Saturday, 25 November 2017

Rais Magufuli aeleza sababu ya kuliacha jengo la Tanesco akiwa waziri



Dar es salaam. Rais John Magufuli amesema hakubomoa jengo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopo Ubungo alipokuwa waziri wa ujenzi kwa kuwa aliogopa kufukuzwa kazi.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumamosi Novemba 25,2017 alipozindua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), kampasi ya Mloganzila.

Akizungumza mbele ya waziri mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda aliyehudhuria uzinduzi huo, Magufuli amesema wakati huo aliogopa baada ya kuzuiwa na waziri mkuu huyo, lakini sasa yeye ndiye Rais hakuna wa kumzuia.

Akizungumzia ubomoaji unaoendelea sasa amesema, “Nilishatoa maagizo, najua Mizengo Pinda kwenye hili alinipinga wakati ule, lakini najua leo hawezi akanipinga kwa sababu mimi ndiye Rais. Wakati ule nilikuwa waziri wake, ndiyo maana nilinyamaza nilijua ninaweza nikafukuzwa, hutakiwi kumpinga mkubwa.”

 “Hilo jengo la Tanesco, narudia kama itakuwa ni kubomoa nusu, no problem (hakuna tatizo); kama ni lote hakuna tatizo, pamoja na jengo la wizara ya maji. Najua katibu mkuu wa wizara ya maji yupo hapa ananiangalia, wakaanze kulitoa eneo lililopo kwenye hifadhi ya barabara,” amesema.

Machi 6, 2011 akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Chato, mkoani Kagera, Pinda ambaye alisifia utendaji wa Dk Magufuli alimwagiza kusimamisha ubomoaji maeneo kadhaa yaliyokuwa kwenye hifadhi ya barabara likiwemo jengo la Tanesco hadi Serikali itakapotoa kauli nyingine kuhusu hilo.

Pinda alikuwa akizungumzia hatua ya Dk Magufuli aliyekuwa amewaagiza wananchi waliojenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba hizo na wasitarajie kulipwa fidia.

Pinda wakati huo akiwa waziri mkuu alisema spidi (kasi) ya Magufuli ilikuwa kubwa hivyo alimuagiza kusimamisha ubomoaji huo hadi suala hilo litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.

Pinda, ambaye alikuwa waziri mkuu kuanzia 2008 baada ya kujiuzulu kwa Edward Lowassa alisimamisha ubomoaji huo ili kutoa nafasi kwa Serikali kujipanga upya.

Alisema Serikali inamuamini Magufuli kuwa kiongozi mwenye uwezo na ndio maana ilimpa nafasi akawabane makandarasi wazembe.

Dk Magufuli akiwasilisha bajeti bungeni mwaka 2012/13, alizungumzia ubomoaji akisema siasa iachwe akisisitiza sheria zimepitishwa ikiwamo Sheria namba 13 ya mwaka 2007 na ya hifadhi ya barabara iliyoanza tangu mwaka 1932.

Alizungumzia jengo la Tanesco alisema liko kwenye hifadhi ya barabara na kwamba hata kama asipolibomoa yeye kuna siku litabomolewa vinginevyo sheria ibadilishwe.

Novemba 15 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Magufuli alimuagiza wakala wa barabara nchini (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.

Mwananchi:

Mourinho amponda Mkhitaryan, amwambia kiwango chake kimeshuka



Mkufunzi wa Manchester United Jose Mourinho ameukosoa mchezo wa Henrikh Mkhitaryan huku Borussia Dortmund ikisema kuwa iko tayari kumsajili kwa mara nyengine mshambuliaji huyo wa Armenia

Mkhitaryan, ambaye alijiunga na United kutoka Dortmund mwezi Julai 2016 kwa dau la £26.3m, hakushirikishwa katika kikosi cha United katika mechi mbili zilizopita.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hatahivyo atarudi katika kikosi cha kwanza cha United katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Brighton.

