Monday, 22 January 2018

Dalali ameanza ruti kuhamasisha Simba kutwaa Ubingwa


MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Mzee Hassan Dalali ‘Handsome Boy’, ameanza harakati za kuhamasisha wanachama wa timu hiyo kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo amepanga kutembelea Tanga na Zanzibar kabla ya mikoa mingine.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mzee Dalali alisema kuwa tayari ameshaanza kuzunguka katika matawi mbalimbali ya Mkoa wa Dar kwa ajili ya kuhamasisha umoja na mshikamano kwa lengo la kuweza kutwaa ubingwa wa msimu huu.

“Tayari nimeshaanza ziara yangu ya kuzunguka matawi ya nchi nzima, kwa hapa Dar nimeshakwenda kuongea na wanachama wa matawi ya Mabibo na leo (jana) nitakwenda Gongo la Mboto, lengo kubwa ni kuhamasisha umoja na mshikamano wa matawi ambao kama ulitoweka lakini sasa umeanza kuzaa matunda kutokana na ushirikiano wa viongozi wa juu wa timu, nawapongeza sana.

“Hili nimeamua kufanya mwenyewe kwa mapenzi ya timu yangu kwa sababu ni muda mrefu umoja na mshikamano umekuwa kama umepotea lakini wiki ijayo nitakwenda Tanga kisha Zanzibar, ikizingatiwa tulikuwepo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, muda mrefu umepita sasa bila ya kuchukua ubingwa lakini kwa mabadiliko chini ya viongozi wangu ambayo wanayafanya, naamini tutafanikiwa na kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Mzee Dalali.


Humphrey Polepole afunguka kuhusu UKAWA


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa hakuna kitu kinaitwa UKAWA kwani mpango huo ulianzishwa na CHADEMA ili kuvitumia vyama vingine kisiasa.

Polepole amesema kuwa kama UKAWA ingelikuwepo hadi leo basi isingetokea baadhi ya majimbo CHADEMA kushindana na CUF ile hali vyama vyote vipo chini ya muavuli wa UKAWA.

“Hakuna kitu kinaitwa UKAWA, hii ilikuwa project ya Chadema ikivitumia vyama vingine, CUF, NCCR na NLD. Kilichobaki ni UKIWA, katika jimbo lililokuwa la CUF leo CDM na CUF wanamenyana,”ameandika Humphrey Polepole kupitia Twitter.

Hata hivyo, kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kinondoni CUF kwa upande wa Prof Lipumba imesimamisha mgombea wake huku CHADEMA nao wakisimamisha mgombea wao.

Alichokisema Isha Mashauzi kuhusu mziki wa Taarabu


Msanii Isha Mashauzi maarufu kama Jike la Simba ameibuka na kusema muziki wa miondoko ya taarabu nchini hauwezi kufa kama baadhi ya watu wanavyodhani, kwa madai wao hawategemei 'kiki' katika kufanya kazi zao kama wanavyofanya wasanii wengine.

Isha amebainisha hayo wakati akitambulisha 'video' yake mpya ya wimbo 'nibembeleze' kwenye kipindi cha 'FRIDAY NIGHT LIVE' (FNL) kinachorushwa na EATV tinga namba moja kwa vijana, baada ya kuwepo minong'ono mingi kwa wapenzi na mashabiki wa nyimbo hizo wakidai huenda muziki huo umekufa, kwa maana hawasikii vijembe vya maneno wanavyopigana wasanii wenyewe kwa wenyewe kama wanavyofanya baadhi ya waimbaji wa muziki wa bongo fleva.

"Taarabu haiwezi kufa, naweza kusema ni muziki mama wa Afrika, Tanzania au hata duniani. Muziki wa taarabu ukipigwa sehemu yeyote kila mtu ataujua fika kwamba hii ni taarabu tofauti na muziki mingine kwa hiyo hauwezi kufa", alisema Isha Mashauzi.

Pamoja na hayo Isha ameendelea kwa kusema "naweza sema tu kwamba labda wanamuziki wa taarabu hawapendi zile kiki ambazo zipo kwa wanamuziki wengine, leo utasikia huyu sijui anatoka na fulani mara yule vile ndiyo mwisho wa siku aachie kazi yake mpya. Hicho kitu kwenye taarabu hamna naweza kutetea hivyo ndiyo maana wanasema hivyo"

Inasikitisha, Mashabiki Wawili wa WCB Wafariki Dunia kwa Ajali



Mashabiki hao waliopata ajali ya gari maeneo ya Chalinze wakitokea Morogoro kurudi Dar es Salaam, ni Philly Nevvo na mwingine ni Platnumz Mondi kwa majina ambayo walikuwa wanatua Instagram.

