Wednesday, 31 January 2018

Chama cha Mitindo chazinduliwa rasmi leo



Baada ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) miezi mitatu iliyopita, kutaka wabunifu nchini kuanzisha chama kitachowakutanisha pamoja katika shughuli zao, leo Januari 31, Chama cha Mitindo Tanzania (FAT) kimezinduliwa rasmi.

Akizindua chama hicho, Katibu Mtendaji Basata, Godfrey Mngereza amesema uanzishwaji wake licha ya kuwainua wabunifu wachanga na wakubwa kutambulika kimataifa, utakuza viwanda vya pamba na ngozi nchini ambavyo vitategemea malighafi za ndani.

Mngereza amesema wabunifu wakijengewa utamaduni wa kutumia bidhaa za ndani kama ngozi na nguo kutengeneza mavazi yenye utamaduni wa ndani, wataendana na kauli ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda. Mngereza amesema Serikali inafanya kazi na chama kinachotambulika kisheria kikiwa kimesajiliwa hivyo kupitia chama hicho wataweza kuelekeza matatizo yao.

Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi (TAFCA), Adrian Nyangamalle amesema watahakikisha wanawasaidia katika changamoto mbalimbali zitakazotokea katika chama hicho.

“Tutatoa ushirikiano sehemu yoyote inayohitajika kuisukuma Serikali ili malengo ya chama hiki yatimie kwa haraka,” amesema Nyangamalle.

Mwanzilishi wa FAT, Asia Idarous amesema wamekuwa na changamoto mbalimbali katika tasnia hiyo, hivyo wanaishukuru Serikali kwa kutaka kuanzisha chama hicho kitakachowaunganisha na Serikali ili kuifikisha Sanaa hiyo kimataifa.

Gigy money aponda utaratibu wa Basata kuhusu video vixen



Gigy Money ameonyesha kutokubaliana na utaratibu wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) uliowataka ma-video vixen kujisajili katika Baraza hilo.

Muimbaji huyo ameiambia XXL ya Clouds Fm kuwa Basata walimueleza hilo lakini anaona kuna ma-video vixen wengi ambao hawajasalijiwa na wanafanya kazi hiyo.

“Waliniambia hivyo, lakini sasa Hamisa Mobetto anafanya nini, Tunda tuseme anafanya nini, officialnai anafanya nini, ma-video vixen unataka kuniambia wanajulikana Basata, why Gigy kwa sababu umeonekana ashapata chochote kitu,” amesema Gigy Money.

“Basata mtajalije utamaduni wa msanii mkiwa hamjali Ugali wake, haujali mfuko wake, wewe unaniona tu napendeza unajua mimi napoteza shilingi ngapi,”

Gigy Money kwa sasa anafanya vizuri na ngoma yake mpya inayokwenda kwa jina la Mimina baada ya kutamba na ngoma ‘Papa’.


Akutwa ameuwawa na mwili wake ukichunwa ngozi



Mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Mpande mkoani Songwe amekutwa amekufa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani huku akiwa amechunwa ngozi na kutolewa baadhi ya viungo vya mwili wake na watu wasiojulikana.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani hapo Yusuph Sarungi amesema ni kweli tukio hilo limetokea na wameweza kubahatika kumtambua kwa jina marehemu huyo kuwa ni Luntinala Tunyepa mwenye umri wa miaka ipatayo 75.

Aidha, Sarungi amesema mpaka sasa chanzo cha tukio la kuuawa mwanamke huyo hakijafahamika huku akisema wanaendelea na msako mkali ili kuweza kuwabaini watu hao waliotenda hivyo.

Msikilize hapa chini Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe Yusuph Sarungi akielelezea mkasa mzima wa tukio hilo.

Karia kuongoza ujumbe wa TFF mkutano wa CAF


Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limetoa taarifa leo kuwa viongozi wake watatu wa juu watakuwa ni miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria mkutano mkuu wa CAF.