Mourinho alisema kuwa kiwango cha mchezo wa Mkhitaryan kimekuwa kikipungua hatua baada ya hatua

Mkhitaryan alianzishwa mechi 10 kati ya 11 za ligi ya Uingereza kabla ya kuachwa nje baada ya kutolewa katika dakika 62 katika mechi ambayo United ilipoteza kwa Chelsea kwa 1-0 mnamo tarehe 5 mwezi Novemba.

"Sikufurahia kiwango chake cha mchezo'', alisema Mourinho kuhusu mchezaji ambaye amefunga mabao mawili pekee katika mechi 16 alizochezeshwa msimu huu.

Waziri Kigwangalla awajibu wanaosema vyuma vimekaza




Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Hamisi Kigwangalla amesema maisha yataendelea kuwa magumu kwa watu wasio na shughuli maalum ambao wamezoea kuishi kwa ujanja ujanja.

Ameyasema hayo wakai akijibu maswali ya wananchi kupitia mtandao wa ‘Twitter’ ambao wengi walitaka kujua kuhusu utendaji kazi wake na hali halisi ya maisha yalivyo wakidai kuwa ni magumu.

“Wanaofanya shughuli zao halali hawatoona vyuma vimekaza, badala yake watafurahia sema watoto wa mjini, wasanii sanii na wajanja wajanja ndiyo watapata shida! Hawa wajanja wajanja ni wangapi? Na wenye shughuli halali ni wangapi?”, alisema Kigwangalla akiacha maswali kwa mmoja wa watu waliomuuliza.

Waziri Kigwangalla aliendelea kwa kutoa ufafanuzi juu ya namna ya kujenga uchumi kupitia kufanya kazi na sio kutegemea kupata pesa kwa njia rahisi rahisi.

“Mfumo wa uchumi unataka watu tufanye kazi kwa ubunifu ndipo tupate maisha mazuri siyo kufanya usanii kidogo tayari ukatajirika! Kukaza vyuma maana yake kuziba mianya ya wasanii ili walio kwenye uchumi halisi na wasanii wawe sawa siyo kuonea watu!” alimaliza.

Waziri Kigwangalla hivi sasa yupo jimboni kwake Nzega vijijini akiwa amepiga kambi kwaajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Nata.

CAF yataka Yanga, Simba Kupeleka Majina




Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezitaka Simba na Yanga haraka kupeleka majina ya wachezaji wake kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa ajili ya ushiriki wa michuano yake mwakani, pia watakaguliwa mahesabu yao.

Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, huku Simba wakishiriki Kombe la Shirikisho kutokana na kuwa mabingwa wa Kombe la FA.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema klabu hizo zinatakiwa kuwasilisha majina yao Caf mapema kabla ya mwisho wa mwezi huu.

“Simba na Yanga wanatakiwa kutuma majina ya usajili wa wachezaji wao mapema kabla ya Novemba 30, mwaka huu kwa sababu wakichelewa inaweza
kuwa tatizo kwao,” alisema Lucas.

 “Na kwa sasa kamati ya leseni za klabu inakwenda kufanya ukaguzi katika klabu hizo ili kufahamu kama zimetimiza matakwa ya kupata leseni ya kushiriki michuano ya Caf.

“Timu zitakaguliwa ofisini na watendaji wake, umiliki wa nyaraka mbalimbali, ukaguzi wa mahesabu na ripoti ya fedha ya mwaka mzima kama Kanuni ya 11 ya ligi kuu na kanuni ya saba ya Caf zinavyojieleza kuhusiana na leseni za klabu,” alisema Lucas.

Chelsea wawasili Liverpool tayari kwa kazi



Chelsea wametua salama jijini Liverpool kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Liverpool ambayo inasubiriwa kwa hamu leo Anfield.

Lakini kiungo mkongwe wa timu hiyo, Cesc Fabregas amefanya kituko wakati wakiwasili, ameonekana akiwa amefunika uso wake gubi gubi.

Kwa kila timu, mechi hiyo ni muhimu, Liverpool ikataka kurejesha imani na kasi yake katika EPL lakini Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wanataka kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutetea taji.

