Saturday, 25 November 2017

RC Aggrey Mwanri aamua kuwapa fursa hii vijana




Vijana Mkoani Tabora wametakiwa kuacha tabia ya kukaa vijiweni na kusikiliza maneno ambayo hayawasaidii wala kuwafundisha namna ya kupata maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri katika maeneo mbalimbali ya Kata za Wilaya ya Kaliua kwenye zoezi la uhamasishaji wa kilimo cha kisasa cha zao la Pamba na mazao mengine.

Aidha mkuu huyo wa mkoa amewataka vijana kutumia muda wao kujiajiri katika sekata ya kilimo na uzalishaji wa pamba pamoja na mazao mengine yatakayowasaidia kujipatia kipato na kuinua maisha yao.

“Kijana uliyekuja hapa leo ninakuambia kuwa kama unarafiki yako unashinda nae kijiweni na kucheza karata, Pool kuanzia leo achana naye, kwani hana nia njema nawewe, mwambie kuwa mkuu wa mkoa amenifundisha juu ya kulima pamba kisasa kuanzia sasa urafiki wangu mimi na wewe bye bye”, amesema RC Mwanri.

Mkuu wa Tabora yuko katika ziara mkoani mwake kuhamasisha kilimo cha kisasa cha zao la pamba na mazao mengine ambayo yatawasaidia wakulima kupata pesa zitakazoboresha maisha yao.

Lema amueleza Mrisho Gambo maneno haya



Mbunge wa Arusha Mjini, Mh. Godbless Lema amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kutojaribu kufanya hila zozote za kuisababishia CCM ipate ushindi kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika hapo kesho, Nov 26.

Lema amesema kwmba anafahamu kila hatua na vikao ambavyo Mkuu huyo wa Mkoa na kwamba ana ushahidi wa kutosha wa kila kitu kunachopangwa.

"Mrisho Gambo,unapaswa kujua kwamba huna mamlaka wala  uwezo wa kushinda huu uchaguzi kwa nguvu/hila, hakuna kikao umekaa ambacho sina taarifa zake na ushahidi wa kila kitu".  Lema
Aidha Lema ameongeza kwa kumkanya kiongozi huyo asijaribu kufanya hivyo.

"Unataka kushinda uchaguzi huu kwa gharama yoyete ile ?sababu polisi wako nyuma yako ? usijaribu" Lema ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter asubuhi ya leo
Kesho kata 43 zinatarajiwa kufanya uchaguzi wa marudio wa kuwapata madiwani.

Waziri Kigwangalla awajibu wanaosema vyuma vimekaza



Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Hamisi Kigwangalla amesema maisha yataendelea kuwa magumu kwa watu wasio na shughuli maalum ambao wamezoea kuishi kwa ujanja ujanja.

Ameyasema hayo wakai akijibu maswali ya wananchi kupitia mtandao wa ‘Twitter’ ambao wengi walitaka kujua kuhusu utendaji kazi wake na hali halisi ya maisha yalivyo wakidai kuwa ni magumu.

“Wanaofanya shughuli zao halali hawatoona vyuma vimekaza, badala yake watafurahia sema watoto wa mjini, wasanii sanii na wajanja wajanja ndiyo watapata shida! Hawa wajanja wajanja ni wangapi? Na wenye shughuli halali ni wangapi?”, alisema Kigwangalla akiacha maswali kwa mmoja wa watu waliomuuliza.

Waziri Kigwangalla aliendelea kwa kutoa ufafanuzi juu ya namna ya kujenga uchumi kupitia kufanya kazi na sio kutegemea kupata pesa kwa njia rahisi rahisi.

“Mfumo wa uchumi unataka watu tufanye kazi kwa ubunifu ndipo tupate maisha mazuri siyo kufanya usanii kidogo tayari ukatajirika! Kukaza vyuma maana yake kuziba mianya ya wasanii ili walio kwenye uchumi halisi na wasanii wawe sawa siyo kuonea watu!” alimaliza.

Waziri Kigwangalla hivi sasa yupo jimboni kwake Nzega vijijini akiwa amepiga kambi kwaajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Nata.

