Tuesday, 31 October 2017

RC Makonda anusuru zaidi ya Tsh Bilioni 1

RC Makonda anusuru zaidi ya Tsh Bilioni 1


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda leo amekabidhi Mabasi 10 chakavu ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kampuni ya DAR COACH LTD kwaajili ya kufufuliwa upya na kuwa ya kisasa.

Mabasi hayo 10 chakavu yanatoka kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ Magari 3, Jeshi la Polisi Magari 4 pamoja na Jeshi la Magereza Magari 3 ambapo yote kwa pamoja Matengenezo yake yameokoa kiasi cha Shilingi Billion 1,110,000,000 ya Serikali.

RC Makonda amesema kuwa Gari hizo zitatengenezwa na kukamilika ndani ya Siku 90 ambapo ameipongeza Kampuni ya DAR COACH LTD kwa kujitolea kukarabati Magari hayo bila kutumia pesa ya Serikali.

Aidha Makonda amesema Magari hayo yatafungwa Vifaa vya Kisasa ikiwemo Kiyoyozi (AC), Mfumo wa Chaji ya Simu kila Seat, Runinga, Radio, Viti vya kisasa, Vyoo vya Ndani, Bodi mpya pamoja na mwonekano mzima wa Gari ili ziwe za kisasa.

RC Makonda amesema mpango wake wa kuendelea kuongezea nguvu Vyombo vya Ulinzi na Usalama hautokoma kwakuwa lengo lake ni kuwatumikia Wananchi na Askari wajivunie kufanyakazi chini ya RC MAKONDA



Amemuagiza Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa kuhakikisha Ving'ora vya Jeshi la Polisi vinakuwa tofauti na kampuni za Ulinzi na Usalama, Magari ya Wagonjwa ili kupunguza Mkanganyiko kwa wananchi na kujengea heshima Jeshi la Polisi.

Katika hatua nyingine amewataka Wanasiasa kufanya Sasa za kistaarabu badala ya kutukana na kutoa lugha chafu kwa Serikali.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na usalama akiwemo Kamanda wa Polisi Dar es Salaam LAZARO MAMBOSASA, Mkurugenzi wa usafirishaji JWTZ Kanal RAJAB MWENYUMBU, Mnadhimu wa Jeshi la Magereza ACP. NOEL JAMES ambapo wote kwa pamoja wamempongeza RC Makonda

Aslay anunua BMW

Aslay anunua BMW



Msanii wa muziki wa bongo fleva Aslay Isihaka ambaye kwa sasa anafanya vyema na wimbo wake 'Natamba' amefunguka na kushukuru uongozi wake mpya kwa kufanikisha yeye kuweza kupata ndinga mpya aina ya BMW.


Aslay ambaye ndani ya muda mfupi ameweza kuachia nyimbo zaidi ya 10 na ngoma hizo nyingi kufanya vizuri na kupokelewa vyema na wananchi jambo ambalo limeweza kufungua milango kwa msanii huyo kuweza kupata show nyingi na mafanikio mbalimbali.

"Alhamdulillah Asantee Mungu kwa hiki ulichonipa naishukuru management yangu Chambusso na Mxcarter, nakupenda Mama yangu kokote ulipo kila hatua dua 'new car' Umma unaongea" alindika Aslay kupitia mtandao wake wa Facebook.

Aslay Isihaka kwa mara ya kwanza kuanza kumiliki gari yake alizawadiwa na uongozi wake wa kwanza wa Yamoto Band chini ya Mkubwa Fella katika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake mwaka 2015

Halima Mdee afunguka kuhusu bunge

Halima Mdee afunguka kuhusu bunge


Mbunge wa Kawe kupitia CHADEMA Halima James Mdee, amesema mambo yanayoendelea nchini yamechangiwa na kutokuwa na bunge imara, ambalo linashindwa kuwawajibisha viongozi wanapokwenda kinyume.

Halima Mdee ameyasema hayo alipokuwa akiongea na mwandishi wa East Africa Radio, na kusema kwamba hata Spika anayeliongoza Bunge hilo hana uamuzi huku akishindwa kuchukua uamuzi kadri mamlaka ya bunge yanavyomtaka


Wadau kutoka sekta mbalimbali wafurahishwa na kasi ya maendeleo inayoletwa na Rais Magufuli

Wadau kutoka sekta mbalimbali wafurahishwa na kasi ya maendeleo inayoletwa na Rais Magufuli


Ikiwa imetimia miaka miwili ya rais Magufuli tangu aingie madarakani kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wananchi,wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wameonesha kuridhishwa na kasi ya rais Magufuli katika maendeleo inayohusisha utendaji kazi wake pamoja na msimamo thabiti anaouonesha katika kulinda rasilimali za nchi ili kuwanufaisha watanzania walio wanyonge na masikini.