Tambwe yupo fiti kuivaa Tanzania Prisons leo



MSHAMBULIAJI Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe anatarajiwa kurejea leo timu yake, Yanga ikimenyana na Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Tambwe hajacheza mechi hata moja ya mashindano msimu huu, baada ya kuumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba Agosti  20 mwaka huu, Yanga ikijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba.

Na baada ya kufanya mazoezi mfululizo wiki hii, ikiwa ni mara ya kwanza kufuatia kushindwa kufanya mazoezi japo kwa siku mbili mfululizo awali, kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina anatarajiwa kumtumia Tambwe katika sehemu ya mchezo wa leo.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dissmas Ten alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba Tambwe yuko fiti na atakuwepo kwenye mchezo wa leo.

Ten alisema majeruhi ambao wataendelea kukosekana katika kikosi hicho ni Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao wote wanapambana na hali zao warejee uwanjani mapema. 

Kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi alikuwa anasumbuliwa na Malaria naye anaweza kukosekana katika mchezo wa pili mfululizo leo, baada ya kutokuwepo pia wakati Yanga ikiichapa 5-0 Mbeya City Jumapili iliyopita.

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliendelea jana kwa mchezo mmoja tu, wenyeji Ndanda FC wakilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mechi nyingine za leo, Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Kesho Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Zimbabwe: Morgan Tsvangirai aomba Mugabe kusamehewa



Kiongozi wa chama cha ZANU-PF Lovemore Matuke amesema kuwa hakushiriki katika harakati za kumuondoa Mugabe madarakani.

Kwa mujibu wa habari,Matuke amesema kuwa Mugabe na familia wako salama na daima atakumbukwa kama shujaa.

Wakati huohuo kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai amewataka wananchi wamsamehe Mugabe.

Morgan Tsvangirai amesema kuwa ni vyema Mugabe akasamehewa na taifa kwani si taifa halijengwi kwa kulipiza visasi.

Misri: Rais al Sisi aahidi adhabu kali kwa wliohusika na shambulizi dhidi ya mskiti Sinai


Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi aahidi adhabu kali kwa magaidi waliohusika na ashambulizi dhidi ya mskiti lililopelekea vifo vya watu zaidi ya 230  Sinai

Rais wa Misrii Abdel Fatah al Sisi ameahidi adhabu kali kwa magaidi waliohusika na shambulizi walilotekeleza  katika mskiti wakati wa kutekelezwa ibada ya Ijumaa.

Watu 235 walifariki na wengine zaidi ya 130 kujeruhiwa katia shambulizi lililolenga mskiti wa al Arish unaopatikana Sinai nchini Misri.

Jeshi la Polisi litatoa jibu linalostahili kwa waliotekeleza shambulizi hilo.


Wastara ateswa na macho yake




STAA wa filamu za Kibongo, Wastara Juma ameibuka na kueleza jinsi macho yake yanavyomtesa kwani watu wamekuwa wakimsema vibaya kuwa anajilegeza makusudi akitaka kutupia picha mtandaoni.

Akipiga stori na Risasi Jumamosi,Wastara alisema kuwa macho yake ndivyo yalivyo kwani amezaliwa hivyo ni macho yaliyolegea kama mtu mwenye usingizi wakati wote na kutokana na vichambo anavyovipata amejikuta akitamani kuhama Insta lakini hawezi kwa sababu ana manufaa na page yake.

“Jamani haya macho yananitesa kwani kutwa kucha natukanwa mitandaoni kuwa nalegeza macho hawajui kuwa nimeumbwa hivi kwani hata nikijitahidi kuyafanya yawe magumu nashindwa, hivyo watu wakisema najifanyisha huwa najisikia vibaya kusema ukweli,” alisema Wastara.