Bwana harusi afariki, mkewe ajeruhiwa katika ajali wakitoka kufunga ndoa



Watu 12 wamekufa na wengine 22 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kijiji cha Ighuka wilayani Ikungi kwenye Barabara Kuu ya Singida – Manyoni baada ya Toyota Hiace waliyokuwa wakisafiria kutoka kumchukua bibi harusi kugongana uso kwa uso na Toyota Noah iliyokuwa imepakia watu kutoka msibani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku kwa kulihusisha gari lenye namba za usajili T 581 BBV iliyokuwa ikitokea Singida kwenda Manyoni na T 423 CFF iliyokuwa ikitokea Manyoni kwenda Singida.

Alisema kuwa ingawa uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo bado unaendelea, taarifa za awali zinaonesha kuwa sababu kuu ni mwendo kasi na uzembe wa madereva.

“Baadhi ya majeruhi walituambia dereva wa Toyota Hiace aliyekuwa anatoka Singida mjini alihama kutoka upande wake na kwenda upande wa pili wa barabara ambako aligongana uso kwa uso na Noah iliyokuwa imebeba watu waliokuwa wakitoka msibani na kusababisha vifo vya abiria 10 hapo hapo na majeruhi 24,” alisema.

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Ng’hungu Kusenza alisema kuwa majeruhi wawili waliofikishwa Hospitali ya Misheni Puma kwa ajili ya matibabu pia walikufa hivyo kufanya idadi ya watu waliokufa kuwa 12.

Aliwataja waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya mkoa kuwa ni John Duma, Jasson Nsunza, Abubakar Omari, Mary Kinku, Mwanaidi Juma na Husna Juma, Wengine ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Misheni Puma wilayani Ikungi ni Ezekiel Joseph, Mussa Daniel, Namtaki Daniel, Hamis Omari, Jumanne Mganga na Wansola Shalua. Habari ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa Bwanaharusi na madereva wa magari yote mawili ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Chanzo: Habarileo

Mbeya City yafanya mabadiliko haya



Klabu ya soka ya Mbeya City imelazimika kubadili jezi yake iliyokuwa imepanga kuitumia kwenye mechi ya ugenini leo dhidi ya Singida United.

Mbeya City imefikia uamzi huo baada ya kuwepo kwa mfanano kati ya jezi yake ya Singida United ambao ni wenyeji wao katika mchezo wa leo.

Jezi hizo ni kama zinavyoonekana hapo chini ambapo kushoto ni jezi ya wenyeji Singida United na kulia ni jezi ya Mbeya City iliyokuwa imepangwa kutumika leo.



Hata hivyo bado Mbeya City hawajasema ni jezi gani ambayo watatumia lakini msimu huu jezi zao za pili kwaajili ya mechi za ugenini ni zile zenye rangi ya damu ya mzee hivyo huenda ndio zitakazotumika leo.

Singida United inayoshika nafasi ya 5 ikiwa na alama 17 inacheza leo na Mbeya City yenye alama 11 katika nafasi ya 10 kwenye mchezo wa raundi ya 11, uwanja wa Namfua mjini Sungida.

Kocha wa Simba awaambia wachezaji wake kutowadharau Lipuli katika mechi yao Kesho



KOCHA wa Simba, Joseph Omog amewataka wachezaji wake kutowadharau wapinzani wao wa kesho timu ya Lipuli ya Iringa na kuwataka kuwa makini kwa dakika zote 90.

Akizungumza kabla ya kuanza mazoezi ya jana kwenye uwanja wa chuo cha Polisi Kurasini, Omog, alisema kuwa hawatakiwi kuwabeza wapinzani wao hao kwa kuwa mpira ni mchezo wa makosa.

“Hakuna timu ndogo kwenye ligi, wachezaji nimekuwa nikiwaambia hivyo, lazima nidhamu ya mchezo ifuatwe, kama wachezaji watafuata maelekezo tuna nafasi nzuri ya kushinda,” alisema Omog.

Alisema kuwa kwenye mazoezi ya timu hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Sportpesa, amekuwa akikazania wachezaji wake kucheza soka la kasi na kuhakikisha wanatumia vyema nafasi wanazozipata.

“Kwanza naangalia zaidi ushindi kabla ya kutazama wingi wa mabao, kama tutatengeneza nafasi nyingi na kuzitumia vizuri tunaweza kupata ushindi wa mabao mengi,” aliongeza kusema Omog.

