Friday, 2 February 2018

Meli ya mizigo yapinduka


Meli ya mizigo imetipotiwa kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja China.

Kwa mujibu wa habari,wafanyakazi sita wa meli hiyo walianguka katika maji baada ya ajali hiyo kutokea.

Shirika la Shingua limetangaza kuwa ajali hiyo imetokea katika mto wa Yangtze katika mji  wa Huanggang.

Meli hiyo ilikuwa ina wafanyakazi sita,mmoja wao akiwa amefariki huku watano wengine hawajulikani walipo mpaka sasa.

Timu ya uokoaji iliweza kumtoa mmoja wao katika maji lakini haikuwezekana kuyanusuru maisha yake.

Juhudi za kuwatafuta wafanyakazi watano waliobaki zinaendelea.

Tundu Lissu amlilia Mzee Kingunge


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amezungumzia kifo cha Kingunge Ngombale Mwiru akisema historia itamkumbuka.

Akizungumza leo Februari 2, 2018 na Mwananchi akiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu ya viungo, Lissu akizungumzia kifo hicho ameanza kwa kusema “namtakia mapumziko mema.”

Amesema Mzee Kingunge alikuwa miongoni mwa wazee wenye historia kubwa na alionyesha ujasiri mkubwa wa kuhama chama chake cha CCM bila kuhofia kuhudhuriwa kutokana na mazingira yalivyokuwa.

“Ni mmoja wa wazee walioonyesha ujasiri mkubwa katika mazingira ya siasa za Tanzania yalivyokuwa, akahama chama tena CCM bila hofu za kuhudhuriwa  akaeleza madhabi yake kuwa hiki chama (CCM) kinatupeleka kuzimu,” amesema Lissu na kuongeza “historia itamkumbuka.”

Kingunge aliyekuwa kada wa CCM mwenye kadi namba nane, Oktoba 4, 2015 alitangaza kukihama chama hicho na kusema hatojiunga na chama chochote lakini mara kadhaa alionekana akipanda majukwaa ya upinzani kumnadi aliyekuwa mgombea urais wa Chadema/Ukawa, Edward Lowassa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015..

Humud aipeleka KMC ligi kuu Bara


KMC imeongeza idadi ya timu zinazotokea Dar es Salaam katika Ligi Kuu Bara baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya JKT Mlale waliokuwa vinara wa Kundi B la Ligi Daraja la Kwanza.

Ushindi huo unaifanya KMC kupanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza huku shujaa wake akiwa ni kiungo mkongwe Abdulhalim Humud aliyefunga bao hilo pekee.

Huenda furaha kuu itakuwa kwa kocha Fred Felix Minziro maarufu kama Majeshi ambaye aliipandisha Singida United na sasa amejiunga na KMC na kuipandisha pia.

JKT Mlale iliyokuwa nyumbani ilionekana ina nafasi kubwa zaidi ya kupanda kwa kuwa ndiyo ilikuwa kinara ikiwa na pointi 25 sawa na KMC.


Lakini ushindi huo wa KMC umeifanya ifikishe pointi 28 na kupaa kileleni ikifuatiwa na Coastal Union iliyoshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Mawezi mjini Morogoro. Coastal imemaliza ikiwa na pointi 26 wakati Mlale wanabaki na 25.


KUNDI B
                                P   W   D   L   F   A  GD  Pts
1. KMC                     14   8   4   2   17  13  4    28
2. Coastal Union       14   7   5   2   18   9   9   26
3. JKT Mlale             14   7   4   3   13   7   6   25
4. Polisi Tanzania     14   6   6   2   18   12  6   24
5. Mbeya Kwanza      14   6   4   4   14   10  4   22
6. Mufindi            14   3   4   7   13   21 -8  13

Thursday, 1 February 2018

Papii kuanza kuachia ngoma mfululizo

MKALI wa Dansi Bongo, Johnson Nguza ‘Papii’ amesema kuanzia mwezi huu wa Februari, ataanza kuachia ngoma mfululizo kwani tayari wameshaanza kurekodi nyimbo za kutosha.

Papii alisema mpaka sasa tayari amesha-fanya ngoma nne ambazo amezipika kwa staili tofauti katika dansi la kisasa ambalo halich-oshi.

