Tuesday, 31 October 2017

Sababu za Rais Magufuli Kutokugawa Milion 50 Alizoahidi Kwa Kila Kijiji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ameeleza sababu zinazomfanya achelewe kutimiza ahadi ya milioni 50 kwa kila kijiji alizoziajidi wakati wa kampeni za kugombea urais kuwa ni kutokana na kuwepo kwa mambo mengi nchini yanayohitaji utekelezaji wa haraka.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika mkutano wa hadhara ikiwa ni moja ya vitu alivyopanga kuvifanya katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani hapo.

Ameeleza kuwa ameona ni sahihi kuanza na mambo ya muhimu zaidi kama vile miundombinu ya barabara, huduma za afya pamoja na elimu kabla ya kutoa fedha hizo ambazo aliziahidi katika iilani ya uchaguzi wa mwaka 2015.

“Halitokuwa jambo jema mimi kutoa milioni 50 kwa kila kijiji nchini wakati huduma mbalimbali kama vile elimu, afya na miundombinu ya barabara na usafirishaji haijakaa vizuri. lakini niwahakikishie kuwa hizo fedha zipo na zitakabidhiwa kwa kila kijiji kama nilivyosema,” alisema Rais Magufuli.

“Inabidi muwe watulivu wakati serikali ikishughulikia matatizo na changamoto zinazohitaji utatuzi wa haraka kabla hatujazitoa fedha hizo,” aliongeza Rais Magufuli.

Rais Magufuli alimtaka pia Mkuu wa mkoa wa mwanza kuhakikisha kuwa anachochea maendeleo ya viwanda na kupitia hivyo nchi itapata maendeleo.

“Viwanda vitatengeneza ajira nyingi kwa watanzania na vitaongeza mapato ya serikali. Mapato yakiongezeka serikali itaweza kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi,” Alisema Rais

Polisi wawili wasimamishwa kazi



Polisi wawili wa trafiki nchini Afrika Kusini wamesimamishwa kazi na wanakabiliwa na mashtaka ya kuaibisha kikosi cha polisi baada ya video yao "wakila pesa" kusambaa sana mitandao ya kijamii.

Video hiyo inawaonesha polisi hao wawili wakitumia noti za pesa kuchonokoa meno yao na pia kujipangusa, huku muziki wa sauti ya juu ukisikika kwenye gari lao.

Wawili hao wanaonekana pia wakila chakula chao cha mchana kutoka kwenye mikebe ya Styrofoam kwenye sehemu ya kubebea mizigo nyuma ya gari.

Idara ya polisi wa jiji la Ekurhuleni amesema wafanyakazi hao, ambao wamevalia sare rasmi ya polisi wakati huo, wameiaibisha idara hiyo na kwamba vitendo hivyo si vya kistaarabu.

Msemaji wa idara hiyo Wilfred Kgasago amesema wawili hao wamekabidhiwa barua za kuwasimamisha kazi mapema na kwamba watafika katika kamati ya nidhamu Jumanne.

Waziri wa polisi nchini Afrika Kusini Fikile Mbalula alipakia video hiyo kwenye Twitter mwishoni mwa wiki, na akafurahia hali kwamba wawili hao wataadhibiwa.

Neymar aanza kuimisi Barcelona


Hivi majuzi wikiendi Neymar alionekana nchini Hispania akirudi kuwasalimia washkaji zake wa Barcelona na kuonekana kupiga nao story nyingi sana hii ikiwa karibia mara ya tatu kwa Mbrazil huyo kurudi.

Lakini wakati akiwa Hispania kumetoka ripoti toka Ufaransa kwamba Neymar hafurahii tena maisha ya PSG na Ufaransa kwa ujumla na ndio maana kila baada ya mechi huwa anaondoka nchini humo.

Ugomvi kati ya Neymar na mshambuliaji mwenzake Edison Cavanni unatajwa kuwa moja kati ya sababu kubwa kwa Neymar kutopapenda PSG huku habari mpya zikidai Neymar hamfurahii kocha wa klabu hiyo.

Neymar inasemekana kwamba hafurahii mbinu za kocha Unai Emery na inasemekana kocha huyo hapendwi na wachezaji wengi wa PSG kwani anawafanya wakose raha na kutojisikia amani PSG.

Kingine kinachomfanya Neymar kujutia PSG ni habari kwamba wachezaji wenzake hawana furaha kutokana na upendeleo anaopewa na anamiss furaha aliyokuwa nayo akiwa na MSN wakati wa Barcelona

Polisi wakamata Vifaranga vya kuku 6,400



Arusha. Vifaranga vya kuku 6,400 vinatarajiwa kuchomwa moto baada ya kunaswa vikiingizwa nchini kupitia Longido mkoani Arusha.

