Monday, 29 January 2018

Ang'oa paa la nyumba anayoishi mke wake


Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la David Kinyua mkazi wa Gichiche nchini Kenya ameng'oa mabati ya nyumba anayoishi mke wake ambaye anadai amempangisha, akimtuhumu amekaa muda mrefu ndani ya nyumba hiyo kinyume na makubaliano.

Kwenye tukio hilo ambalo limeleta sintofahamu kwa majirani, limeelezwa kwamba Bwana Kinyua ambaye ni mume wa Juliet Karimi alifanya tukio hilo, ili mke wake huyo aweze kuhama na kupisha mpangaji mpya.

“Nilipanga kukarabati nyumba baada ya Julieti kutoka, ili mpangaji akija akute nyumba yenye hali ya kupendeza, lakini amekataa kutoka, na alisaini makubaliano kama mpangaji kufuata utaratibu”, amesema bwana Kinyua.

Upande wa mke wake Bi. Juliet Karimi ambaye ndiye mke alikutwa na balaa hilo, amesema ameshangaa kuona watu wamekuja kutoa paa la nyumba kwenye nyumba anayoishi, na hata haelewi ni kwa namna gani aliishia kuwa mpangaji kwenye nyumba aliyoshiriki kujenga.

'Nilichangia kiuchumi kwenye kujenga nyumba hii, nashangaa haya yanatokea, naomba wanaohusika na masuala ya sheria inisaidie nipate haki yangu”, amesema Julieth ambaye amepangishwa kwenye nyumba aliyoshiriki kujenga yenye vyumba vinne.

Majirani wa wawili hao wamesema wanamfahamu Juliet kama mke wa David, na sio mpangaji kama anavyodaiwa.


Mourinho aweka rekodi nyingine Man Utd


Kocha wa Manchester United Jose Mourinho ametimiza mechi 100 tangu ajiunge na timu huku akiwa na wastani mzuri wa ushindi akiwazidi makocha waliomtangulia akiwemo Sir Alex Ferguson.

Mourinho ambaye alijiunga na United majira ya kiangazi mwaka 2016 amedumu na klabu hiyo kwa msimu mmoja na nusu sasa, na hivi karibuni ameongeza mwaka mmoja kwenye mkataba wake uliokuwa unamalizika 2019.

Katika mechi zake 100 Mourinho amefanikiwa kuiongoza United katika mechi za EPL 62 ambapo ameshinda 34, sare 20 na kufungwa 8. Katika mechi 6 za UEFA Mourinho ameshinda 5 na kupoteza moja.

Kwa upande wa EUROPA Mreno huyo ameshinda mechi 10 akitoka sare mara tatu na kupoteza mbili. Kwa upande wa Kombe la FA amecheza mechi 6 akishinda 5 na kupoteza moja. Kombe la Ligi EFL kocha huyo ameshinda mechi saba na kupoteza mbili.

Kwa upande wa makocha waliomtangulia Ferguson alishinda mechi 48, Moyes ambaye alikomea mechi 51 alishinda 27 pekee huku Louis Van Gaal akishinda mechi 52. Mourinho yupo juu yao akiwa ameshinda jumla ya mechi 62.


Mwijage atoa rai kwa uongozi wa Chuo cha CBE




Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ameutaka uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kutoa elimu ya ujasiriamali ili wahitimu waweze kujiajiri.

Akizindua bodi ya CBE jana, Mwijage alisema ujasiriamali liwe somo la lazima ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.

“Katika zama hizi na tunakokwenda, kuajiriwa itakuwa zilipendwa, hivyo tuwafundishe vijana ili wawe na uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri,” alisema Mwijage.

Alifafanua kuwa zamani wahitimu wa vyuo vikuu walitegemea ajira za Serikali lakini sasa hali iko tofauti.

Mwijage alisema chuo hicho kinatakiwa kutoa elimu itakayowasaidia kuwa na mbinu nyingi za ubunifu na kujiajiri.

Mwenyekiti mpya wa bodi, Ester Ishengoma alimhakikishia waziri kuwa bodi hiyo inafuata maelekezo yake kwa lengo la kukiboresha chuo hicho.