“Tumefanya staili kama ya wanayofanya Yamoto Band, tumefanya moja kama ya dini na pia tumerudia Seya ambazo kimsingi zitawateka tu mashabiki,” alisema Papii.

Akifafanua zaidi, Papii alisema, atakuwa na mfululizo wa kutoa ngoma mbilimbili zenye ujazo wa hali ya juu.

“Nitakuwa naachia ngoma mbilimbili mfululizo ambazo karibia zote nimefanya na mzee wangu (Nguza). Nimezifanyia katika Studio ya Wanene iliopo Mwenge,” alisema Papii.

Mwana FA: sijawahi kuvaa suruali za kubana

MKONGWE kwenye Muziki wa Bongo Fleva, Hamisi Mwinjuma, ‘MwanaFA’ amesema, katika maisha yake ya kisanii, hajawahi kuvaa suruali za kubana kama ilivyo kwa vijana wenzake wa kileo kwa kile alichodai nguo hizo zinamfanya ashindwe kupumua.

Akipiga stori na Showbiz Xtra, MwanaFA alisema, tamaduni za Muziki wa Hip Hop ndizo zilizomfanya ashindwe kabisa kuvaa suruali za kubana kwa kuwa kila anapojaribu kuvaa hujikuta anashindwa kupumua.

“Unajua nguo zetu sisi watu wa Hip Hop ni ile suruali pana na tisheti kubwa, nimekulia katika mavazi hayo, licha ya kwamba dunia inabadilika lakini mimi nashindwa kabisa kuvaa suruali za kubana kwa kuwa nguo hizo hunifanya nishindwe kuhema,” alisema MwanaFA.

Lulu Diva arudisha mahari kwa mikono yake



MWANAMUZIKI wa kike anayekuja kwa kasi Bongo, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ amerejesha kwa mikono yake mwenyewe mahari aliyokuwa ametolewa na mchumba wake aliyedumu naye kwa takriban miaka mitatu.

Chanzo chetu makini kilisema kuwa, mwanamuziki huyo alikuwa afunge ndoa mwishoni mwa mwaka jana lakini kutokana na kuvuja kwa habari kuwa anatoka na mwanamuziki mwenziye wa Bongo Fleva, mwanaume huyo akadai mahari yake.

“Kama kuolewa basi Lulu angeolewa mwaka jana mwishoni lakini mchumba huyo alibaini anatoka kimapenzi na mwanamuziki mwenzake akaomba mahari yake irudishwe,” kilisema chanzo.

Gazeti hili lilipompigia simu Lulu na kumuuliza madai hayo alisema, ni kweli alirudisha mahari lakini si kwamba mwanaume huyo alijua anatoka na mwanaume mwingine bali alipata shinikizo kutoka kwa ndugu zake.

“Aliposhinikizwa sana nikaona isiwe tabu nikamrudishia mahari yake kwa maana alikuwa akiwasikiliza sana ndugu zake ambao walikuwa hawataki anioe,” alisema Lulu.

Waziri atoa neno kesi kusikilizwa kwa kutumia mtandao

WAKATI mahakama nchini zinatarajia kuanza kusikiliza kesi kwa kutumia mtandao kuanzia mwakani, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema utaratibu huo utasaidia kupunguza gharama.

Waziri Kabudi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam  wakati akihojiwa na waandishi wa habari, baada ya kufungua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na kuongeza kuwa mashahidi watatoa ushahidi wakiwa nje ya mahakama.

Waandishi wa habari walitaka kupata maoni yake kuhusiana na mpango wa mahakama wa kufanya maboresho kwa kuanza kusikiliza kesi kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Mimi mwenyewe sikujua kabisa matumizi ya mtandao hata WhatsApp, nimeanza kutumia hivi karibuni baada ya kuapishwa…  teknolojia yoyote mpya inapokuja ambao ni wagumu kuielewa ni watu wa umri wangu, lakini kwa vijana wanaelewa kwa haraka zaidi,” alisema.

Waziri alisema kuwa utaratibu huo wa mahakama kuingia kwenye mfumo wa Tehama utasaidia kupunguza gharama kwa mfano, kesi ikiwa Dar es Salaam na shahidi yupo Mbeya hatalazimika kusafiri kwa ajili ya kutoa ushahidi.