Viongozi hao ni Rais wa TFF Wallace Karia, Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred.

Mkutano huo mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa CAF utafanyika Februari 2, 2018 nchini Morocco.

Morocco ni mwenyeji wa michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN zilizoanza Januari 13 na leo ni hatua ya nusu fainali ambapo wenyeji Morocoo wanacheza na Libya huku Sudan wakikipiga na Nigeria.

Shule iliyoongoza kidato cha nne yataja siri ya ufaulu


Baada ya shule ya Sekondari ya wasichana ya St. Francis Mjini Mbeya kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa jana wameeleza kuwa bidii ya walimu na wanafunzi ndio siri ya mafanikio hayo.

Wakizungumza na EATV  baadhi ya walimu akiwemo Mwalimu wa Somo la Kemia ambaye pia ni Mwalimu wa Nidhamu katika Shule hiyo, Neema Kimani, Mwalimu Msaidizi wa Taaluma Reginald Chiwangu bidii na kumtanguliza Mungu ndio siri ya mafanikio hayo.

''Kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, bidii ya walimu na wanafunzi, utawala bora na kusikiliza ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ndio vimechangia shule yetu kuongoza kitaifa'', wamesema.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo akiwemo Joyce Msigala, Lorette Leone na Bibiana Karumuna wamesema kuwa matokeo hayo yametoa mwanga wa jinsi gani  walijiandaa ili kufanya vizuri kwenye mtihani wao.

Wahitimu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya St. Francis waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ambao ndio wameongoza kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza walikuwa 92.

EATV.

Nape aipongeza Serikali kuhusu umeme na kuipa ushauri


Mbunge Nape Nnauye leo Bungeni ameipa changamoto Serikali juu ya gharama za kuunganisha umeme na kuishauri kuendelea kuchaji elfu 27,000 hata baada ya mradi REA kupita ambapo wataanza kuchaji 177,000 kuunganisha umeme.

Nape Nnauye ametoa ushauri huo alipopata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Bungeni kwenda kwenye Wizara ya Nishati

"Kwanza niipongeze Serikali chini ya Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayofanya ya usambazaji mzuri wa umeme vijijini hasa REA awamu ya 3, kwa kuwa gharama za kuunganisha umeme wakati mradi unaendelea ni elfu 27,000 na mradi ukipita ni 177,000 na kwa kuwa idadi kubwa na nzuri ya watumiaji wa umeme ni biashara nzuri kwa TANESCO kwanini bei hii isiwe moja ya elfu 27" alisema Nape Nnauye

Hata hivyo Nape Nnauye aliendelea kusisitiza kuwa kama jambo hilo halitawezekana basi REA waendelee na uwekaji wa nguzo na miundombinu na TANESCO wafanye kazi moja ya kupeleka umeme na kukusanya kodi baada ya kupeleka umeme.

Naibu Waziri Wizara ya Nishati alijibu hoja hiyo na kudai kuwa amepokea ushauri huo wa Mbunge wa Mtama na kuwa atapeleka katika ngazi zingine na kuona Serikali nini itafanya

"Wazo alilosema Kaka yangu Nape Nnauye linapokelewa na litafanyiwa kazi kwani ni la msingi kwa sababu Wizara yetu na shirika letu la TANESCO na wadau wengine wa nishati tunauza bidhaa hii hivyo ni vema tunapouza tupate wateja wengi ili tupate mapato na kuendesha shughuli mbalimbali na uwekezaji mpya wa maeneoya nishati"

Mbunge aliyesimamia kuapishwa kwa Odinga atiwa mbaroni


Jeshi la Polisi nchini Kenya, leo Januari 31, 2018 mchana limemtia mbaroni mbunge wa Jimbo la Ruaraka, Tom J Kajwang’, ambaye alisimamia “kuapishwa” kwa kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga kwenye viwanja vya Uhuru Park jana Jumanne.

