Friday, 19 January 2018

Kenya: Daktari ataka ukeketaji uhalalishwe

Daktari mmoja nchini Kenya amewasilisha kesi mahakamani akitaka upashaji tohara wa wanawake ambao hufahamika pia kama ukeketaji uhalalishwe.

Dkt Tatu Kamau anasema sheria inayoharamisha ukeketaji wa wanawake na wasichana inakiuka utamaduni katika jamii nyingi za Kiafrika.

kadhalika, amesema ni ubaguzi dhidi ya wanawake ikizingatiwa kwamba upashaji tohara wa wanaume unakubalika kisheria.

Daktari huyo anataka pia bodi ambayo iliundwa nchini humo kukabiliana na upashaji tohara wa wanawake ivunjiliwe mbali.

Aliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama Kuu mjini Machakos, mbele ya jaji David Kemei.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mwezi ujao.

Dkt Kamau, akizungumza na wanahabari baada ya kuwasilisha kesi yake, alisema wanawake wote, sawa na watu wazima popote pale, wanafaa kuruhusiwa kufanya uamuzi kuhusu miili yao wenyewe bila kuwekewa vikwazo na sheria.

Amesema ukeketaji ni neno ambalo lilitetwa na watu kutoka nchi za Magharibi

Lakini sasa amesema raia wa nchi za Magharibi wanafanya jambo sawa na ukeketaji, kufanya upasuaji kwenye uke kurekebisha maumbile.

"Upashaji tohara ulikuwa sehemu ya utamaduni wa Waafrika kabla ya kufika kwa wakoloni na haifai kuharamishwa," amesema.

"Punde tu itakapohalilishwa, tutaweza kufanya tohara kwa njia iliyo bora Zaidi, mojawapo ikiwa njia ya hospitali. Tukifanya hivyo basi itakuwa salama kabisa. Na njia hii ni mojawapo wa upasuaji wa kawaida duniani kote."

Anasema wanawake wengi wamekuwa wakisumbuliwa na maafisa wa dola au hata kufungwa jela kwa sababu ya ukeketaji.

"Ingawa tunataka sana kumlinda mtoto msichana, kuna wanawake wengi sana ambao wamekamatwa na kufungwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita," anasema.

"Unapokuwa mtu mzima, hakuna sababu yoyote ya kuzuia kufanya uamuzi (iwapo ungependa kupashwa tohara)" alisema.

Takwimu muhimu kuhusu ukeketaji Kenya

Asilimia 21 ya wanawake wa umri wa kati ya miaka 15-49 Kenya wamepashwa tohara

Kuna ushahidi kwamba siku hizi, wasichana wamekuwa wakikeketwa wakiwa na umri mdogo.

Asilimia 28 ya wanawake wa miaka 20-24 walikeketwa wakiwa na miaka 5-9, ikilinganishwa na asilimia 17 ya wanawake wa miaka 45-59.

Kuhusu aina ya ukeketaji, asilimia 2 ya wanawake wa miaka 15-49 hawakutolewa sehemu yoyote kwenye uke wao, asilimia 87 walikatwa na kuondolewa sehemu fulani, nao asilimia 9 walikatwa kisha kushonwa.

Wasichana wa miaka 0-14 wana uwezekano wa juu wa kukeketwa ikiwa mama zao wamekeketwa.
Wanawake na wanaume asilimia 11 huamini kwamba ukeketaji unahitajika kwa mujibu wa jamii yao au dini na kwamba unafaa kuendelea.

Chanzo: Takwimu ya Utafiti kuhusu Afya na Watu Kenya ya mwaka 2014

Dkt Kamau alisema jamii nyingi zimekuwa zikifanya upashaji tohara kwa njia nyingi na kwamba si aina zote za tohara hiyo ambayo ina madhara kwa mwanamke.

Alisema sawa na jinsi watu huonywa dhidi ya athari za uvutaji sigara au ungwaji pombe, kampeni ya kuwahamasisha watu kuhusu madhara ya ukeketaji inafaa kuendelea lakini wale wanaoamua au wangependa kupashwa tohara wanafaa kuruhusiwa.

Dkt Kamau ameshutumu hatua ya Bunge nchini Kenya la kupitisha sheria ya kuharamisha ukeketaji akisema Bunge lilivuka mipaka na kuingilia masuala ya utamaduni.