“Haitatakiwa kutolewa mkoani Mbeya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya ushahidi, atatoa ushahidi wake akiwa Mbeya na jaji ama hakimu ambaye yupo Dar es Salaam atamuona na kumsikiliza,” alisema.

Aliongezea: “Hata kwa maabusu ambao wapo gerezani kwa ajili ya kwenda kuahirisha kesi au maombi ya dhamana hana haja tena ya kwenda mahakamani.”

Hata hivyo, Prof. Kabudi alieleza kuwa kuna haja ya watu kujifunza.  Ni kweli tunahitaji kujifunza zaidi kuhusu matumizi ya mtandao, lakini umuhimu huo ni kwa watu wenye umri mkubwa kuliko vijana, maana vijana mtandao anao mkononi,” alisema. Kabudi alisema teknolojia kwa sasa imesogezwa hadi kwenye simu kwa hiyo mtu anaweza kupata taarifa zake za kesi.

Alisema baada ya muda Watanzania wengi watafurahia mfumo wa mahakama kwa njia ya Tehama kwa kuwa kwa sasa miundombinu ipo pamoja na uelewa, ingawa ni jukumu ya mahakama kuwaelimisha wananchi kuhusiana na utaratibu huo.

Alisema suala hilo ni muhimu na linaendana na wakati, hivyo ni jambo nzuri kuipongeza mahakama kwani mahakama zinakuwa nyuma kwenye mabadiliko, lakini kwa Mahakama ya Tanzania imekuwa mbele ya taasisi nyingi za sheria katika kuleta mabadiliko.

Aidha, aliwataka wananchi wa Kigamboni waitumie mahakama hiyo na kuyatunza majengo hayo ili ya yadumu kwa muda mrefu.

ONYO WASIMAMIZI MIRATHI Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi aliwataka wasimamizi wa mirathi kutojihusisha na mali za urithi na kwamba kazi yao ni kuhakikisha mali zinawafikia wahusika badala ya kujinufaisha.

Waziri Kabudi alisema msimamizi wa mirathi sio mrithi wa mali, kazi yake ni kugawa mali kwa wahusika halali, lakini wengi wao wamekuwa wakijisahau.

”Huyu msimamizi anatakiwa kutoa taarifa mahakamani baada ya miezi sita toka alipoteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi, wengi huwa hawafanyi hivyo na matokeo yake kujiona wao ndio warithi wa mali, nataka wajue kuwa msimamizi wa mirathi  sio mrithi wa mali,” alisisitiza.


Jaji Mtungi atoa onyo kwa Vyama vinavyoshiriki Uchaguzi mdogo

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi, amevikumbusha vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo kuhakikisha vinatii sheria zake, sheria za gharama za uchaguzi na kanuni zake katika kipindi hiki cha uchaguzi mdogo katika Majimbo ya Siha na Kinondoni.

Jaji Mtungi aliyasema hayo kupitia barua aliyoiandikia vyama hivyo juzi kuhusu wajibu wao wa kutii sheria wakati wa uchaguzi huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Monica Laurent, alisema vyama hivyo vimetakiwa kutii sheria hasa kwa kuepuka vitendo vya fujo, lugha za uchochezi na matusi.

“Natambua kuwa vyama vyenu vinashiriki katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani zinazoendelea katika majimbo na kata, hivyo natumia fursa hii pia kuvipongeza vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi huo katika tukio hilo muhimu la kidemokrasia,” ulisomeka ujumbe wa barua hiyo kwa vyama vya siasa.

“Aidha, naviasa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo, kuheshimu na kufuata sheria za nchi, hasa sheria ya vyama vya siasa, sheria ya gharama za uchaguzi na kanuni zake, kwa kuepuka vitendo vya fujo na lugha za matusi na uchochezi,” aliongeza.

Pia Jaji Mtungi alitoa wito kwa wanachama wa vyama vya siasa kutoa taarifa katika mamlaka husika endapo wanashuhudia viashiria vya uvunjifu wa sheria katika kampeni na uchaguzi badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Uchaguzi  katika majimbo ya Kinondoni na Siha unafanyika baada ya wabunge waliokuwapo  kuhama wakitokea vyama vya upinzani vya CUF na Chadema na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia anagombea kupitia CCM baada ya kujiengua kutoka CUF ilhali Siha, Dk. Godwin Mollel, ambaye naye alihama Chadema na kuhamia CCM, anagombea kupitia  chama hicho.