Vifaranga hivyo vilikamatwa juzi vikitokea nchini Kenya.

Taarifa zinasema thamani ya vifaranga hivyo ni Sh12.5 milioni na ni mali ya mfanyabiashara Mary Matia (23) mkazi wa Mianzini jijini Arusha anayeshikiliwa na polisi.

Akizungumza na Mwananchi katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Namanga, ofisa mfawidhi wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Kaskazini, Obedi Nyasembwa alisema tangu mwaka 2007 Serikali ilipiga marufuku kuingiza mayai na vifaranga kutoka nje ya nchi.

Alisema uamuzi huo wa Serikali ulichukuliwa ili kudhibiti magonjwa ya mifugo ukiwamo wa mafua ya ndege.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003, vifaranga hivi tutaviteketeza kwa kuwa vinaweza kuwa na magonjwa,” alisema.

Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka wa Namanga, Edwin Iwato alisema kwa mujibu wa sheria vifaranga hivyo havikupaswa kuingizwa nchini, hivyo licha ya kuviteketeza, gari lililotumika kuvisafirisha litatozwa faini.

Akizungumza akiwa chini ya ulinzi wa polisi, mfanyabiashara Matia alikiri kuingiza nchini vifaranga hivyo akisema hakuwa akijua kama uingizaji umepigwa marufuku.

“Naomba wasivichome moto vifaranga, ni bora waniruhusu nivirudishe Kenya kwa kuwa ninadaiwa Sh12.5 milioni nilikovinunua,” alisema.

Hata hivyo, ofisa mfawidhi mkaguzi wa Mifugo, Medard Tarimo alisema kwa muda mrefu yamekuwapo malalamiko ya kuingizwa nchini vifaranga na mayai lakini wamekuwa wakishindwa kuwakamata wahusika.

“Wamekuwa wakipita njia za panya usiku na kuingiza nchini jambo ambalo ni la hatari kwa afya za binadamu kwa kuwa nchi jirani tu ya Uganda kuna ugonjwa wa mafua ya ndege,” alisema

Sweden yamwaga mabilioni



SWEDEN imetoa Sh. bilioni 80.4 kwa Umoja wa Mataifa (UN) ili kusaidia kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuhamasisha wanawake kushiriki katika siasa nchini.

Fedha hizo pia zitaelekezwa katika kusaidia kukuza uchumi, upatikanaji wa ajira, kuimarisha utawala bora na usawa wa kijinsia.

Katika hafla ya kutiliana saini jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt, alisema msaada huo kwa kiasi kikubwa utaelekezwa kusaidia masuala ya kimaendeleo kwenye maeneo yanayomgusa mwanamke.

Alisema Sh. bilioni 33 zitatumika kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa wanawake na vijana wakati Sh. bilioni 22 zitatumika kwa ajili ya kuleta uwazi na uwajibikaji serikalini, kuimalisha shughuli za kibunge, haki za binadamu, kuwakinga waandishi wa habari na kuziinua redio ndogo zisizosikika ili wananchi wapate zaidi habari.

Alisema Sh. bilioni 26.4 zitatumika kuwahamasisha wanawake kushiriki siasa na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Balozi huyo alisema msaada huo pia utakuza uchumi na kusaidia wananchi na nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati.

"Kupitia Umoja wa Mataifa tunaiunga mkono Tanzania katika kufikia malengo iliyojiwekea. Pia tunatambua mchango wa Umoja wa Mataifa katika kufanikisha maendeleo endelevu,” alisema Rangnitt.

Katika hafla hiyo, Mratibu Mkaazi wa UN nchini, Alvaro Rodrigues, alisema Sweden imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa miongo mingi kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum.

Alisema msaada huo utaisaidia UN kuwafikia watu wasio na ajira, kuwawezesha wanawake pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto

Yanga kumaliza hasira zao kwa Singida United.

KOCHA WA TIMU HIYO, GEORGE LWANDAMINA.

BAADA ya kuambulia pointi moja dhidi ya Simba kwenye mechi iliyopita katika Uwanja wa Uhuru, Yanga itaondoka Dar es Salaam kesho kuelekea Singida ikiwa na hasira ya kukisambaratisha kikosi cha Hans van der Pluijm, Singida United.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, kama ilivyo kwa Singida United na Simba, Jumamosi ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya watani zao hao wa jadi kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kikosi hicho cha Yanga katika safari hiyo, kitaendelea kuikosa huduma ya wachezaji wake wa kigeni, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko ambao bado hawajapona kwa asilimia 100.