Kumbe Ngassa bado anaidai Mbeya City



Kiungo mshambuliaji wa Ndanda FC, Mrisho Ngassa, amesema kuwa amechoka usumbufu wa kuidai klabu yake ya zamani, Mbeya City, mshahara wake wa miezi minne, lakini akasisitiza anaomba fedha zake.

Ngassa alijiunga na Ndanda hivi karibuni katika usajili wa dirisha dogo akitokea Mbeya mara baada ya mkataba wake kumalizika kabla ya kugoma kumuongezea mwingine.

Ngassa alisema kuwa anaidai klabu hiyo shilingi milioni 4.8 alizotakiwa alipwe tangu Desemba, mwaka jana.

Ngassa alisema amefikia hatua ya kuweka wazi madai hayo baada ya hivi karibuni viongozi wa timu hiyo kumwambia watampatia fedha hizo baada ya kulipwa fedha kutoka Azam TV ambao wanadhamini klabu za ligi kuu.

“Nimechoka kuongopewa na viongozi wa Mbeya City, kwani kila wakati nikiwapigia simu kudai malipo yangu ya mshahara ambayo ni shilingi milioni 4.8 wamekuwa hawapokei simu.

“Lakini hata wakipokea wakati mwingine wananipiga Kiswahili, kwa maana ya kunitajia siku nyingine na hivi karibuni walinipa maneno mazuri ya kuwa watanilipa fedha zangu baada ya wao kulipwa na Azam TV.

“Ninajua tayari wamepatiwa fedha hizo, lakini wamejikausha kunilipa fedha hizo ambazo ninadai hadi leo (jana Jumapili), hivyo nimechoshwa nao, naomba wanilipe fedha zangu,” alisema Ngassa aliyewahi kuzichezea Simba, Yanga na Azam FC.


Alipotafutwa jana mchana, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema hayupo katika nafasi nzuri kuzungumzia suala hilo.

Kampeni za Kinondoni CHADEMA, CCM wazidi kutifuana


Wagombea ubunge jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia (CCM) na Salum Mwalimu (Chadema) wameendelea kujinadi katika mikutano ya kampeni, huku Mtulia akiwashangaa wanaobeza kujiondoa kwake CUF na kujiunga na chama tawala.

Wakati Mtulia akimwaga sera leo Jumatatu Januari 29, 2018 katika uwanja wa Hananasif Kinondoni, Mwalimu alikuwa uwanja wa Mtambani kata ya Mzimuni.

Tangu kuanza kwa kampeni hizo, hoja ya hamahama ya madiwani na wabunge imekuwa ikitawala kutokana na CCM kujikita kuzungumzia sababu za mgombea wake wa Kinondoni, Mtulia kuteuliwa kuwania tena nafasi hiyo, huku Chadema wakitumia kete hiyo kumnadi Mwalimu.

 “Nyalandu (Lazaro-aliyekuwa mbunge Singida Kaskazini) na Godwin Mollel (Siha) nao walihama vyama vyao lakini mimi ndiye nazungumzwa sana na kusema kila chama kimepoteza mbunge wake lakini kuna chama kimeumia kuliko vingine,” amesema na Mtulia.

Amesema, “Wakati nikiwa upinzani sikuwa na namba ya Rais, sasa ninayo mkiwa na matatizo mnaniambia mimi nampigia na mambo yanatekelezwa. Kama kawaida yake yuko kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ubaguzi.”

Kama ilivyo kwa Mtulia, Dk Mollel naye alikuwa mbunge wa Chadema jimbo la Siha lakini Desemba 14,2017 alihamia CCM na kupitishwa kuwania ubunge huku Nyalandu ambaye alikuwa mbunge kwa tiketi ya CCM, alihamia Chadema.

Akizungumza katika kampeni hizo Mtulia amesema, “Nitakuwa mbunge wa chama dola na ninakwenda kutekeleza ilani ya uchaguzi, mtu yeyote asijaribu kuzuia ilani hii kutekelezwa. Naomba kila mmoja awe mwakilishi wangu wa kuniombea kura. Ukichagua Mtulia umechagua maendeleo.”

Akiomba kura, Mwalimu alisema, “Naahidi kwenda kuwa mbunge wa kuwatumikia wananchi wote si Chadema tu. Siendi kuwa mbunge mnafiki, nitatumia talanta zote na ninaahidi makazi bora Kinondoni, kuna changamoto ya mafuriko.”