"Iwapo wanaweza kuharamisha utamaduni, kesho wataharamisha dini au kitu kingine. Dada anastahili kutetewa akifanya maamuzi yake, na wala si kulazimishwa kufanya mambo mengine," amesema.

Makundi yanayokabiliana na ukeketaji yameshutumu hatua ya Dkt Kamau.

Mwenyekiti wa bodi ya kukabiliana na ukeketaji Bernadette Loloju amesema ukeketaji hupingwa kwa sababu ya madhara yake kwa wanawake, hasa wakati wa kujifungua.

Amesema kampeni hiyo imefanikiwa kupunguza visa vya ukeketaji kutoka asilimia 37 mwaka 2008 hadi 21 mwaka 2014 kwa mujibu wa takwimu za serikali.

Kwa sasa hata hivyo, ukeketaji hutekelezwa kisiri.

Watoto wamekuwa pia wakipashwa tohara wakiwa wadogo kinyume na zamani ambapo ulifanywa wasichana wakibalehe.

Wasichana takriban 140 milioni wamekeketwa maeneo ya Afrika, Mashariki ya Kati na Bara Asia.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo pia zimeathiriwa pakubwa na ukeketaji wa wasichana.

Inakadiriwa kwamba nchini Tanzania, wasichana na wanawake 7.9 milioni wamekeketwa.

Kwa nini imekuwa vigumu kukabiliana na ukeketaji?
Katika baadhi ya jamii Afrika Mashariki, ni utamaduni unaoathiri hadhi ya mwanamke katika jamii. Baadhi ya jamii, mwanamke haruhusiwi kuolewa au kutangamana na wasichana wengine wa rika lake iwapo hatapashwa tohara.

Katika jamii ya Wamaasai kwa mfano, mwanamke huwa na wakati mgumu kuthibitisha kwamba yeye ni mwanamke kamili iwapo hajapashwa tohara.

Aidha, watoto wake huchukuliwa na jamii kama wasiokubalika.

Sherehe ambazo huambatana na upashaji tohara na wazazi wa msichana kutambuliwa kama wazee katika jamii iwapo binti mabinti wao wamepashwa tohara huwafanya kutaka sana mabinti wao wakeketwe.

SOURCE: BBC

Wamiliki wa Mabasi waomba kukutana na Rais Magufuli

WAMILIKI wa mabasi yaendayo mikoani, wameomba kukutana na Rais John Magufuli kumweleza matatizo yanayowakabili ikiwamo  vipengele wanavyodai kuwa ni kandamizi katika kanuni mpya za leseni za usafirishaji.

Wamefikia hatua  hiyo baada ya kutofikia mwafaka katika kikao kilichofanyika jana  jijini Dar es Salaam kati yao  na maofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa  Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, na Jeshi la  Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akitangaza azimio hilo kwa niaba ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi hayo (Taboa), Enea Mrutu, alisema wataandika barua kuomba kukutana na Rais  Magufuli ili kumweleza matatizo yanayowasibu.

"Tukimaliza kikao hapa na kwa kuwa wote mmekubali na mnataka kukutana na Rais  Magufuli, sekretarieti itakutana tutaandika hiyo barua na tutaipeleka nyumba nyeupe (Ikulu)," alisema Mrutu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taboa , Mohammed Hood, alisema kabla ya kuandikia barua ya kuomba kukutana na Rais, watafanya utaratibu wa kuonana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

"Hatuwezi kufika kwa Rais  moja kwa moja bila  kupitia kwa Waziri, hivyo mimi  nitampigia Waziri ili nimwombe tuonane na baada ya hapo ndipo  tutakwenda  Ikulu," alisema Hood.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, alisema hakuna uadui kati ya Sumatra na wamiliki wa mabasi na kwamba suala la faini inayotozwa kuanzia Sh. 250,000 hadi 500,000 haliwezi kuingiliwa kwa sasa kwa sababu ni la  kisheria.

"Jambo hili litafutiwe namna nyingine ya kuzungumza kwa sababu lipo kisheria. Hakuna mmiliki atakayeshitakiwa  au kupelekwa mahakamani kwa kosa la  gari kwenda kasi, dereva ndiye atakayeshitakiwa," alisema Kahatano.

Kahatano aliwataka Taboa kwenda Tume ya Ushindani kulalamika endapo wanaona kanuni au sheria hizo mpya zinawakandamiza.