Mwalimu ahama nyumba kupisha Wanafunzi waitumie kama darasa



MWALIMU wa Shule ya Msingi Makazi Mapya, Kata ya Malangali Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ameihama nyumba aliyokuwa akiishi ili kupisha wanafunzi waitumie kama darasa.

Mwalimu huyo, amelazimika kufanya hivyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na vyumba vya madarasa vya kutosha.

Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani wa Kata hiyo, Anthony Chomo, alisema  shule hiyo ilianzishwa mwaka 2003 lakini ina changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.

Chomo alisema mwalimu huyo amehama katika nyumba ya shule aliyokuwa akiishi ili wanafunzi wa darasa la awali wapatao 51, waitumie kama darasa.

Alisema kutokana na uhaba huo wa vyumba vya madarasa, wanafunzi wa darasa la kwanza ambao idadi yao ni 101 pamoja na wengine 67 wa darasa la tatu,  wanalazimika kusoma kwa zamu katika chumba kimoja kwa zamu za asubuhi na mchana.

Diwani Choma alisema kutokana na changamoto hiyo, walimwomba Mbunge wa  Sumbawanga Mjini fedha na kuwapatia Sh. milioni tatu kutoka katika Mfuko wa Jimbo na wameanza ujenzi wa vyuumba vya madarasa ili kutatua tatizo hilo.

Choma alisema wamekwishafikisha suala hilo kwenye uongozi wa Halmashauri ya Manispaa na wanaendelea kusubiri licha ya kuwa imekuwa muda mrefu na mpaka sasa wanafunzi wanasoma kwa shida na walimu wanafundisha kwa shida pia.

Alisema iwapo jitihada hazitafanyika haraka  kujenga madarasa, wanafunzi hawatakuwa na uelewa mzuri kutokana na kusoma kwa shida na walimu pia ufundishaji wao utakuwa hauna kiwango kinachotakiwa, hivyo lengo la serikali la kila mwanafunzi kupata elimu bora litakuwa halijafikiwa.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu, alisema manispaa inasubiri wananchi waanze nguvu kazi ya ujenzi wa madarasa katika shule hiyo ndipo wasaidie umaliziaji.

Njovu alisema iwapo wananchi watatekeleza wajibu huo, shule hiyo itapata madarasa upesi zaidi kwa kuwa halmashauri imepokea fedha kutoka mradi wa kuimarisha elimu ujulikanao Kama P4R, hivyo fedha hizo zitatumika katika kuboresha mazingira ya elimu ya shule hiyo.

Hata hivyo, Njovu alimwomba diwani huyo kuwahimiza wananchi ambao watoto wao wanasoma katika shule hiyo, kuhakikisha wanajituma katika kuboresha mazingira ya elimu ya watoto wao baada ya kukaa na kusubiri wahisani na serikali kwa kuwa yale yaliyo ndani ya uwezo wao, wanapaswa kuyafanya kwa maslahi ya elimu ya watoto wao na taifa kwa ujumla.

Shilole ampa onyo Dada wa kazi

STAA wa filamu na Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amesema kuwa tangu amekuwa mke halali wa Ashraf Uchebe, haruhusu dada wa kazi ampikie chakula mumewe huyo.

Akizungumza na gazeti hili, Shilole alisema kuwa mastaa wengi wakiingia kwenye ndoa wanajisahau sana kila kitu wanapenda kufanyiwa na mdada wa kazi na ndiyo maana ndoa zao hazidumu.

“Yaani mimi lazima mume wangu ale chakula cha mkono wangu sikubali mdada wa kazi ampikie, ni marufuku kabisa. Nimruhusu, je akinogewa na mapishi ya mkono wake inakuwaje? Chakula napika mwenyewe kuanzia chai mpaka cha jioni,” alisema Shilole. wanavyopakaza, huyo uliyepata picha zake ni kweli,” alisema Uwezo.

Nisha achoshwa na Wanaume wa Kitanzania

MSANII wa maigizo na vichekesho Bongo, Salma Jabu ‘Nisha’ amesema kuwa, amekoma kutoa mapenzi yake kwa wanaume wa Kitanzania kwa kuwa wote wana mapenzi ya kuigiza ambayo yamempotezea muda mno.