Kajwang amekamatwa na maofisa hao waliokuwa wamevalia kiraia nje ya Mahakama ya Milimani jijini Nairobi muda mfupi baada ya kuhudhuria katika Mahakama Kuu mbele ya Jaji George Odunga kusikiliza uamuzi wa kesi aliyowawakilisha wabunge wanaopinga kukatwa mishahara yao na posho nchini humo.

Kajwang’ na mwanasheria mwingine Miguna Miguna, ndiyo walisimamia matukio yote ya “kuapishwa” Odinga kama ‘rais wa watu’ katika viwanja vya Uhuru Park. Imeelezwa kuwa, Kajwang’ alikuwa amevaa vazi na wigi ambapo alish

Wasanii wa filamu watoa msaada wa vifaa tiba

Wasanii wa filamu kutoka taasisi ya ‘Binti Filamu Foundation’ yenye wanawake kumi wa kundi la waigizaji la Bongo Muvi, leo wametoa msaada wa vifaa-tiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 30 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, mmoja wa wasanii hao, Halima Yahya ‘Davina’ alisema:
“Tumejipanga kuwafikia wanawake na mabinti wengi zaidi ili kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwaeleza jinsi ya kukabiliana na masuala ya ukatili kwa wanawake na tutajikita zaidi kwenye afya kwani tunaaamini malengo hayo hayawezi kutimia bila afya bora.

“Hivyo tumeamua kuanza na kampeni rasmi katika hospitali tukihamasisha wadau, makampuni na wananchi kwa ujumla kuwekeza katika afya, kuunga mkono juhudi za serikali za awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli yenye kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Binti Filamu Foundation kwa udhamini mkubwa wa Scientific Suppliers pia tumetoa vifaa-tiba vyenye thamani ya Sh. milioni 30 kuunga mkono juhudi za serikali kujali afya ya mama na mtoto.”

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Wilaya ya Kinondoni ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Benjamin Sitta, amesema wasanii wanapaswa kuwa nguzo kubwa katika jamii na wanasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo nchini. Akaongeza kuwa wasanii wengi wana ushawishi mkubwa katika jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo, Mganga Mkuu Mfawidhi katika hospital hiyo, Isdory Kiwale, amesema wanashukuru msaada huo huku akiwahakikishia kuwa vifaa hivyo vitatumika kama vilivyo kusudiwa.

Malengo makuu ya taasisi hiyo ni kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na raia wengine kama vile ukeketaji, ndoa za utotoni, mauaji ya albino na vikongwe na mengine yananyolenga kudhalilisha utu wa mwanadamu.


Meya Sitta Apokea Msaada Wa Vifaa Tiba Vyenye Thamani Ya Milioni 30



Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamini Sitta amepokea vifaa tiba vitakavyotumika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es salaam vyenye thamani ya Shilingi milioni 30 kutoka kwa taasisi ya Binti Filamu Foundation ambayo inaundwa na wasanii kumi wa filamu nchini Tanzania.

Meya Sitta ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa vifaa hivyo ikiwa ni lengo la kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta ya afya  hususani mama na mtoto ambao ni wahitaji wakubwa wa misaada hiyo.
"Ninafurahi na naawapongeza Binti Filamu Foundation kwa kutoa msaada huu na iwe chachu kwa wasanii wengine kuiga mfano kama wenu kwa kusaidia jamii yenye mahitaji kuliko kila siku kuigwa na kuandikwa mabaya, lazima mtumie akili zenu ili watu waige yaliyo  mazuri, amesema Meya sitta.

Kwa upande wake mlezi na mshauri wa Taasisi hiyo Bi, Asha Baraka amesema kuwa lengo ni kusaidia watoto, kinamama na baadae wazee ili kuunga jitithada za Mama Janeth Magufulli ambae anasaidia wazee na kina mama ambao hawana uwezo.