Rais wa WCB, Diamond Platnumz amesikitisha kutokea kwa ajali hiyo.

“Mbele Yenu Nyuma yetu, Siku zote tutaendela kuwakumbuka na kuthamini Mapenzi na mchango wenu Mkubwa kwa @wcb_wasafi…..Mwenyez Mungu azilaze Roho zenu mahali pema peponi….amen🙏 @philly_nevvo_msafi @,” aliandika Diamond.

Scorpion ahukumiwa miaka saba jela


Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Salum Njwete ‘Scorpion‘ miaka 7 jela kwa kosa la kumjeruhi na kumtoboa macho Said Mrisho, pia mahakama imemtaka kulipa faini ya TSH. Milioni 30 kwa ajili ya fidia kwa majeruhi huyo.

Mlalamikaji amelia akidai adhabu hiyo haitoshi. Amesema atakwenda kwa Rais Magufuli kumueleza masikitiko yake.

Kagera Sugar imejiandaa kuikwamisha Simba


Klabu ya Simba SC leo inarejea kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, sehemu ambayo ina kumbukumbu ya kukwamishwa mipango yake ya kusaka ubingwa msimu uliopita.

Kocha wa Kagera Sugar Meck Mexime, amesema timu yake imejiandaa kwa muda mrefu hivyo leo inaingia uwanjani kupambana na vinara wa ligi Simba SC huku lengo likiwa ni kusaka alama tatu.

''Hali ya hewa leo hapa Bukoba ni jua tu na hali ya uwanja ni nzuri, tumefanya maandalizi kwa muda mrefu leo tuna kazi moja tu ya kucheza mpira kwaajili ya kupata alama tatu kwasababu mpira ndio kazi yetu'', amesema Mexime.

Timu hizo zinakutana kwenye mchezo wa raundi ya 14 ambapo Simba wanahitaji alama tatu ili kuweza kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi. Simba kwa sasa ina alama 29 nyuma ya Azam FC yenye alama 30.

Msimu uliopita Simba ikiwa inaelekea kwenye hatua za mwiosho za kusaka ubingwa ilitibuliwa mipango na Kagera Sugar April 2, 2017 ilipokubali  kipigo cha mabao 2-1 hivyo kuiacha Yanga katika mazingira mazuri ambayo mwisho wa ligi waliibuka mabingwa.

Magogo yaliyokosa mmiliki bandarini kuuzwa wakati wowote kuanzia sasa



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema magogo 938 yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yatauzwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukosa wamiliki wa mzigo huo.

Maamuzi hayo yamekuja  baada ya Waziri Kigwangalla mwezi uliopita kufanya ziara ya kushitukiza bandarini hapo baada ya kupata taarifa kuwa kuna shehena hiyo ya magogo ambayo umiliki wake ulikuwa na utata.

Mhe. Kigwangalla alieleza kuwa magogo hayo yamekuwa bandarini kwa miaka 10 huku mengine yakiwa kwenye makontena 55 .

Kutokana na utata huo, Kigwangalla alitoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 kujitokeza wakiwa na nyaraka zote ili kuthibitisha kama kweli yalivunwa Zambia kama ilivyodaiwa au laah!.

“Kulikuwa na vikao mbalimbali ndani ya serikali kujadili suala hilo, na tumekubaliana kuyauza baada ya wahusika kutojitokeza kuthibitisha umiliki wake,” amesema Waziri Kigwangalla.

Waziri Kingwangalla amesema jukumu la kuyauza magogo hayo wamepewa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wanaoruhusiwa kisheria kufanya kazi hiyo, ambapo watashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS).

Kauli ya Salum Mwalimu kuhusu wanaodai kuwa sio mkazi wa Kinondoni


Mgombea ubunge wa Kinondoni kupitia Chadema, Salum Mwalimu amwajibu baadhi ya watu wanaodai kuwa yeye si mkazi wa wilaya ya Kinondoni, hivyo hana sifa za kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Akizungumza leo Januari 22, 2018 katika mahojiano na kituo cha tevisheni cha Azam, Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Zanzibar amesema ni mkazi wa wilaya hiyo na anajua matatizo ya wananchi wake.

 “Nilianza maisha Kinondoni baada ya kumaliza chuo. Nimeishi kwa miaka 14 na niko Kinondoni kwa miaka zaidi ya 30. Kwa nini Kinondoni? Si kwamba fursa zimejitosheleza lakini ninaifahamu na ninayajua matatizo ya Kinondoni kuhusu barabara, afya na elimu.”

Amesema alipomaliza Chuo Kikuu mwaka 2008 aliishi mtaa wa Togo kisha  akahamia Hananasif, kufafanua kwamba madai kwamba si mkazi wa Kinondoni hazina ukweli wowote.