Kuhusu  kuzuia gari kwa kosa la  dereva, Kahatano alisema sheria ya Sumatra inasema endapo gari litakamatwa, mmiliki wa gari atapewa siku 14 za kulipa faini hiyo na endapo siku hizo zikipita bila kulipa, mmiliki anaweza kufika Polisi au Sumatra na kutaka kesi iende mahakamani.

Alisema hakuna gari lolote litakalozuiwa kwa kosa alilofanya dereva na kwamba makosa ya dereva na mmiliki yametenganishwa.

Wakichangia katika mkutano huo, wajumbe wa Taboa wengi wao  walilamikia kanuni zilizokuwapo katika leseni za usafirishaji kuwa zinawakandamiza, huku wakipendekeza faini za viwango vipitiwe upya pamoja na makosa ya dereva na mmiliki yatenganishwe.

Mwanamke aokotwa akiwa amekatwa matiti

KAMANDA WA POLISI MKOA WA KAGERA, AGUSTINE OLLOMI.

MWILI wa Betia Felix (18) mkazi wa Kijiji cha Nyakatete, wilayani Kyerwa mkoa wa Kagera, umeokotwa ukiwa umekatwa matiti na kufungwa kamba miguuni.

Marehemu huyo, alionekana kichakani Ijumaa iliyopita saa 4:00 asubuhi karibu na maeneo ya mashamba ya wanakijiji hicho baada ya ndugu kutokumwona nyumbani kwao kwa muda wa siku saba na kutoa taarifa ofisi za kijiiji.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Josephat Mtayoba, alisema baada ya kupokea taarifa za binti huyo na kuwasiliana na ndugu wa marehemu walisema wakati akiondoka alikuwa anawasiliana na watu ambao ndugu zake hawakuwafahamu.

"Kwa kijiji hiki ni tukio la kwanza kushuhudia mauaji ya kushtua kama hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kuweka na kuimarisha ulinzi shirikishi, "alisema Mtayoba.

Baba wa marehemu huyo Felix Gabriel , alisema binti yake, alitoka shambani akiwa na jembe na kuliweka nyumbani kisha kuondoka akiwa anaongea na simu, lakini hakufahamu alikuwa akiongea na nani.

Aidha alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu akiwa haonekani nyumbani alidhani kuwa mwanae atakuwa ameolewa hivyo anasubiri kupokea mahari kutoka kwa wakwe.

“Aliondoka nyumbani tangu Januari 5, mwaka huu na mwili wake kuokotwa na mdogo wake mchunguzi Felix Ijumaa iliyopita Januari 12 mwaka huu,”alisema Gabriel.

"Nilivyoona anaondoka sikushtuka kwani nilijua atarudi na alivyokaa siku nyingi nilidhani atakuwa ameolewa nilijipanga kupokea mahari ya binti yangu, "alisema Gabriel kwa uchungu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustine Ollomi, alithibitisha tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta wahalifu hao na kwamba hakuna aliyenaswa.

Kipimo cha kutambua aina tofauti za saratani chagundulika

Wanasayansi wamepiga hatua kubwa katika matibabu ya binadamu kwa kupata kipimo cha damu kinachogundua aina tofauti za Saratani.

Timu ya Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins wamefanyia utafiti njia ambazo zinaweza kugundua aina nane zinazosababisha ugonjwa huo.

Watafiti hao kutoka Uingereza wanasema mtu anapaswa kufanyiwa uchunguzi kwa mwaka, ili kuweza kugundua ugonjwa wa Saratani mapema na kuweza kuokoa maisha yake. Huku wakisifia matokeo ya utafiti wao.

Uvimbe hutokea na kuonesha dalili kwamba ni ugonjwa wa Saratani hutoa viashiria vidogo vya vinasaba -DNA- zilizobadilika pamoja na protein kwenye mfumo wa damu.

Uchunguzi wa kutafuta saratani unatafuta mabadiliko ya vinasaba 16 ambavyo hutokea mara kwa mara katika saratani, na proteni nane ambazo huwa ni viashiria vya hali ya mgonjwa.

Utafiti huo ulifanyiwa majaribio kwa wagonjwa 1,005 wenye Saratani katika ini, tumbo, mirija ya uzazi, mapafu na maeneo mengine mbalimbali ambayo bado ugonjwa huo haujaenea katika maeneo mengine.

Kwa ujumla vipimi vya utafiti huo hupata asilimia 70 ya Saratani.

Akizungumza na BBC Dokta Cristian Tomasetti kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins amesema hatu ya kutambua ugonjwa wa Saratani mapema ni muhimu na matokeo ni ya kusisimua.