Hayo yamebainika kwa kutoka kwa wakazi waliopo jijini Dar es Salaam na pembezoni ambapo pamoja na mambo mengine wakazi hao wanaridhishwa na namna serikali ya awamu ya tano chini ya rais Magufuli inavyojitoa katika kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi haraka tofauti hapo awali huku wengine wakianisha  mambo ambayo rais Magufuli ameyatekeleza kwa haraka ndani ya miaka  miwili ilihali ya kwamba bado ana miaka mingine mambo hayo ikiwa ni  elimu bure,madawati,ujenzi wa miundombinu,kuokoa fedha zilizokuwa zikilipwa kwa watumishi hewa.

Aidha,kutokana na uchapakazi wake katika vita vya kiuchumi na kutaka  kulifikisha taifa katika uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda wananchi hao wamesema ni dira njema ya kuleta mafanikio kwa taifa hivyo rais Magufuli aendelee na juhudi zake za kutosikiliza maneno  ya wale wanaopinga juhudi hizo.

Mvua kubwa zatarajiwa kuanza kunyesha usiku wa leo

Mvua kubwa zatarajiwa kuanza kunyesha usiku wa leo




Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa(TMA) imetangaza vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya masaa 24 vinatarajiwa kuanza usiku wa kuanzia leo Jumanne.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo Jumanne imeeleza kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani pamoja visiwa vya Unguja na Pemba yataaririka.

“Mvua hiyo inatarajiwa kusambaa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Lindi kuelekea siku ya Ijumaa ya tarehe 3 Novemba 2017.”

“Hali hii inatokana na kuwepo na kuimarika kwa ukanda wa mvua (Inter Tropical Convergency Zone –ITCZ) katika maeneo hayo.”

Mamlaka hiyo imewataka wakazi wa maeneo yaliyotajwa kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zinazotolewa

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo kila itakapobidi

Meya wa jiji la Mwanza afunguka

Meya wa jiji la Mwanza afunguka



Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire amefunguka juu ya sababu zilizomfanya akamatwe na polisi wakati wa msafara wa Rais Magufuli alipokuwa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari Meya huyo amesema sababu ya kukamatwa kwake alielezwa ni amri kutoka kwa viongozi wa juu ili asiwepo kwenye msafara wa Rais, na kupata fursa ya kuzungumza yale ambayo anayajua.

Meya Bwire ameendelea kwa kusema kwamba katika jiji hilo kuna vitendo vya matumizi mabaya ya fedha pamoja na kudhulumu haki za wananchi, na kamwe hatoacha kuzungumza hata kama anahatarisha kibarua chake

Simba wampa Omog nafasi nyingine

Simba wampa Omog nafasi nyingine



Pamoja na taarifa kuendelea kuzagaa kwamba Kocha Joseph Omog kiota kimeanguka,

Kamati ya Utendaji ya Simba imekutana na kukubaliana Kocha Joseph Omog kuendelea kukinoa kikosi hicho.

Omog amekuwa katika hali ya hatihati kama vile atafukuzwa kazi kutokana na mwenendo wa timu yake.

Lakini taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza, katika kikao hicho wamekubaliana Omog kuendelea na kazi yake.

“Lakini ametakiwa kubadili mambo na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, Simba inataka ushindi,” kilieleza chanzo.

Mwenendo wa Simba katika mechi nane ilizocheza imekuwa ni milima na mabonde kwa kupitia ushindi, sare, ushindi sare.

Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa taarifa nyingi ambazo zinaeleza kwamba Omog anakaribia kutimuliwa.

Hata hivyo, bado hali inaonekana kuwa haijatulia na Omog atalazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha anabadili mambo.

Yanga kumkosa Juma Abdul kwenye mechi dhidi ya Singida United

Yanga kumkosa Juma Abdul kwenye mechi dhidi ya Singida United



Wakati Yanga itakuwa na kibarua cha kuivaa Singida United kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida, wikiendi hii, taarifa za uhakika zinaeleza, itamkosa beki wake wa kulia, Juma Abdul.

Abdul ana kadi tatu za njano, ya mwisho akiwa ameipata katika mechi dhidi ya Simba, Jumamosi.

"Juma ana kadi tatu, kadi ya tatu ameipata dhidi ya simba baada ya kupata nyingine dhidi ya Kagera. Hivyo hatacheza mechi ya Singida," taarifa zilieleza.

Hakuna mtu wa benchi la ufundi la Yanga alipatikana kuzungumzia baada ya simu zao kuwa zinaita bila majibu.

Lakini taarifa nyingine zikaeleza kuwa, tayari Yanga wana taarifa kuhusiana na Juma Abdul.

"Hatakuwa katika mipango ya safari, benchi la ufundi linajua Juma ana kadi tatu.

Mavugo akalia kuti kavu Simba

Viongozi wa Simba wameonyesha kutofurahishwa na uchezaji wa mshambuliaji wao Laudit Mavugo hasa kutokana na kushindwa kuonyesha juhudi uwanjani.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza, viongozi wa Simba wamemtaka Mavugo kujituma na kama inashindikana basi wataachana nao.