Alisema kuwa licha ya ugeni wa Lipuli kwenye ligi, anaamini nao wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mchezo huo wa kesho utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

“Walipata pointi moja walipokuja hapa kucheza na Yanga.., kwa hiyo si timu ya kubeza, tutapambana kwa ajili ya pointi tatu,” aliongezea kusema Omog.

Simba ipo kileleni kwa msimao wa ligi ikiwa na pointi 22 sawa na Azam FC wanaoshika nafasiya pili lakini wekundu hao wa msimbazi wana magoli mengi.

Faiza Ally amuonyesha mpenzi wake mambo mapya


Muigizaji wa Filamu Bongo, Faiza Ally ameamua kumuweka wazi mpenzi wake mpya baada ya kuachana na Mr. Sugu aliyebahatika kupata naye mtoto mmoja aitwaye Sasha.

Mrembo huyo ametumia fursa ya mtandao wa kijamii wa Instagram kuweka picha akiwa na mwanaume huyo anayehisiwa  kuwa  baba mzazi wa mtoto wake wa pili wa kiume aliyempata miezi kadhaa iliyopita, picha hiyo imewaonyesha wawili hao wakiwa wanapigana busu zito.





Rais Magufuli ampongeza kikwete



Rais wa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa sifa na pongezi kwa rais mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kufanikisha ujenzi wa hospitali ya Mloganzila.

Rais ametoa pongezi hizo leo wakati akihotubia wananchi waliohudhuria ufunguzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila jijini Dar es salaam.

“Wakati ujenzi wa Hospitali hii unaanza mimi nilikuwa naagizwa tu na niliambiwa nikatafute eneo kubwa nikawaza nitalitoa wapi lakini baadae mzee Jakaya akanipigia tena simu  akaniambia kuna eneo huko Mloganzila ni la serikali nenda kaangalie na ujenzi uanze haraka, ndio nikaja hapa”, amesema Rais Magufuli.

Rais magufuli ameongeza kuwa “Watu tunapenda sifa lakini hizi sifa sio zangu ni za rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwani mimi nilikuwa naagizwa tu nikiwa waziri wa Ujenzi, ndio maana nimeona niseme wazi kuwa sifa zote zimwendee mzee Kikwete”.

Aidha rais Magufuli ameweka wazi kuwa wakati anakwenda kuona eneo la Mloganzila wala hakukuwa na barabara lakini aliambiwa na rais Kikwete aanze ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara haraka iwezekanvyo na alifanya hivyo sambamba na waziri wa maji amnbaye naye aliagizwa kuanza ujenzi wa miundombinu ya maji.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila jijini Dar es salaam ni mpango na jitihada za rais wa awamu ya nne.




Hiki ndio kikosi cha Yanga dhidi ya Tanzania Prisons leo



Yanga wanaokwenda Chamazi kuwava Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, leo, hawa hapa..

1. Youthe Rostand
2. Juma Abdul
3. Gadiel Michael
4. Andrew Vincent
5. Nadir Haroub
6. Pato Ngonyani
7. Pius Buswita
8. Raphael Daud
9. Obrey Chirwa
10. Ibrahim Ajibu
11. Emmanuel Martin

AKIBA:
 Beno Kakolanya
Hassan Kessy
Maka Edward
Yusuph Mhilu
Said Mussa
Geofrey Mwashiuya

Mali: Maafisa 4 wa UN wauawa



Umoja wa Mataifa umesema maafisa wake wanne walinda amani pamoja na mwanajeshi mmoja wameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa eneo la mpakani baina ya Mali na Niger.

Afisa mkuu anayekiongoza kikosi hicho cha walinda amani walioko Mali bw. Mahamat Saleh Annadif, bila kutaja washambulizi ni akina nani, amelaani vikali tukio hilo akisema ametamaushwa na kisa hicho dhidi ya maafisa wake ambao walikuwa wakiendeleza kazi ya udumishwaji wa amani na vilevile kutoa misaada hasa ya kimatibabu kwa wakaazi wa maeneo ambayo yamekumbwa na hali mbaya ya kuzorota kwa usalama.

Kuna makundi kadhaa ya wapiganaji yanayopatikana eneo hilo la Mali, yaliyo na uhusiano na kundi la Al Qaeda.