Saratani inapogundulika mapema inakuwa na nafasi kubwa ya kuweza kuitibu.

Wataalamu wanasema pia kwa baadhi ya wagonjwa matibabu yanaweza kuwa mabaya zaidi kuliko kuishi na saratani yenyewe ambayo haiatarishi haraka maisha.

Wizara kuomba kubali cha Kuajiri



NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile, amesema wizara yake imeanza kukabiliana na changamoto ya watumishi wa Afya kwa kuomba kibali cha kuajiri.

Dk. Ndungulile alitoa kauli hiyo jana alipokuwa ziarani mkoani Mbeya baada ya kupokea taarifa ya wafanyakazi wa idara hiyo kutoka kwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa, Elesia George, unakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa idara hiyo.

Elesia alisema upungufu huo wa watumishi umepelekea vituo vya Afya na Zahanati za Serikali 59 mkoani humo kuongozwa na wauguzi kutokana na kutokuwa na madaktari.

Alisema hali hiyo inahatarisha afya za wananchi kutokana na uwezo mdogo wa wauguzi hao usioendana na majukumu wanayopewa.

Alisema uhaba wa watumishi hao unapelekea wauguzi wanaopewa majukumu hayo kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na hivyo kuwapunguzia ufanisi wa kazi.

Aliomba Serikali iajiri watumishi wa kada hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia mzigo wauguzi ambao wanapewa majukumu wasiyokuwa na uwezo wa kuyamudu.

“Ili huduma za afya ziwe bora ni vizuri tukawa na professionals (wanataaluma), kwenye mkoa wetu tuna upungufu mkubwa wa matabibu hivyo unakuta wauguzi wanafanya kazi zote, tunaomba kwenye kama kuna ajira mpya tunaomba kada hii izingatiwe,” alisema Elesia.

Baada ya maelezo hayo ya Muuguzi Mkuu wa Mkoa, Naibu Waziri Dk. Ndugulile alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, lakini akasema wizara yake tayari imeshaanza kuchukua hatua kwa kuomba kibali cha kuajiri watumishi wapya.

Alisema wanakusudia kuajiri watumishi hasa kwenye maeneo nyeti ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya Afya nchini na hata kuwapunguzia kazi baadhi ya watumishi ambao wana majukumu mengi wakati mwingine.

“Wekeni masanduku ya maoni kwenye maeneo yote ambayo yana mkusanyiko mkubwa wa watu, ili mjuwe malalamiko ya wananchi na myashughulikie na yale mnayoshindwa mnayaleta wizarani tunayashughulikia,” alisema Dk. Ndugulile.

Pia Dk. Ndungulile alisema Serikali inafanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha inaimarisha afya za wananchi hivyo akaeleza kuwa juhudi hizo bila watumishi wa afya wa kutosha hazitakuwa na maana.

Alisema kwa sasa juhudi kubwa zimeelekezwa kwenye ujenzi wa vituo vya Afya na zahanati nchini ikiwa ni harakati za kuimarisha afya ya msingi kwa wananchi wake.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mbeya, Aika Temu, alisema kada hiyo hapa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi na hivyo kufifisha jitihada za kuhamasisha wananchi kwenye shughuli za maendeleo.

Alisema mkoa mzima wa Mbeya wenye wilaya tano na halmashauri saba una maofisa ustawi wa jamii 39 pekee, hivyo akaomba pia Serikali kuimulika idara hiyo wakati wa kuajiri watumishi wapya.

New Zealand: Waziri mkuu afunguka kuwa na ujauzito

Waziri mkuuwa New Zealand mwenye umri wa miaka 37 Jacinda Ardern asema ana ujauzito
Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amefichua kwamba yeye ni mjamzito.

Bi Ardern alisema kwamba yeye na mpenzi wake Clarker Gayford walikuwa wakitarajia mwana wao mwezi Juni ambapo baadaye atachukua likizo ya wiki sita.

''Na tulidhani kwamba mwaka 2017 ni mwaka mkuu'', aliandika katika mtandao wake wa Instagram.

Bi Ardern mwenye umri wa miaka 37 alikuwa waziri mkuu mwenye umri mdogo nchini New Zealand tangu 1856 akiungwa mkono wakati alipotangaza kuhusu hali yake mpya siku ya Ijumaa.

Chama cha leba cha Bi Ardern kilikuwa cha pili katika uchaguzi wa mwezi Septemba ambapo hakuna chama kilichofanikiwa kupata wingi wa kura.