Akizungumza na Ubuyu, Nisha alisema ameumizwa sana na mapenzi ya Kibongo, hivyo bora kama anataka kuwa na mpenzi ni afadhali atafute mwanaume wa nje na si Mbongo tena.

“Hivi sasa hivi naanzaje kutoka kimapenzi na mwanaume wa Bongo walivyo waongo na walaghai maana nimepoteza muda mwingi kwao lakini hakuna chochote nilichopata zaidi ya fedhea tu,” alisema Nisha ambaye amewahi kutoka na staa wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego.

Dar yakosekana katika mikoa 10 iliyofanya vizuri

    Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetoa mpangilio wa ubora wa ufaulu kimikoa wa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, huku Dar es Salaam ukikosekana katika mikoa 10 iliyofanya vizuri.

Hata hivyo, mkoa huo umepanda kutoka nafasi ya 18 mwaka juzi, hadi nafasi ya 16 mwaka jana. Katika orodha hiyo mkoa wa Kilimanjaro umepanda kutoka nafasi ya tano mwaka 2016 hadi nafasi ya kwanza mwaka jana.

Mkoa wa Pwani nao umepanda kutoka nafasi ya saba mwaka juzi hadi nafasi ya pili mwaka jana. Katika orodha hiyo Tabora imeshika nafasi ya tatu kutoka nafasi ya 10 mwaka 2016.

Mikoa mingine iliyofuata na nafasi iliyoshika ni Shinyanga (nafasi ya nne kutoka nafasi ya tisa), Mwanza (nafasi ya tano kutoka nafasi ya sita).

Mkoa wa Njombe uliokuwa kwa kwanza mwaka 2016, mwaka jana umeporomoka hadi nafasi ya 15.

Mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya pili mwaka 2016, lakini mwaka jana umeporomoka hadi nafasi ya 17 huku Kagera ulioshika nafasi ya tatu, ukishuka hadi nafasi ya tisa.

Mkoa ulioshika mkia katika mpangilio huo ni Kaskazini Unguja uliotoka nafasi ya 29 mwaka juzi hadi nafasi ya 31 mwaka jana, ukifuatiwa na Kusini Unguja ulioshika nafasi ya 30 ambayo pia uliishika mwaka juzi.

Mikoa mitano iliyoshika mkia ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na Lindi.   

Uzinduzi wa hati ya Kielektroniki yaibua mambo 10

 Dar es Salaam. Unaweza kusema uzinduzi wa hati ya kielektroniki ya kusafiria uliofanywa jana na Rais John Magufuli umeibua mambo 10.

Baadhi ya mambo hayo yalizungumzwa na kiongozi huyo mkuu wa nchi katika hotuba yake wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, mengine kuelezewa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Ukiacha ulazima wa Mtanzania kuwa na Kitambulisho cha Taifa na Sh150,000 ili kupata hati hiyo mpya, kuna mambo mengine matano yaliibuka baada ya uzinduzi huo.

Mambo hayo ni sifa za hati hiyo zikiwamo za kuwa na alama nyingi za usalama, kuweza kuhifadhiwa katika programu ya simu ya mkononi “App”, hati za kusafiria za zamani kutumika hadi mwaka 2020, ikiwa mtu ana safari ya dharura na hana Kitambulisho cha Taifa, atapewa hati ya dharura na kuitumia si zaidi ya miaka miwili.

Mengine ni kutokuwapo uwezekano wa kughushi hati mpya, utaratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kutoa vitambulisho, hati mpya kuwa na kurasa nyingi kuliko ya zamani na hivyo kuweza kutumika muda mrefu zaidi na Mtanzania kupata huduma ya haraka katika balozi ikiwa ataipoteza.

Akitoa maelezo kabla ya uzinduzi huo uliofanyika Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini, Dk Makalala alisema mfumo wa uhamiaji mtandao ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji.

Alisema kupitia mfumo huo, Idara ya Uhamiaji imeanza kutoa hati za kusafiria, viza za kielektroniki, vibali vya ukaazi vya kielektroniki na udhibiti wa mipaka wa kielektroniki.