Akizungumza na Nipashe jana, kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, alisema kuwa matokeo waliyoyapata dhidi ya Simba yamewapa ari ya kufanya vizuri kwenye mchezo wao huo wa ugenini.

"Hatutakuwa na Tambwe, Ngoma na Kamusoko kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Simba, lakini hilo halinipi shida sana, nakiamini kikosi changu," alisema Lwandamina.

Alisema tofauti kwao ni kwa kuwa wanacheza mchezo huo ugenini na Singida ni moja ya timu imara kwenye Ligi Kuu msimu huu.

"Naamini tutafanya vizuri, wachezaji wangu wana ari na morali ya juu hasa baada ya matokeo tuliyoyapata dhidi ya Simba... tumekuwa na wachezaji majeruhi ambao ni muhimu na mchango wao unahitajika, lakini tumefanikiwa kuhimili changamoto za Ligi Kuu," alisema kocha huyo raia wa Zambia.

Kikosi cha timu hiyo leo kitaanza mazoezi ya uwanjani kwenye uwanja wa Uhuru baada ya jana kufanya mazoezi ya viungo gym.
Yanga wataondoka Dar es Salaam leo kwa basi kuelekea Singida tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Namfua ambao ukarabati wake umekamilika.

Mabingwa hao watetezi wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 16 sawa na vinara Simba, Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini Wanamsimbazi hao wanabebwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa

Sunday, 29 October 2017

Tutaunda silaha yoyote kujilinda - Iran

Tutaunda silaha yoyote kujilinda - Iran

Rais wa Iran amesema kuwa nchi yake itaunda silaha zozote inazohitaji kujilinda dhidi ya uvamizi.

Wakati akihubia bunge Rais Hassan Rouhani, alisema kuwa Iran haitakuwa ikikiuka makubaliano yoyote ya kimataifa kwa kuunda silaha yakiwemo makombora ya masafa marefu.

Aliionya Marekani kuwa ukiukaji wa mkataba wa nyuklia uliotiwa sahihi kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu ni kwa manufaa yake.

Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni alikataa kuidhinisha mkataba huo akiitaja Iran kama nchi kaidi inayounga mkono ugaidi.

Ushindi wa Anthony Joshua dhidi ya Takam wapingwa na mashabiki

Ushindi wa Anthony Joshua dhidi ya Takam wapingwa na mashabiki

Hata kabla ya mpambano bondia Anthony Joshua alishatabiri kwamba inaweza kumchukua raundi 10 kumpiga mpinzani wake Carlos Takam na hakufanya kosa na alitimiza ahadi yake.

Pamoja na kuzomewa na mashabiki wengi waliokuwepo uwanjani hapo kushuhudia pambano hilo lakini Anthony Joshua amefanikiwa kutetea ubingwa wake wa IBF.

Muamuzi wa mpambano huo aliamua kuukatisha katika raundi ya 10 baada ya mpinzani huyo wa Anthony Joshua kuonekana anavuja damu nyingi kwenye uso wake juu ya jicho kutokana na ngumi za AJ.

Lakini watu walizomea maamuzi hayo kwani pamoja na kuvuja damu lakini Takam alionekana bado yuko fiti na ana nguvu kwani alikuwa akiendelea kurusha ngumi japokuwa alikuwa amepasuka usoni.

Wengi baada ya mchezo huo wanaamini Takam alionewa na muamuzi kwa kukatisha pambano hilo na badala yake angeendelea kumpa muda wa kusimama ulingoni kupigana.

Baada ya mpambano huo promota wa Joshua bwana Eddie Hean amewaahidi mashabiki wa Joshua kwamba mwakani Joshua atakuwa na mpambano mkubwa mwingine huku Tyson Furry akipewa nafasi.

Anthony Joshua amejitamba kwamba angeweza kummaliza na kumuumiza zaidi Carlos Takam lakini maamuzi ya muamuzi wa mpambano huo yamemuokoa Mcameroon huyo na sasa Aj anakuwa ameshinda mapambano 20 mfululizo.

Helikopta ya Urusi iliyopotea yapa

Helikopta ya Urusi iliyopotea yapa                             

Mabaki ya helikopta ya Urusi iliyokuwa imepotea Svalbard nchini Norway yamepatikana.

Kwa mujibu wa habari,helikopta hiyo imekuwa ikitafutwa toka 26 mwezi Oktoba.

Helikopta hiyo imepatikana ufukweni.

Raia wa Urusi nane,watano wakiwa ni wafanyakazi wa helikopta hio huku watatu wakiwa ni abiria wa kawaida wanakisiwa kuwa wamefariki tayari.