Aliunda serikali kupitia usaidizi wa Winston Peters ambaye ni kiongozi wa chama kidogo cha New Zealand.

''Nitakapokuwa ugenini Bwana Peters atakuwa kaimu waziri mkuu, akifanya kazi na ofisi yangu mbali na kuwasiliana nami'', alisema bi Ardern katika taarifa ilioripotiwa na gazeti la New Zealand Herald siku ya Ijumaa.

''Nitawasiliana na kupatikana katika kipindi hicho cha wiki sita wakati nitakapohitajika''.

Bi Ardern alisema kuwa aligundua kwamba ni mjamzito siku sita kabla ya kujua kwamba atakuwa waziri mkuu , na lilikuwa swala la kushangaza.

''Mimi sio mwanamke wa kwanza kufanya kazi mbili.Sio mwanamke wa kwanza kufanya kazi huku nikihudumia mwanangu, kuna wanawake wengi ambao wamekuwa katika hali kama hii awali'', alisema.

''Bwana Gayford atakuwa baba ambaye atakuwa akisalia nyumbani'', aliongezea.

Mawaziri 2 wakuu wa zamani nchini humo walikuwa watu wa kwanza kutoa pongezi zao.

Ndege yatetemeka angani

Ndege moja ya Malaysia ililazimika kutua katika eneo la Australia ya kati baada ya tatizo la kiufundi kuifanya kuanza kutetemeka ikiwa angani, wamesema abiria.

Ndege hiyo aina ya MH122 ilikuwa inasafiri kuelekea Kuala Lumpur kutoka Sidney siku ya Alhamisi wakati iliporudi katika eneo ambalo haliko mbali na Broome, kaskazini Magharibi mwa Australia.

Ndege hiyo iliokuwa ikiwabeba watu 224 ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Alice Springs Airport.

Abiria wanasema kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitetemeka na kutoa sauti kubwa.

Katika taarifa yake, kampuni ya ndege ya Malaysia Airline ilisema kuwa ndege hiyo ilibadilsha safari kutokana na tatizo la kiufundi.

Hatahivyo haikusema ni matataizo gani. Abiria Sanjeev Pandev alisema kuwa ndege hiyo ilionekana kuwa na tatizo hilo saa nne kabla ya safari kuanza.

''Ilikuwa ikitetemeka na kelele zilikuwa kubwa '', aliambia BBC.

''Watu walikuwa wakiomba na wengine walikuwa wakitokwa na machozi'', aliambia BBC.

Alisema kuwa abiria walionyeshwa njia za kubaliana na dharura na wafanyikazi wengi wao wakionekana kuogopa na kushtuka.

Simba kukutana na waliokwamisha mipango

Vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC leo alfajiri wameondoka kwa ndege kuelekea mjini Bukoba mkoani Kagera kwaajili ya mchezo wao wa raundi ya 14.

Simba ambayo jana ilishinda mchezo wake wa raundi ya 13 kwa mabao 4-0 dhidi ya Singida United kwenye uwanja wa Uhuru, inakwenda kukutana na Kagera Sugar ambayo ilikwamisha mipango yake ya ubingwa msimu uliopita.

Kagera Sugar ilitibua mipango hiyo April 2 mwaka jana baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa uwanja wa Kaitaba hivyo kuinyima nafasi ya kurejea kileleni ikibaki na alama 55 katika nafasi ya pili na kuwaacha Yanga wakiwa na alama 56 kileleni.

Endapo Simba ingeshinda mchezo huo ingefikisha alama 58 hivyo huenda ingetwaa ubingwa kutokana na bingwa wa msimu uliopita kupatikana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, baada ya timu hizo mbili za Kariakoo kufungana pointi.

Simba ambayo kwasasa inaongoza ligi kwa alama 29 mbele ya Azam FC yenye alama 27, itashuka dimbani Kaitaba siku ya Jumapili.


Thursday, 18 January 2018

Audio | Jacko Beatz Ft Moni Centrozone – Baby | Mp3 Download

Audio | Jacko Beatz Ft Moni Centrozone – Baby | Mp3 Download
Audio | Jacko Beatz Ft Moni Centrozone – Baby | Mp3 Download

Batuli awataka mastaa kumrudia Mungu


Yobnesh Yusuph ‘Batuli’.