Kuhusu suala la kugombea ubunge akiwa na wadhifa Chadema amesema, “Ninachotafuta ni uwakilishi wa wananchi, kwa sasa ni mwakilishi ndani ya chama. Hata  CCM kuna wenye vyeo viwili. Tunatafuta mwakilishi madhubuti ndani ya Bunge na katika chama chetu hakuna changamoto ya kofia moja au mbili.”

“Kama ni kofia mbili au moja mbona kuna mawaziri ambao ni wabunge, ili uwe  mbunge ni lazima uwe raia wa Tanzania,  lakini mbona Rais John Magufuli ni mwenyekiti wa CCM, mbona Rais wa Zanzibar ni makamu mwenyekiti wa CCM, kwa hiyo hilo la vyeo halitupi shida.”

Amesema yeye kiuhalisia ni mzaliwa wa Kikwajuni Zanzibar huku akigusia kwa kifupi kwamba anaungwa mkono na CUF.


AT: Tuzo zangu za Marekani siwezi kuzipasua


Msanii wa muziki Bongo, AT amesema hawezi kuzipasua tuzo zake alizoshinda nchini Marekani November mwaka jana, 2017.

Muimbaji huyo katika mahojiano na kipindi cha Leo Tena cha Clouds Fm amesema awali alipanga kupasua tuzo zake za Kilimanjaro Music Award (KTMA) zilizokuwa zikitolewa hapa nchini lakini baadaye akagundua kuwa tuzo hizo ni mali ya Baraza la Sanaa Taifa (BASATA).

“Ni baada ya kuomba msaada ili nisaidiwe kwenda Kongo nikafanye kolabo na Koffi Olomide, wakanizungusha sana, ilikuwa hasira tu, ila hizi tuzo zangu za Marekani siwezi kuzipasua,” amesema AT.

November mwaka jana AT alishinda tuzo mbili katika ‘B&K Music & Video Music Awards’, vipengele alivyoshinda ni International Artist na Best Music Video kupitia wimbo wake ‘Sili Feel’.

Kingozi CCM awataka Wananchi Kuwaombea JWTZ Waliopo Kongo


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewasihi wananchi wa Tanzania   kuendelea kuwaombea Dua na visomo mbali mbali Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanaouawa  wakilinda Amani katika nchini mbali mbali ikiwemo DRC Kongo.

Pia ameliomba Jeshi hilo pamoja na familia za ndugu wa marehemu Askari 10 waliofariki waliofariki siku za hivi karibuni wakilinda Amani Kongo, kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Wito huo ameutoa leo mara baada ya kumalizika shughuli ya kisomo cha Khitma na Dua ya pamoja ya Arubaini ya kuwaombea marehemu hao iliyoandaliwa na Kamati ya Amani Kitaifa Zanzibar huko katika Msikiti wa Noor Muhammad (SAW) kwa Mchina Mwanzo Zanzibar.

Dk.Mabodi ameeleza kwamba Askari hao watakumbukwa daima kwa mchango wao wa kutetea na kulinda maisha ya Waafrika katika Nchi ya Kongo ambapo walikuwa wakiiwakikisha Tanzania kupitia Jeshi la Pamoja la Umoja wa Mataifa lililopo nchini humo kwa ajili ya kulinda Amani.

Aliwambia wananchi kuwa Mashujaa hao hakuna cha kuwalipa kwa sasa kwani wamepoteza uhai wao kutokana na uzalendo uliotukuka hivyo kilichobaki ni kuwaombea Dua wao Mwenyezi Mungu awapumzishe pahala pema peponi Amini na kuziombea familia zao ziendelee kuwa na subra.

Amefafanua kuwa msiba huo mzito ni sehemu ya Askari wa Majeshi mbali mbali ya Ulinzi na Usalama nchini wanaoendelea na kazi zao za kawaida wawe imara Kifkra na Kimwili bila kukata tamaa ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Kituo kikuu cha Amani Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

Akizungumzia matunda ya kulinda misingi ya Amani nchini Dk.Mabodi amesema ni kuwepo kwa maendeleo katika Nyanja mbali mbali za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.

“Wananchi tulinde tunu ya Amani na Utulivu tuliokuwa nao katika Taifa letu, ili tuweze kuwa Mabalozi wazuri wa kulinda Amani kwa nchi jirani na Mataifa mengine.”, amesisitiza.

“Nawapongeza Kamati ya Amani ya Taifa Zanzibar kwa maandalizi yao mazuri ya kuandaa shughuli ya kuwaombea Dua kubwa kama hii vijana wetu waliouwawa na watu wanaosadikiwa kuwa Waasi huko Nchini Kongo.”, amesema Dk.Mabodi.