Mwalimu amesema, “Naahidi  tutatenga fedha kuondoa mafuriko. Kuna tatizo kubwa la afya, tuna kata nne tu zenye zahanati na kituo kimoja cha afya. Napaswa kusimamia afya. Naenda kusimamia, hakuna bodaboda wala mama ntilie atakayenyanyaswa.”

Sh 1.1 Tirilioni zatolewa kusaidia mapambano dhidi ya Malaria


Shirika la Global Fund limetoa ufadhili wa dola za Marekani 525 milioni sawa na Sh1.1 trilioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi kati ya mwaka 2018 na 2020.

Kati ya fedha hizo, Sh67 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kifua kikuu zikihusisha elimu kwa wanajamii, vipimo na dawa  kwa watu ambao watabainika kuwa na ugonjwa huo.

Hatua hiyo inalenga kufikia dhamira ya Serikali ya kuwapa matibabu asilimia 70 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2020.

Kuhusu malaria Sh320 bilioni zimetengwa kwa ununuzi wa vyandarua, vipimo (mRDTs) na dawa za kutibu ugonjwa huo.

Kwa mapambano dhidi ya Ukimwi zimetengwa Sh769 bilioni kiasi ambacho Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekitaja kuwa ni kikubwa kuwahi kutolewa na shirika hilo kwa ugonjwa huo.

Akizungumza leo Jumatatu Januari 29,2018 wakati wa utiaji saini makubaliano ya ufadhili huo, Ummy amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na wadau wa masuala ya afya.

Waziri Ummy amemhakikishia mwakilishi wa shirika hilo kuwa, Serikali itaongeza usimamizi katika fedha zinazotolewa na wafadhili kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Rais mwenyewe ameniambia kuwa fedha hizi ni nyingi, hivyo tufanye kila linalowezekana kuhakikisha zinatumika kama ilivyoelekezwa, nami naahidi nitazifuatilia kuona zinafanya kazi iliyopangwa,” amesema.

Mwakilishi wa Global Fund nchini, Linden Morris amesema shirika hilo litaendelea kusaidia mapambano dhidi ya maradhi hayo.

Morris amesisitiza wasimamizi wa fedha hizo kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa.
 

Pep Guardiola azidisha sifa EPL, sasa kumnasa Laporte


Mlinzi wa Athletico Bilbao, Aymeric Laporte akikabiliana ba Staa wa Barcelona Lionel Messi

Hizi sasa sifa! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya klabu ya Manchester City kufikia makubaliano na klabu ya Athletic Bilbao kulipa kiasi cha £57m  takribani shilingi bilioni 158 kwaajili ya kukamilisha usajili wa mlinzi wa kati wa klabu hiyo Aymeric Laporte.

Kiasi hicho ambacho Man City inakilipa kwa Bilbao ni kwa ajili ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo (Buy Out Clause) na Pep Guardiola ameonekana kuhitaji huduma ya beki huyo ili kuimarisha safu yake ya ulinzi.

Ripoti nchini England zinasema kuwa Laporte raia wa Ufaransa mwenye miaka 23 huenda kesho akakamilisha vipimo na kusaini mkataba na vinara hao wa ligi kuu soka nchini humo.

Endapo Laporte atatua ndani ya Man City atakuwa ndiye mchezaji ghali zaidi akivunja rekodi ya usajili ya klabu hiyo inayoshikiliwa na kiungo Kevin de Bruyne ambaye alisajiliwa kwa dau la £55m mwaka 2015 akitokea VfL Wolfsburg ya Ujerumani.

Laporte huenda akaungana na walinzi wengine ghali duniani ambao ni John Stones na Kyle Walker waliosajiliwa ndani ya uongozi wa Pep Guardiola.


Baada ya vichapo Mbao FC kujiuliza kwa Kariakoo ya Lindi


Baada ya kuchezea vichapo viwili mfululizo katika Ligi Kuu kwa Mbao FC, sasa imepanga kufanya kweli katika mchezo wao wa kombe la FA dhidi ya Kariakoo Lindi utakaopigwa Jumatano hii.

