Tuesday 5 December 2017

Bomoabomoa yawaathiri Wafanya Biashara wanafanya shughuli zao chini ya miti



 picha ya mtandao

    Dar es Salaam. Uboreshaji wa miundombinu ya usafiri unazidi mchungu kwa wakazi wa Dodoma, ambako wafanyabiashara wanafanya shughuli zao chini ya miti, na na Dar es Salaam, ambako wanatafakari jinsi ya kuukabili mwezi Januari ulio na mahitaji mengi ya kifedha.

Mjini Dodoma, wafanyabiashara wamebomolewa mabanda yao kupisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa, wakati wakazi wa Dar wanatakiwa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro.

Ada za watoto kwa ajili ya mwaka 2018, gharama za usafiri, sikukuu na kodi ya pango ndiyo mambo ambayo wakazi hao wa eneo la Ubungo hadi Kimara hawajui watayatekelezaje wakati huu ambao nyumba zao zilizojengwa ndani ya mita 91 kutoka katikati ya barabara, zinatakiwa zibomolewe.

“Hapa nawaza kipato ninachopata, watoto wanatakiwa ada mwezi Januari, wanataka nguo za sikukuu, huko niendako nahitaji kupanga chumba. Kwa hiyo ni majukumu juu ya majukumu,” alisema mkazi wa Kimara Bucha, Anastazia Alfred alipohojiwa na Mwananchi.

Anastazia alisema wapo tayari kuondoka, lakini kinachowaumiza ni hali ngumu waliyonayo hasa kwa kipindi hichi cha mwezi Desemba.

Anastazia, ambaye ni mama wa watoto watatu, alisema watoto wake wanahitaji kulipiwa ada, sare, na nguo za siku kuu lakini hataweza kuyamudu yote kwa kuwa hali ni ngumu.

“Jana tu watoto wameniuliza kuhusu nguo za sikukuu. Nawaonea huruma kwa sababu sikukuu ni siku ya kufurahi lakini mimi nawaza nitakuwa wapi kipindi hicho,” alisema.

“Hapa nawaza tu nipate pesa ya ada ili watoto waende shule mwezi ujao na kama Mungu akijalia nipate hifadhi kwa ndugu ili wakija hapa wabomoe tu. Nipo tayari vitu viharibiwe kwa kuwa sitamuda gharama za kuvihamisha.”

Mkazi mwingine wa Ubungo, Joyce John alisema mwezi huu kuna mambo mengi atashindwa kuyatekeleza kutokana na changamoto ya fedha, akitoa mfano wa gharama za kusafirisha vyombo wakati wa kuhama.

Alisema alikuwa amelenga kutafuta ada kwa ajili ya watoto pamoja na sare za shule, lakini amejikuta akikabiliwa na gharama nyingine ambazo hakuzitarajia.

“Walivyokuja kuweka alama ya ‘X’ nilijua hadi mwezi wa tatu kwa kuwa ni mwezi ambao hauna mambo mengi kwa watoto kama ilivyo mwezi huu wa mwisho wa mwaka,” alisema.

Alisema Serikali ingesogeza mbele ubomoaji ili wakazi waweze kumudu gharama za shule ambazo ndizo zinazowaumiza vichwa wazazi wengi hasa kuanzia kipindi hiki cha Desemba hadi Januari.

Frank Damas, aliyeishi katika eneo hilo kwa miaka sita, alisema anapenda maendeleo lakini haya yana maumivu kwa kile alichodai kuwa baadhi ya wananchi wapo kwenye hali mbaya kifedha.

Alisema kuwa ndani ya hifadhi ya barabara ni kosa, lakini waliuziwa maeneo hayo bila wao kujua kuwa ni hifadhi ya barabara.

“Yani huu ndio mwezi ambao tutaona mengi. Mfano mimi sina watoto, lakini nawaza kwa wale wenye watoto wanaohitaji ada, nguo za sikukuu, bado aende akapange na siku ya kuondoka anahitaji usafiri,” alisema Damas.

Alisema wamepewa notisi muda ambao kila mtu anauona mrefu kutona na matukio mengi kuhitaji pesa.

Dodoma nao walia

Wakati wakazi wa Dar es Salaam wakitafakari hayo, ubomoaji majengo mjini Dodoma unaofanywa na Kampuni ya Miliki ya Mali za Reli (Rahco) wamelazimika kufanya biashara zao chini ya miti na miavuli mikubwa baada ya kukosa maeneo.

Ubomoaji wa maeneo yao ya biashara ulifanyika kwa siku mbili (Jumamosi, Jumapili) na umevikumba vibanda 487 na nyumba 128, kikiwemo kituo cha mafuta, ofisi za mabasi ya Shabiby, ABC na mighahawa mikubwa mitano,

Jana, mawakala wa kampuni za mabasi yanayosafiri kwenda nje ya mkoa walikutwa chini ya miti na wengine katika miamvuli mikubwa wakiwahudumia wateja wao.

Wauzaji wa vyakula nao walionekana wakipika na kuhudumia wateja wao chini ya miti na miavuli.

Jengo kubwa lililojengwa katika viwanja vya mashujaa ambalo hutumika kama jukwaa la viongozi wakati wa shughuli za hadhara, pia limewekewa alama ya kutakiwa kubomolewa.

Katika maeneo ya kituo cha mabasi cha Jamatini ambako kuna wauza mitumba na migahawa mikubwa, wafanyabiashara walikutwa wamejikusanya wakijadiliana ubomoaji na wengine wakibeba vipande vya mbao na mabati vilivyobakia.

Mwenyekiti wa Usafirishaji wa Mkoa wa Dodoma, Laurent Mwashinga alisema hadi sasa hawajapata taarifa yoyote kutoka Manispaa ya Dodoma kuwa wataendeshaje shughuli zao baada ya vibanda vyao kubomolewa.

“Kama unavyotuona inabidi tujibanze katika miti hapa ili tuwahudumie wateja wetu,” alisema.

“Sasa ikija mvua ndio itakuwa shughuli maana hata pakujificha kwa majirani zetu nao wamevunjiwa.”

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa eneo la Jamatini, Neema Ally alisema mgogoro wa kutakiwa kuondoka eneo hilo ulianza Julai mwaka huu na kulikuwa na mabishano kati ya manispaa na Rahco kuhusu nani hasa mmiliki wa eneo na aliyepaswa kulipa kodi.

“Lakini baada ya kutokea kwa mgogoro huo, uongozi wa manispaa ulituhakikishia kuwa eneo hili ni mali yao na kututaka tuendelee kulipa kodi kwao,” alisema.

“Hata hivyo watu waligawanyika wengine walikwenda kuchukua mkataba Rahco ili kuwalipa na wengine walitaka kuendelea na manispaa.”

Hata hivyo, alisema walishindwa kufikia muafaka na hivyo kuacha kulipa kodi hadi Novemba walipokuja kubomolewa na Rahco na kwamba ubomoaji huo umesababishwa na mgogoro.

Lakini ofisa uhusiano wa Rahco, Catherine Moshi alisema ubomoaji haihusiani na mgogoro wa nani alipwe kodi ya pango.

No comments:

Post a Comment