Aidha ameeleza kuwa wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuenzi Amani na Utulivu, uliopo nchini kwa lengo la kuepuka machafuko na migogoro isiyokuwa ya lazima nchini.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Hussein Mwinyi, amewashukru wananchi mbali mbali waliojitokeza katika Khitma hiyo kwa lengo la kuwaombea Dua Marehemu Askari hao.

Amesema licha ya Tanzania kuwapoteza Mashujaa hao bado Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) litaendelea kuwa imara na kulinda mipaka na kushiriki harakati mbali mbali za kulinda amani hata nje ya Tanzani kwa lengo la kudumisha mahusiano mema na nchi nyingine Duniani

Baada ya kuona picha ya mtoto akiomba jezi yake, Samatta afunguka


 Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars anayecheza soka la kulipwa katika club ya KRC Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta licha ya kuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili lakini ameonesha kuzidi kupendwa na mashabiki wa club yake.

Moja kati ya ujumbe unaosambaa kwa sasa katika mitandao ya kijamii ni pamoja na post ya bango ya shabiki mtoto wa KRC Genk ikiwa imeandikwa “Mbwana Can I have Your Shirt Pendeza” akiwa kamaanisha “Mbwana unaweza kunipa jezi yako? Pendeza”

Baada ya Mbwana Samatta kuona post ya picha ya mtoto huyo akajibu “Ndio naweza kukupa kwa nini ishindikane” hiyo imezidi kudhihirisha mapenzi ya dhati ya mashabiki kwa Mbwana Samatta maana sio kila mchezaji soka huwa anapata nafasi ya kupendwa na mashabiki kwa kiwango hicho.

Wenger atakuwepo George Weah akiapishwa?


Wananchi wa Liberia wanasubiria kwa hamu tukio la kuapishwa kwa Rais mteule George  Weah, ambapo wengi wamekesha katika uwanja wa mpira wa taifa hilo, mahali ambapo leo January 22, 2018 anategemea kuapishwa na kuandika historia mpya kutoka kung’aa kwenye soka hadi kuwa Rais

George Weah, maisha yake ya utoto, yalikuwa katika mazingira duni katika mji mkuu wa Liberia Monrovia, alipata mafanikio makubwa katika  soka na kufanikiwa kuchezea timu kadhaa barani Ulaya ikiwemo Chelsea, Monaco na AC milan.

Ni Muafrika pekee kuwahi kushinda tuzo mchezaji bora wa FIFA na tuzo ya Ballon. Weah aliingia katika siasa baada ya kustaafu soka mwaka 2002 na akawa miongoni mwa Maseneter katika bunge la Liberia.

Aligombea urais mwaka 2005 na alimshinda Johnson Sirleaf wakati wa duru ya kwanza katika uchaguzi huo lakini akashindwa katika duru ya pili ambapo kambi yake ilisusia kushiriki.

Aliyewahi kuwa meneja wa George Weah katika klabu ya Monaco ya ligi kuu ya Ufaransa Arsene Wenger amealikwa na atakuwepo katika tukio la kuapishwa.

Wazazi wanashikiliwa na Polisi kwa kupokea mahali ya Ng'ombe saba


JESHI la Polisi mkoani Geita linawashikilia watu  wawili wakazi wa  Kijiji cha Kasubuya  wilayani Nyang’wale kwa kula njama wakiwa wazazi  kupokea mahari ya ng’ombe saba na kumwozesha  mwanafunzi wa  kidato cha pili.

Binti huyo  aliyekuwa anasoma katika shule ya sekondari Nyijundu, sasa ana ujauzito.

Aliyethibitisha kukamatwa kwa wazazi hao wa pande zote mbili ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson na kuwataja ni baba mzazi wa msichana huyo, Herman Makanika (48) na Maximillian Makila ambaye ni baba mzazi wa mtuhumiwa aliyemuoa mwanafunzi huyo.

Ingawa hakulitaja jina la mtuhumiwa, Kamanda Mpojoli alimpongeza mwalimu wa shule ya sekondari aliyetoa taarifa  za kuwapo kwa tukio hilo na akabainisha  jinsi wazazi wa pande zote mbili walivyoshiriki  kutenda kosa licha ya mtuhumiwa kutoroka.

Alisema wazazi wa pande zote mbili wanahusika ingawa mtuhumiwa (muoaji) anaendelea kusakwa, hivyo wanapaswa kuwajibika kutokana na kufanya makubaliano kwa kutoa mahari ya ng’ombe saba na mzazi wa msichana kuwapokea ng’ombe hao kama mahari.

Aliongeza kuwa baada ya polisi kuarifiwa ilichukua hatua za haraka na watuhumiwa kukamawta na hadi jana walikuwa wanaendelea kushikiliwa huku juhudi za kumsaka mtuhumiwa zikiendelea kuhakikisha anapatikana na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.