Wababe hao wa vigogo wa Ligi Kuu Simba na Yanga, walichezea vipondo mechi zao mbili bila majibu,ambapo walianza kulizwa na Stand United bao 1-0 wakiwa nyumbani, kisha kuchapwa tena na Ruvu Shooting mabao 2-0 ugenini.

Nahodha kikosi hicho,Yusuph Ndikumana alisema wanawafuata Kariakoo kwa lengo moja tu kusaka ushindi ili kusonga mbele kwenye mashindano hayo.

Alisema makosa waliyoyafanya katika mechi zao za Ligi Kuu hawatarajii yajirudie na kwamba wanahitaji kutwaa ubingwa huo ambao waliukosa msimu uliopita.

“Tunaenda kwa lengo moja la kusaka ushindi ili kusonga mbele,ni mchezo mgumu na muhimu sana kwetu,makosa tuliyoyafanya hatutarajii kuyarudia kwenye FA”alisema Ndikumana.

Beki huyo aliongeza kuwa Kariakoo hawaijui kiundani, hivyo watakuwa makini kuzuia aina yoyote ya mashambulizi langoni mwao kuhakikisha hawapiti kirahisi ili kufikia malengo yao.

“Hatuwajui Kariakoo, kwahiyo tutakuwa na tahadhari sana nao kuwakabili, tunalenga sana kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa msimu uliopita”alisema nahodha huyo Mrundi.

Mbao ilifanikiwa kufika fainali ya mashindano hayo katika msimu uliopita na kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba, ambayo tayari imeshayaaga mashindano hayo.


Wakazi Wa Dar Wamiminika Ofisi za Mkuu Wa Mkoa Kujua Hatima Yao


Zaidi ya Wananchi  elfu tatu leo wamejitokeza ikiwa ni Siku ya kwanza ya Utatuzi wa Malalamiko ya Kisheria kwa Wananchi waliodhulumiwa chini ya Wanasheria Magwiji 160 ikiwa ni Mkakati wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kusaidia wanyonge waliodhulumiwa Mali zao kupata haki pasipo kuvunja sheria.

Wananchi hao wametaabika kwa muda mrefu baada ya kudhulumiwa Mali zao Walizochuma kwa Tabu na sasa kupitia huduma ya Masada wa kisheria uliotangazwa na RC Makonda wanaamni watarejeshewa haki yao.
Makonda amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza leo inatoa picha kamili Kuwa wapo viongozi wasiotekeleza vyema majukumu yao ya kiofisi kwenye idara zao ambapo ameahidi kuwawajibisha.

Aidha  Makonda amesema kilichomgusa kuandaa Wiki ya msaada wa kisheria ni baada kubaini uwepo wa wananchi wanaonyanyasiki na hata kufikia hatua ya kufa kwa presha au kupooza miili baada ya kudhulumiwa na watu wenye pesa au wanaotumia uelewa wa sheria kukandamiza wanyonge.

Kutokana na idadi kuwa kubwa wanaoendelea kujitokeza Makonda anaongeza wanasheria wengi zaidi ili kuhakikisha Kila anaefika na kupata namba anahudumiwa ipasavyo ambapo amewaomba wanasheria kuhakikisha wanawasikiliza wananchi kwa umakini na kuchambua nyaraka kwa ufasaha na wasitoe hukumu.

Makonda amesema katika zoezi hili limehusisha Wanasheria wabobezi, Wataalamu wa kutambua nyaraka zilizogushiwa, watendaji wa Ardhi na watumishi wa Mahakama ambao wapo kwaajili ya kuwahudumia Wananchi.

Pia Makonda amesema baada ya kupokea ripoti kamili ya kesi zote atasimama kuhakikisha Hakuna mnyonge anabaki akinyanyasika.
Zoezi la kusikiliza wananchi waliodhulumiwa Mali zao ikiwemo Nyumba, Viwanja, Magari, Mirathi na Kazi litaendelea hadi siku ya Ijumaa ya February 2.

Nao wananchi waliojitokeza wamemshukuru  Makonda kwa kutambua Tabu wanazozipata baada ya kudhulumiwa na wajanja ambapo wengine wamesema wamepoteza Waume, Wake zao na wengine kupata magonjwa baada ya kudhulumiwa na wametaabika Muda mrefu kutafuta haki pasipo kufanikiwa lakini kupitia utendaji kazi makini wa  Makonda wanaamni haki inapatikana.