Nae Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dr. Isdory Kiwale ameishukuru taasisi hiyo kwani siyo mara ya kwanza kufika hospitalini hapo na kutoa msaada walishanya hivyo kipindi ilipohitajika damu ili kuokoa maisha ya watu, walijitolea kutoa damu.

Akisoma risala mbele ya mgeni Halima Yahaya amesema kuwa Binti Filamu Foundation imefikia kina mama zaidi  ya elfu 7 Tanzania bara na visiwani  huku wakitoa elimu kupinga unyanyasaji wa kijinsia ambao upo kwenye jamii ya Kitanzania.

 Aidha kupitia mpango huu tunashirikiana na taasisi mbalimbali za wanawake  kama vile jukwaa la wanawake  ambapo huendesha kampeni ijulikanayo kama ''ELIMIKA NA BINTI FILAMU'' mwaka 2016/2017 na mwaka huu kauli mbiu ni ''Silaha ya mwanamke ni malengo'' ikiwa lengo na la kuwafikia wanawake zaidi ili kuwaelimisha kuhusiana na unyanyasaji na pia kusaidia sekta ya afya  kwani malengo hayawezi kufikiwa bila kuwa na afya bora.



Tuesday, 30 January 2018

VIDEO: Rosa Ree akana Bifu na Navy Kenzo, Chemical

RAPA anaefanya vizuri kwenye kiwanda cha Bongo Fleva, Rosa Ree amekana kuwa na bifu na wakali Navy Kenzo, Chemical. Rosa Ree ameyasema hayo alipokuwa akitambulisha ngoma yake mpya kwa mara ya kwanza ndani ya Muungwana TV inayoitwa Marathoni ambayo amempa shavu hitmaker wa Sina Jambo, Bill Nas


TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI .............USISAHAU KUSUBSCRIBE..............

Mshindi wa pili kidato cha nne amtaja Mungu na wazazi wake


Elizabeth Mangu, mshindi wa pili Kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne  amesema kumtanguliza Mungu katika kila kitu  ndoto ya kuwa wa kwanza, bidii kwenye masomo na usimamizi wa karibu wa wazazi na walimu ndiyo  siri ya mafanikio yake.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Mwanza leo Januari 30, Elizabeth amesema  tangu alipojiunga kidato cha kwanza, alijiwekea lengo la kushika nafasi ya kwanza katika mitihani ya Taifa na aliwafuata walimu wake kuomba ushauri wa kufanikisha lengo hilo.

“Niliweka lengo la kushika nafasi ya kwanza kama alivyofanya Robina aliyeongoza mitihani ya kitaifa akitokea shule yetu ya Marian Girls; nilimfuata Mwalimu wa taaluma Ihonde na mwenzake wa Civics anayeitwa Mwanduzi kuwaomba ushauri wa kufanikisha hilo,” anasema na kuongeza

“Wote walinishauri kuzingatia masomo, kusoma pamoja na kusaidia wenzangu darasani kama njia ya kujifunza, kuzingatia maelekezo ya walimu na wazazi shuleni na nyumbani pamoja na kumcha Mungu kama mwanzo wa hekima,”

Akizungumza mbele ya mama yake mzazi, Wande Mandalu ambaye ni mwalimu katika shule ya Sekondari ya Kiloleli jijini Mwanza, Elizabeth alisema mwongozo na ukali wa wazazi wake aliposhuka kitaaluma pia imesaidia mafanikio yake.

“Nawashauri wazazi wawe karibu na kufuatilia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani hadi shuleni na kuwatia moyo wanapofanya vema bila kuacha kuwaonya na kuwakaripia wanapokosea,” amesema

Kauli hiyo iliungwa mkono na mama yake, Wande Mandalu pamoja na Mwalimu wake wa masomo ya dini katika Kanisa la KVCC, Geofrey Lugwisha waliosema liha ya kuwajenga watoto katika imani ya kiroho, wazazi wana wajibu wa kuwasaidia watoto wao kielimu, kuwapongeza na kuwaonya wanapopotoka.