MSANII mwenye mvuto Bongo Muvi, Yobnesh Yusuph ‘Batuli’ amewasihi wasanii wenzake wajaribu kumrudia Mungu japo mara moja kwa wiki.

Akizungumza na Showbiz Xtra, Batuli alisema kuwa anatambua mastaa wengi wamesahau kusali kabisa na kujua kama kuna Mungu huku wakiendelea kufanya vingi vya kidunia.

“Jamani hakuna kitu kizuri kama kuona staa akiwa kanisani au msikitini yaani hata jamii inakuchukulia kwa mtazamo wa tofauti kabisa, tumrudie Mungu,” alisema Batuli.


Picha ya Selfie kwenye Facebook yasababisha muuaji kupatikana Canada


Mkanda unaovaliwa na Cheyenne Antoine (kushoto) unaonekana kwenye picha na rafiki yake Brittney Gargol

Mwanamme mmoja nchini Canada amepatikana na hatia ya kumuua rafiki yake baada ya polisi kugundua kuwa kifaa kilichotumiwa kuua kilichokuwa kwenye picha ya kujipiga (selfie) ya wawili hao iliyokuwa katika mtandao ya kijamiii.

Cheyenne Rose Antoine, 21, alikiri siku ya Jumatatu kumuua Brittney Gargol, 18, Machi mwaka 2015.

Gargol alipatikana amenyongwa karibu na Saskatoon, Saskatchewan, huku mkanda wa Antoine ukiwa kando na mwili wake.

Antoine alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa mauaji

Alitajwa kama mshukiwa baada ya kuchapisha picha ya selfie kwenye mtandao wa Facebook, ikionyesha amevaa mkanda uliotumika saa kadhaa kabla ya Gargol kuuliwa.

Alisema walikuwa wamekunywa pombe na pia wakavuta bangi kabla kuanza kuzozana.

Polisi wanasema kuwa taarifa ambayo alikuwa amewapa, kuwa Gargol aliondoka na mwanamume mmoja huku naye akionda kumuona shangazi yake.

Ndipo wakatumia picha zake za Facebook kufuatilia mienendo ya wawili hao usiku huo.



Hii ndio Treni inayobweka kama mbwa ili kuwafukuza swara kwenye reli



Watafiti nchini Japana wameiwekea treni kipasa sauti ambacho kinabweka kama mbwa na kutoa mlio wa swara ili kuzuia treni kugonga swara njiani.

Gazeti la Asahi Shimbun lilisema kuwa sauti hizo zinatumiwa kuwafukuza swara kutoka kwa reli kwa lengo la kupunguza idadi ya wanaogongwa na kuuawa na treni.

Maafisa kutoka kwa taasisi ya reli wanasema kuwa mlio wa sekunde tatu wa swara humfanya swara kuwa makini na kusikiliza, ukifuatiwa na sekunde 20 za mbweko wa mbwa, inaweza kusababisha swara kukimbia.

Watafiti wanasema kuwa majaribio ya usiku wakati swara wanakusanyika kando ya reli yamesababisha swara hao kupungua.

Swara hukaribia reli nyakati za usiku kulamba chuma za reli wakitafuta virutubishi muhimu vya madini ya mwili.

Wizara ya uchukuzi nchini Japan inasema kuwa kulikuwa na visa 613 vya treni kugonga swara na wanyama wengine mwaka 2016.

Abiria wasota Kivukoni


Dar es Salaam. Abiria wanaotumia kivuko eneo la feri wamejikuta wakisota kituoni hapo leo Alhamisi baada ya kivuko kikubwa cha MV Magogoni kupata hitilafu hivyo kubaki vivuko viwili ambavyo vinabeba idadi ndogo ya abiria.

Mwananchi ilifika eneo la kivukoni na kukuta msongamano mkubwa wa abiria wakiwa wanasubiri usafiri huo na wengine wakiamua kuondoka kutokana na kusubiri kwa muda mrefu.

Mmoja wa wasimamizi wa ufundi aliejitambulisha kwa jina moja la Ndunguru amesema tatizo hilo limeanza toka usiku kutokana na MV Magogoni kubeba idadi kubwa ya abiria lazima usumbufu ujitokeze.

“Tatizo limeanza tangu usiku ingawa mimi sio msemaji ila unavyoona mafundi wanaendelea na kazi kuhakikisha tatizo linaisha, kivuko hiki ni kikubwa na kinabeba idadi kubwa ya abiria hivyo kikiaribika lazima usumbufu ujitokeze,” amesema Ndunguru.