"Viongozi hawajafurahishwa na Mavugo kwa kuwa hajaonyesha juhudi zozote katika mechi dhidi ya Simba.

"Unajua hata katika upangaji, awali kocha alionekana kama nafasi ya kuanza angempa Bocco. Lakini alibadili ikawa ni Mavugo," kilieleza chanzo.

"Viongozi wao hawana uwezo wa kumuingilia kocha lakini wanakerwa na namna Mavugo asivyoonyesha kama ana uchungu. Hivyo walitaka kama ameshindwa aende zake.

"Tayari kaelezwa kuwa lazima ajitume na acheze kuitumikia timu na kuisaidia kwa kuwa kama ilivyo kwa wengine anapata kila kinachotakiwa."

Lisu afunguka kuhusu Nyalandu






Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema), Tundu Lissu amempongeza aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki(CCM), Lazaro Nyalandu kwa kupata ujasiri wa kuchukua hatua kubwa ambayo hata wabunge wengi waliopo ndani ya CCM wanashindwa kuichukua.

Lissu ambaye yuko kwenye matibabu jijini Nairobi  amempongeza Nyalandu kwa kuwa ni alikuwa mbunge jirani yake na kuwa ujasiri wa kufanya hivyo.

Mbali na kumpongeza Nyalandu pia Lissu amezungumzia  uchaguzi wa madiwani katika kata 43 akieleza kuwa kuwapa CCM kura katika kata hizo ni sawa na kukubaliana na yanayoendelea nchini.

“Kuwapa CCM kura sasa hivi ni sawa na kuwapa CCM mamlaka ya kutapanya mali zetu kama wanavyotaka,”amesema Lissu leo Jumanne akiwa jijini Nairobi

VIDEO: Makonda amjibu Nyalandu

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amewata wanasiasa  kukubaliana na hali ya mabadiliko kwani sasa ni muda wa kufanya kazi na sio wakati wa kutafuta umaarufu na maneno mengi.
TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI

Msigwa: Nyarandu amewaonyesha watanzania mambo saba muhimu

Msigwa: Nyarandu amewaonyesha watanzania mambo saba muhimuMbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya (CHADEMA) Peter Msigwa amefunguka na kumpongeza Lazaro Nyalandu na kumwambia kuwa amechukua uamuzi sahihi kuachana na chama hicho na kusema amewaonyesha watanzania mambo saba muhimu.


Msigwa amesema kitendo cha Nyalandu jana kuamua kuachana na Chama Cha Mapinduzi ni wazi kuwa amethibitisha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) si chama tena bali kimekuwa chini ya dola na hakina uwezo wa kuikosoa serikali tena. Msigwa aliainisha mambo hayo saba kama ifuatavyo

1. Nyalandu umethibitisha kwamba CCM sio Chama Cha siasa tena. CCM iko chini ya miguu ya dola na haina uwezo wa kuikosoa serikali tena

2. CCM imepoteza mwelekeo wake. Imeshindwa kusimamia uchumi, siasa na uongozi wa nchi
3. Misingi ya nchi yetu imebomolewa chini ya utawala wa CCM na umeitisha mwito wa kila mmoja wetu kuijenga upya misingi ya nchi yetu

4. Tanzania imekithiri ukiukwaji wa haki za binadamu , dhulma na kutekwa na serikali mhimili wa bunge pamoja mahakama.

5. Watanzania wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inafaa na sio kutishiwa na kulazimishwa.

6. Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini yatapatikana kwa mfumo wa demokrasia na Uhuru wa mawazo.

7. Mwisho umeonesha umuhimu wa kupata Katiba Mpya kwa sasa katika Nchi yetu
Mbali na hilo Mbunge Msigwa alimaliza na kusema kuwa "Kuishi nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inawezekana"

CCM kupeleka vijana Ulaya

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa fursa ya kuwapeleka barani Ulaya vijana watakaochaguliwa na shirikisho la soka nchini Tanzania TFF kwaajili ya kupata mafunzo ya kuchezesha soka.

Hilo limedhibitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho ndugu Humphrey Polepole kwenye mahojiano na eatv.tv ambapo amebainisha kuwa fursa hiyo imetolewa na vyama rafiki vya chama hicho kwenye nchi za Ulaya.

Polepole amesema kupitia kikao kikubwa cha vyama vyote vya kijamaa barani Afrika na Ulaya kilichofanyika mapema mwaka huu ilitolewa fursa kwa CCM kuweza kupeleka vijana kwenye baadhi ya nchi barani Ulaya ili kupatiwa mafunzo hayo.

Aidha Polepole amebainisha kuwa zoezi hilo litasimamiwa na TFF kwasababu wao ndio wana dhamana ya kupitisha watu wanaohusiana na soka hivyo watashirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha vijana wanatumia fursa hiyo ambapo baada ya mafunzo hayo watarudi kuitumikia sekta ya michezo nchini.