“Wazazi lazima tuwe wasimamizi wa karibu kwa kufuatilia nyendo za watoto kuanzia nyumbani, shuleni hadi mitaani; lazima wajua ratiba na kuwapa miongozo inayofaa maishani, hasa msisitizo kwenye elimu ambayo ndio urithi wa kudumu,” amesema  Mwalimu Mandalu, mama wa watoto watatu

Eliza ni mtoto wa pili katika familia yake ya watoto watatu akitanguliwa na kaka yake Joseph Mangu na mdogo wake, Carren Mangu aliyesoma kidato cha kwanza shule ya wasichana ya Marian.

Mashabiki wa Arsenal wamuona Aubameyang kama Henry mpya


Mashabiki wa Arsenal tayari wamenunua jezi ya Pierre-Emerick Aubameyang yenye namba 14, wakati nyota huyo wa Dortmund akiwa njiani kwenda Emirates.

Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wameonekana wakiwa wamevaa jezi ya mshambuliaji huyo wa Dortmund ikiwa na jina lake namba 14, namba hiyo ilikuwa kivaliwa na mshambuliaji Thierry Henry na Theo Walcott.

Gunners sasa inakimbizana na muda katika kukamilisha utakaovunja rekodi wa pauni 55.4milioni kwa nyota huyo wa Gabon (28).

Hiyo itampa nafasi Aubameyang kuungana na nyota mwenzake wa zamani wa Dortmund Henrikh Mkhitaryan alijiunga na Arsenal akitokea na Manchester United kwa kubadilishana na Alexis Sanchez wiki iliyopita.

Ujio wa Aubameyang unamweka katika wakati mgumu mshambuliaji Alexandre Lacazette aliyesajiliwa mwanzo wa msimu huu kwa pauni 46.5milioni akitokea Lyon.

Hata hivyo uamuzi wa shabiki kupiga picha akiwa na jezi ya Aubameyang umepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wengine wa Emirates.

Taarifa zinasema kuwa Arsenal wamekubali kununua nyota huyo ambaye anatagemewa kuaga Borussia Dortmund ndani ya saa 24 zijazo.

Shabiki mmoja alitweeted: Love you Aubameyang." Lakini wenzake wakamjibu "Acha kwanza asaini."

Straika wa Uganda aitamani VPL


Straika Hood Mayanja, anayekipiga katika klabu ya African Lyon, inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza, amesema anajitahidi kufanya vizuri ili timu iweze kurudi Ligi Kuu.

Mayanja aliondoka nchini na baadaye kurudishwa kwa kazi moja tu, kuifanya timu hiyo irudi juu sasa isiporudi atakuwa ajatimiza ndoto yake.

"Niliitwa kwa kazi moja tu kuhakikisha kwamba timu inarejea Ligi Kuu, mimi nilikuwa muda mrefu hapa nikaona nirudi nije kupambana iweze kufanya vizuri turejee juu, lakini natakiwa kushirikiana na wenzangu ili tuweze kusogea," alisema.

Aliongeza kwamba, kadri miaka inavyozidi kwenda ndio ligi daraja hilo linazidi kuwa ngumu, hivyo kama wakifanikiwa kupanda, hawatoleta mzaha tena.

"Miaka inavyozidi kwenda ndio ugumu wa ligi unazidi kuonekana yaani, sasa kama tukifanikiwa kupanda hatutoleta masihara badala yake tutahakikisha kwamba tunasalia katika ligi," alisema.

Mayanja aliondoka klabuni hapo msimu uliopita, wakati timu hiyo ikiwa inashiriki Ligi Kuu na kujiunga na Mbeya City, lakini alijikuta na wakati mgumu badala yake akatimkia kwao Uganda, lakini amerejea tena nchini na anapambana kuirudisha upya timu hiyo katika Ligi.