Umoja wa mataifa umekuwa na kikosi cha walinda amani huko Mali tangu 2013 wakisaidiwa pia na kikosi cha kijeshi cha Ufaransa.

Mbowe afunguka kuhusu kampeni za udiwani



Moshi. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wamewazidi CCM kimkakati katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika kesho  katika kata 43 nchini.

Mbowe amesema chama tawala hakina mpango mkakati wa kufahamu mambo gani wananchi wanataka na shida gani zinawakabili zaidi ya kuzungumzia kwa jumla na kujinasibu kufanya mambo makubwa ikiwamo kujenga barabara, kununua ndege na kupambana na mafisadi.

Amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa ndiyo maana katika kampeni za kuwanadi wagombea wa uchaguzi huo alinadi ajenda tatu ambazo ni dhana ya uhuru, maendeleo na demokrasia.

Mbowe amesema maendeleo hayapimwi kwa kununua magari, kujenga viwanja vya ndege, kupambana na mafisadi bali yanapimwa kwa maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

"Tunaaminishwa uchumi unakuwa kwa sababu nchi imenunua ndege, inapambana na mafisadi na inajenga viwanja vya ndege, hayo ni mambo mazuri hakuna anayepinga, lakini je, mwananchi wa kawaida ananufaika vipi," amesema Mbowe.

Amesema hali ya maisha ni ngumu, hivyo Serikali isijifungie na isizibe masikio kusikia wanacholalamika wananchi.

"Wananchi wana hali ngumu, sisi tuliozunguka na kuzungumza nao tunajua, biashara zinafungwa, wananchi masikini hali zao zimezidi kuwa ngumu, watumishi hawajapandishiwa mishahara hivyo hali kuzidi kuwa duni kwa wanaotegemea kuchuuza bidhaa kwa sababu hakuna anayemudu kununua," amesema Mbowe.

Amesema amani ya kudumu na demokrasia haiwezi kuwepo kama hakuna nafasi ya vyama vya siasa kufanya kazi zake bila kuonekana kama wahalifu.

Mbowe amesema wananchi wana kiu na shauku ya kuhudumia mikutano ya kisiasa.

Mwananchi:

Zitto Kabwe asema kinachotakiwa ni mabadiliko ya maendeleo kabla ya 2020


 

Mtwara. Kiongozi wa Chama wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kitendo cha kuchukua watu kutoka vyama vya upinzani siyo mafanikio bali kinachotakiwa ni kuwaletea wananchi mabadiliko ya maendeleo kabla ya mwaka 2020.

Zitto alisema hayo juzi katika mkutano wa kampeni za udiwani Kata ya Reli mjini Mtwara.

“CCM kazi yao sasa hivi ni kuchukua watu kutoka vyama vya upinzani, wanaona ni mafanikio wakisajili dirisha dogo. Huu mtaa wenu si ulikuwa hivi tangu mwaka 2015 kuna mabadiliko yoyote?

“Itakapofika mwaka 2020 mtaangalia wamechukua watu wangapi kutoka upinzani au mtaangalia mabadiliko kwenye mtaa wenu?” Alihoji Zitto.

Pia, alisema ameshangaa kuona foleni ya watu waliojipanga kwenye meli ya Wachina inayotoa huduma za afya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma akidai hiyo ni dalili ya kuonyesha kuna tatizo.

Aliendelea kusema kuwa maendeleo si idadi ya madaraja, bandari na barabara za juu zilizojengwa bali ni afya, elimu na uwezo wa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi.

Zitto alisema kwa sasa Tanzania inajenga reli lakini inachukua vyuma kutoka Uturuki ikiwa ni pamoja na kampuni ya kuponda kokoto kwa ajili ya ujenzi wa reli.

“Nchi ya aina gani, kuna haja gani ya huu uhuru ambao tunao mpaka sasa? CCM inaamini ninyi nyote mtawapa kura,” alisema.

Mgombea wa udiwani wa kata hiyo, Mwajuma Hassan alisema kwamba vipaumbele vyake ni kuhakikisha kila mkazi wa kata hiyo anajiajiri.

Pia, mgombea huyo aliahidi kusimamia huduma za kijamii kama afya, maji na elimu.

Mwananchi: