mabinti wengi zaidi ili kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwaeleza jinsi ya kukabiliana na masuala ya ukatili kwa wanawake na tutajikita zaidi kwenye afya kwani tunaaamini malengo hayo hayawezi kutimia bila afya bora.

“Hivyo tumeamua kuanza na kampeni rasmi katika hospitali tukihamasisha wadau, makampuni na wananchi kwa ujumla kuwekeza katika afya, kuunga mkono juhudi za serikali za awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli yenye kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Binti Filamu Foundation kwa udhamini mkubwa wa Scientific Suppliers pia tumetoa vifaa-tiba vyenye thamani ya Sh. milioni 30 kuunga mkono juhudi za serikali kujali afya ya mama na mtoto.”

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Wilaya ya Kinondoni ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Benjamin Sitta, amesema wasanii wanapaswa kuwa nguzo kubwa katika jamii na wanasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo nchini. Akaongeza kuwa wasanii wengi wana ushawishi mkubwa katika jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo, Mganga Mkuu Mfawidhi katika hospital hiyo, Isdory Kiwale, amesema wanashukuru msaada huo huku akiwahakikishia kuwa vifaa hivyo vitatumika kama vilivyo kusudiwa.

Malengo makuu ya taasisi hiyo ni kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na raia wengine kama vile ukeketaji, ndoa za utotoni, mauaji ya albino na vikongwe na mengine yananyolenga kudhalilisha utu wa mwanadamu.