Baada ya kimya kirefu, Jokate afunguka kuhusu Lulu



MWANAMITINDO Jokate Mwegelo hivi karibuni baada ya kukaa kimya bila kumposti msanii mwenzake Elizabeth Michael ‘Lulu’ wala kuongea lolote kuhusiana na hukumu yake ambapo mastaa kibao walionesha kumuhurumia na k
umposti kwa kuweka maneno tofauti tofauti, yeye ameibuka na kusema kuwa anamuombea dua huko alikoenda kwani ndio jambo pekee ambalo anaweza kulifanya.

Akilonga na Risasi Jumamosi, Jokate alisema kuwa yeye anamuombea dua Lulu Mungu amfanyie wepesi huko alikokwenda kwani ndio njia pekee ya kumfariji.

Mwanamitindo huyo aliongea hayo baada ya kuulizwa sababu ya yeye kutomposti na maoni yake juu ya hukumu hiyo. “Kikubwa ni kumuombea na mimi namuombea ndicho ninachoweza kusema,” alisema Jokate.




Sikutarajia Dk Slaa kuwa balozi - Profesa Lipumba



   Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amezungumzia uteuzi wa Dk Wilbroad Slaa kuwa balozi akisema hakutarajia.

Rais John Magufuli juzi alimteua Dk Slaa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema kabla ya kukihama chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakati wa mchakato wa uchaguzi huo, Profesa Lipumba na Dk Slaa ambao vyama vyao vilikuwa katika umoja uliojulikana Ukawa, walijiondoa baada ya Chadema kumpitisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.

Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Lipumba alisema, “Imekuwa kama surprise, sikutegemea kama Dk Slaa atateuliwa kwa sababu muda mwingi yupo Canada.”

Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema hana shaka na uteuzi huo kwa kuwa Dk Slaa ni mzoefu wa siasa na mzalendo ambaye ataitumikia vyema nafasi hiyo mpya.

“Narudia, sikutegemea. Ila popote atakapopangiwa kazi Dk Slaa atafanya kwa sababu najua ni mchapakazi,” alisema.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Rais Magufuli ana mamlaka kisheria ya kumteua mtu atakayemuona anafaa katika nafasi fulani.

“Huu ni uamuzi wa Rais sisi wengine hatuna comments zaidi ya kuwatakia kila heri katika utendaji wao wa kazi,” alisema Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza uteuzi huo wa Dk Slaa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema Rais Magufuli amemuonea huruma Dk Slaa ndiyo maana akaamua kumpa nafasi ya ubalozi.

Profesa Safari alisema hawezi kumsema vibaya Dk Slaa lakini nafasi hiyo ni huruma na zawadi ya Rais Magufuli.

Amedai Dk Slaa alijaribu kuivuruga Chadema wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 lakini hakufanikiwa.

“ Hii ni huruma. Siku zilizopita Dk Slaa aliandikwa katika vyombo vya habari kuwa anafanya kazi Super Market. Mimi nimekaa Ulaya najua maisha ya kule na Dk Slaa ni rafiki yangu sana lakini kwa kitendo alichokifanya mwaka juzi, haya ndiyo matokeo yake,” alisema Profesa Safari.

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi kuanzia mwaka 2002 hadi 2008, Patrick Chokala alimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Dk Slaa kuwa balozi.

“Sina shaka hata kidogo na Dk Slaa ana uwezo wa kufanya kazi nchi yoyote. Hii kazi anaiweza na ni mtu mwenye dhamira ya kweli,” alisema Balozi Chokala.

Alisema anamfahamu Dk Slaa kwa kipindi kirefu tangu akiwa padre na kwamba, amekuwa ni mchapakazi hodari na mwenye hekima kwa watu.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam TV, Dk Slaa alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua ili aungane naye kujenga nchi na hivyo atafanya kazi kwa uwezo wake wote.

Dk Slaa ambaye hivi sasa anaishi Canada alisema, “Ni mapenzi ya Mungu, nashukuru kwa uteuzi. Ninachoweza kusema katika hatua hii, huu ni wajibu mkubwa kwenye kipindi cha kulijenga Taifa letu.”    