Uchunguzi zaidi unaendelea

Uturuki yalaani vikali shambulizi lililofanywa nchini Somalia

Uturuki yalaani vikali shambulizi lililofanywa nchini Somalia

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amelaani vikali shambulizi lililosababisha vifo vya watu takriban kumi mjini Mogadishu.

Kwa mujibu wa habari,waziri huyo katika mtandao amewatakia amani wale wote waliopoteza maisha na kutuma salamu za rambirambi kwa familia zote zilizofikiwa na msiba huo.

Uturuki vilevile imeahidi kuwa na Somalia bega kwa bega katika kupambana na ugaidi.

Watu takriban kumi wamepoteza maisha huku wengine nane wakiwa wamejeruhiwa vibaya katika milipuko miwili ya gari katika moja ya hoteli mjini Mogadishu.

Ripoti zilizotolewa na kituo cha habari cha Somalia (SONNA) zimeonyesha kuwa kati ya waliopoteza maisha ni mbunge wa zamani Abdinasir Garane na Mkuu wa polisi wa zamani Mohamed Yusuf.

Samatta afikisha mechi 69 akiwa na KRC Genk jana

Samatta afikisha mechi 69 akiwa na KRC Genk jana

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza mechi yake ya 69, timu yake, KRC Genk ikilazimisha sare ya 0-0 na wenyeji, KV Kortrijk katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A, Ubelgiji uliofanyika Uwanja wa Guldensporen mjini Kortrijk.

Samatta alicheza kwa dakika 70 kabla ya kumpisha  Nikolaos Karelis aliyekuwa anarejea uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.

Katika mechi hizo 69, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mechi za mashindano yote tangu alipowasili Genk Januari mwaka jana akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika mechi hizo, Samatta ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka jana alipokuwa na Mazembe, 41 ameanza na mechi 24 ametokea benchi.

Kikosi cha KV Kortrijk kilikuwa: Kaminski, Verboom, Kovacevic, Rougeaux, Attal, D'Haene/Kagé dk84, Vanderbruggen, Azouni, Ajagun, Chevalier and Perbet/Budkivskyi dk72.

KRC Genk : Vukovic, Uronen, Colley, Aidoo, Mata/Maehle dk74, Heynen, Writers, Malinovskyi/Buffalo dk87, Pozuelo, Samatta/Karelis dk70 na Ingvartsen.

Kiongozi wa Catalonia apewa nafasi ya kushiriki uchaguzi ujao

Kiongozi wa Catalonia apewa nafasi ya kushiriki uchaguzi ujao

Serikali ya Uhispania inasema kuwa inakaribisha kushiriki kwa kiongozi aliyefuwa wa Catalonia Carles Puigdemont kwenye uchaguzi mpya.

Serikali ya Madrid imeamrisha kuwa uchaguzi mpya kwa bunge la eneo la Catlonia utafanyika mwezi Disemba.

Madrid ililivua eneo la Catalonia utawala wake baada ya bunge la Catalonia kupiga kura ya kujitangazia uhuru,

Bwana Puigdemont amewashauri watu kukataa udhibiti kamili kutoka Madrid.

Alilaani kufutwa kwa utawala wa Catalonia na kuahidi kuendelea kufanya kazi ya kujenga nchi ili huru.

Wakati huo huo mamia ya raia wa Uhispania wamekusanyika katika mji mkuu Barcerlona kuunga mkono umoja wa Uhispania.

Aidha Uhispania inaendelea kushinikiza kuchukua udhibiti wa nguvu dhidi ya serikali ya jimbo la Catalonia, iliyofutiliwa mbali.

Yaya Toure ataka kuinua kombe la UEFA akiwa na Man City

Yaya Toure ataka kuinua kombe la UEFA akiwa na Man City

Nyota wa Manchester City Yaya Toure amesema anatamani kutwaa ubingwa wa UEFA akiwa na timu hiyo ili kukamilisha ndoto yake.

Toure amedai furaha pekee anayoitamani ndani ya kikosi cha Manchester City ni kushinda taji la Ligi ya mabingwa barani Ulaya kwani  ndio kombe pekee ambalo hajafanikiwa kutwaa akiwa Etihad.

Yaya Toure hadi sasa ametwaa makombe mawili ya EPL, mawili ya EFL pamoja na moja la FA hivyo anaona kama hadaiwi chochote kutoka nchini England zaidi ya ubingwa wa Ulaya.

Raia huyo wa Ivory Coast ameshawahi kutwaa ubingwa wa UEFA akiwa na FC Barcelona mwaka 2009, hivyo anahitaji taji lake la pili la Ulaya.