Alisema hati mpya ni ya kisasa ikiwa na alama nyingi zaidi za usalama, ni ngumu kughushi, “Ina kurasa nyingi zaidi ukilinganisha na ya zamani hivyo kumwezesha mtumiaji kuitumia zaidi na kwa muda mrefu.

“Pasipoti hii inamwezesha mtumiaji kuwa na nakala ya pasipoti ya kielektroniki kwenye simu yake ya kiganjani baada ya kupakua ‘app’ ya hati yake ya kusafiria katika simu.”

Alisema Mtanzania anapokuwa na nakala ya hati yake katika simu, itamuwezesha kupata huduma ya haraka katika Balozi za Tanzania nje ya nchi, ikiwa aitapoteza.

Kuhusu utaratibu wa kuipata, Dk Makakala alisema sharti kuu ni lazima mhusika awe na Kitambulisho cha Taifa.

“Nitoe wito kwa wanaoataka kuja kuomba pasipoti mpya waje na kitambulisho cha Taifa ndio sharti muhimu. Pasipoti za kawaida zinazotumika sasa zitaendelea kutumika hadi Januari 2020 kisha zitaondolewa kabisa,” alisema.

Alisema hati za kusafiria za Afrika Mashariki zilizokuwa zikitumika awali, hazitatolewa tena baada ya kuanza kutolewa hati za kusafiria za kimataifa.

Alipotakiwa na Mwananchi kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo mpya, Dk Makakala alisema “Tunaendelea kutoa hati za zamani katika kipindi cha miaka miwili hadi Januari 2020 tutakapositisha. Hatuwezi kusitisha moja kwa moja, tupo katika kipindi cha mpito.”

Alisema ikiwa mtu ana hati ya kusafiria ya zamani na anataka kubadili apate mpya, atalazimika kuambatanisha maombi yake na kitambulisho cha Taifa.

“Tunafanya hivyo kwa sababu kuna taarifa tunahitaji kuzichukua ingawa mhusika tayari tutakuwa na ukaribu naye kwamba tayari si mgeni kwetu,” alisisitiza.

Awali, alisema mradi huo ulianza mwaka 2013 na Septemba 2017 walisaini mkataba na kampuni ya HDI ya Marekani na kwamba hadi kufikia Desemba mwaka huu, mfumo mzima utakuwa umekamilika ikiwa ni pamoja na kuufunga katika balozi za Tanzania zilizo nje ya nchi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba alisema gharama ya kupata hati mpya ni Sh150,000 na mhusika ataitumia kwa kipindi cha miaka 10.

Alipoulizwa kuhusu idadi ya Watanzania waliopata Vitambulisho vya Taifa, msemaji wa Nida, Rose Mdami alisema wengi wamepata.

“Kwa asilimia kubwa Watanzania wengi wamepata vitambulisho na tunaendelea kutoa katika mikoa 20. Lengo letu ikifika Desemba mwaka huu Watanzania wenye sifa wawe wamepata.”

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Rais Magufuli alitoa sababu za kumteua Dk Makakala, Februari 10 mwaka jana, kwamba ni kutokana na matatizo mengi yaliyokuwamo Uhamiaji.

Alisema miaka ya nyuma, Uhamiaji iligubikwa na matatizo mbalimbali ikiwamo utoaji ovyo wa vibali vya uraia hata kwa watu ambao hawakuwa na sifa za kupata uraia.

“Kuna raia wengi walipata uraia bila sifa na wapo waliopata uraia na vyeo vya juu kabisa serikalini. Hii ndiyo sababu niliamua kumteua mwanamama kuongoza idara hii muhimu na wanawake ni waaminifu sana, ameanza kutatua matatizo haya,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alimwagiza kamishna huyo kuwachukulia hatua kali, ikiwamo kuwavua vyeo watumishi wa Uhamiaji ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti wahamiaji haramu.

“Haiwezekani wahamiaji haramu wanakamatwa Mbeya halafu wamepita Kilimanjaro, Manyara, wamepitaje kote huko hadi wakafika Mbeya? Au wamepita Chato (Geita), Buboka (Kagera) hadi Singida, huko walikopita hakuna watu?” alihoji.

Kuhusu mchakato wa mfumo huo wa utoaji hati mpya, Rais Magufuli alisema umegharimu Sh127.2 bilioni ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Sh400 bilioni.

“Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Sh400 bilioni, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu,” alisema.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.

Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.