Mwananchi:

Wema Sepetu asema ameirudisha heshima ya Bongo Movie

Wema Sepetu asema ameirudisha heshima ya Bongo Movie


Msanii wa filamu nchini Tanzania, Mrembo Wema Sepetu ambaye yupo nchini Rwanda tangu Jumatano ya wiki hii, amesema ndiye aliyeifufua tasnia ya Bongo Movie iliyokufa baada ya kifo cha Kanumba.

Wema amesema marehemu Kanumba alipofariki  hata kiwanda cha Bongo Movie kilionekana kuyumba kwani alikuwa ndiye nguzo muhimu kwenye ramani ya filamu Tanzania.

“Zamani Bongo Movie ilikuwa inafanya vizuri sana enzi za marehemu Steven Kanumba, alivyofariki kama na yenyewe ikafa. Tumekuwa tukiomboleza kifo chake na kifo chake kimetusababishia mazingira mabaya sisi kama waigizaji  kwa sababu tuko kwenye fani moja. Wengi wetu tumejikuta watu wanaona Bongo Movie haina mashiko.“amesema Wema Sepetu kwenye mkutano na Waandishi wa Habari jijini Kigali nchini Rwanda na kuelezea jinsi alivyoinyanyua Bongo Movie baada ya kifo cha Kanumba.

“Kwa bahati nzuri mimi nimeweza kuirudisha tena Bongo Movie back to where it was (ilipokuwa enzi za Kanumba) baada ya kutoa filamu yangu ya Heaven Sent. Bongo Movie kama Bongo Movie zilikuwa zimelala kiukweli kabisa mpaka nilipozindua filamu yangu hiyo na nimeweza kuiweka kwenye application yangu kumekuwa kuna muhemko, yaani waigizaji wengi hata mkiwaona kwenye mitandao ya kijamii wanashoot, wanafanya vipindi, yaani Bongo Movie haijafa ni kazi nzuri tu tumeshindwa kuziweka sokoni. Tukiwa tuna kazi nzuri tukafanya vitu ambavyo vitapendwa na watu Bongo Movie itakuwa imara tena Inshallah!“.

Steven Charles Kanumba almaarufu The Great alifariki katika mazingira ya kutatanisha mnamo mwezi Aprili 2012 akiwa chumbani kwake na mpenzi wake Elisabeth Michael ‘Lulu’ ambaye mwezi huu amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumuua Kanumba bila kukusudia.

Waziri Kigwangalla awajibu wanaosema vyuma vimekaza




Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Hamisi Kigwangalla amesema maisha yataendelea kuwa magumu kwa watu wasio na shughuli maalum ambao wamezoea kuishi kwa ujanja ujanja.

Ameyasema hayo wakai akijibu maswali ya wananchi kupitia mtandao wa ‘Twitter’ ambao wengi walitaka kujua kuhusu utendaji kazi wake na hali halisi ya maisha yalivyo wakidai kuwa ni magumu.

“Wanaofanya shughuli zao halali hawatoona vyuma vimekaza, badala yake watafurahia sema watoto wa mjini, wasanii sanii na wajanja wajanja ndiyo watapata shida! Hawa wajanja wajanja ni wangapi? Na wenye shughuli halali ni wangapi?”, alisema Kigwangalla akiacha maswali kwa mmoja wa watu waliomuuliza.

Waziri Kigwangalla aliendelea kwa kutoa ufafanuzi juu ya namna ya kujenga uchumi kupitia kufanya kazi na sio kutegemea kupata pesa kwa njia rahisi rahisi.

“Mfumo wa uchumi unataka watu tufanye kazi kwa ubunifu ndipo tupate maisha mazuri siyo kufanya usanii kidogo tayari ukatajirika! Kukaza vyuma maana yake kuziba mianya ya wasanii ili walio kwenye uchumi halisi na wasanii wawe sawa siyo kuonea watu!” alimaliza.

Waziri Kigwangalla hivi sasa yupo jimboni kwake Nzega vijijini akiwa amepiga kambi kwaajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Nata.