Saturday, 27 January 2018

Alichokisema Mr T kuhusu Darassa kuwa teja



Baada ya kimya cha muda mrefu kwa msanii Darassa ambaye mwaka juzi 2016 alitingisha sana na wimbo wake 'Muziki' kumeibuka tetesi kuwa msanii huyo naye amejiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, jambo ambalo limewashtua wengi. 

Kufuatia tetesi hizo mtangazaji wa kipindi cha Bongo fleva Top 20 ya East Africa Radio, Jr Junior alimvutia waya msanii huyo lakini bahati mbaya hakuweza kupokea simu yake jambo ambalo lilimfanya kumpigia simu mtu wake wa karibu ambaye ni producer wake Mr T Touchez ili kufahamu ukweli juu ya tuhuma au tetesi hizo. 

Baada ya Mr T Touchez kupigiwa simu alisema yeye hafahamu lolote juu ya jambo hilo na kukiri kuwa kwa sasa hajakutana na msanii huyo muda kidogo, hivyo hafahamu lolote kuhusu hicho kinachoelezwa kutumia dawa za kulevya. 


Kikosi cha Yanga VS Azam FC

                                            Kikosi cha Yanga kitakachovaana na Azam FC leo

Kabila ataja mwezi wa kufanyika uchaguzi DR Congo

Rais Joseph Kabila amepinga ukosoaji unaotekelezwa na jamii ya kimataifa kuhusu kucheleweshwa kwa uchaguzi katika jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika mkutano na wanahabari kuadhimisha miaka 17 madarakani, aliahidi kwamba uchaguzi huo utafanyika mwisho wa mwaka huu.

Kulingana na mwandishi wa BBC Alex Duval Smith mkutano huo na vyombo vya habari mjini Kinshasa ulikuwa wa kwanza katika kipindi cha miaka mitano.Na ulichukua saa tatu.

Aliikosoa Monusco akisema ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa hauko nchini DRC ili kuendesha shughuli za taifa hilo.

Katika shutuma dhidi ya muungano wa Ulaya na Marekani, ambao wamekosoa makabiliano dhidi ya waandamanaji, alisema: DRC sio koloni .Taifa hili lazima liheshimiwe.

Alionekana akilikumbusha kanisa katoliki akisema kuwa maandamano yanayofanywa na wakristo dhidi ya serikali yake yanafaa kuruhusiwa lakini waandalizi ni lazima washtakiwe.

Serikali hiyo hivi majuzi ilitangaza kwamba uchaguzi utafanyika tarehe 23 Disemba, ikiwa ni miaka miwili baada ya kukamilika kwa muda wa utawala wa rais huyo.

Kampuni ya Mugabe yaingia kwenye matatizo

Kampuni moja ya rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe inatakiwa kuondoka katika kipade kimoja cha ardhi kinachomilikiwa na shule moja la sivyo ishtakiwe.

Kampuni hiyo kwa Jina Gushungu Holdings inadaiwa kunyakuwa kipande hicho cha ardhi chenye ukubwa wa hekari 23 katika eneo moja la makaazi ya mji wa Harare.

Kanisa la Reform linasema kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na kundi la shule zake la Eaglesvale.

Wakili wa shule hiyo Rodney Makausi aliambia BBC kwamba mwaka 2016 serikali ilichukua ardhi hiyo kwa nguvu.

Serikali baadaye ikaondoa madai yake baada ya swala hilo kuwasilishwa mahakamani.

Lakini mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Enos Chomutiri anasema kuwa mahindi yalipandwa katika shamba hilo mwaka uliopita na bango kubwa la shule hiyo likaondolewa.

Mawakili wametaka kampuni hiyo kuondoka katika shamba hilo mwisho wa mwezi huu ama ishtakiwe.

Sio mara ya kwanza familia ya Mugabe imetuhumiwa kuchukua mali kwa nguvu.

Awali, familia hiyo imekuwa na mgogoro na wakulima masikini kuhusu ardhi moja inayodaiwa kuwa na utajiri wa dhahabu ,pia familia hiyo imetuhumiwa kwa kunyakua shamba moja linalalozalisha ndimu zinazouzwa nje ya taifa katika eneo hilo hilo.